Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Habari

DSE yavunja rekodi, yafikisha mtaji wa trilioni 40/-

Moja ya nguzo kubwa kwa Watanzania kumiliki uchumi wao, ni kupata fursa ya kuwekeza kwenye masoko ya hisa. Hivi sasa DSE imeongeza mtaji, vyema kila Mtanzania kuchangamkia.

Alhamisi, 8 Oktoba 2026 · 07:12Dakika 2 kusomaToleo 182, uk. 16
Mkurugenzi Mtendaji wa DSE, Peter Nalitolela.
Mkurugenzi Mtendaji wa DSE, Peter Nalitolela. — Picha na Mpigapicha Wetu

SOKO la Hisa la Dar es Salaam (DSE) limeandika historia kubwa kwa kufikia kiwango cha juu cha mtaji cha Shilingi trilioni 40.

Hatua hiyo inadhihirisha kuongezeka kwa thamani ya kampuni zilizoorodheshwa na imani ya wawekezaji katika soko la mitaji nchini.

Thamani ya jumla ya kampuni zote zilizoorodheshwa DSE ilifikia rekodi ya Shilingi trilioni 40.3 mnamo Septemba 10, 2026, ikilinganishwa na Shilingi trilioni 38.74, kilichokuwa kiwango cha juu kilichorekodiwa Agosti 28 mwaka huu.

Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa mnamo Septemba 10, 2025, mtaji wa jumla wa DSE ulikuwa Shilingi trilioni 21.73, ikimaanisha kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja, soko hilo lilishuhudia ongezeko la takribani Shilingi trilioni 18.57, sawa na asilimia 85.5.

Wataalamu wa soko la mitaji wanasema kuvuka kwa kiwango hicho kunaashiria kukua kwa nafasi ya DSE katika uchumi wa Tanzania, hasa katika kuchochea upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu kwa kampuni na kutoa fursa zaidi kwa wawekezaji kushiriki katika ukuaji wa biashara.

Hatua hiyo pia inakuja wakati Tanzania inaanza kutekeleza Dira ya Maendeleo ya 2050, ambayo inaweka sekta binafsi katika nafasi muhimu katika kufadhili mabadiliko ya kiuchumi yanayolenga kuifanya nchi kuwa na uchumi wa thamani ya dola trilioni moja.

NMB yainua kiwango cha soko Miongoni mwa kampuni zilizochangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa thamani ya DSE ni Benki ya NMB, ambayo sasa imeingia katika kundi jipya la kampuni zenye thamani ya zaidi ya Shilingi trilioni 10.

NMB ilikuwa kampuni ya kwanza iliyoorodheshwa DSE kuvuka kiwango hicho baada ya bei ya hisa zake kufikia Shilingi 2,130 mnamo Agosti 28 mwaka huu na kuipa benki hiyo mtaji wa soko wa takribani Shilingi trilioni 10.65.

Mkurugenzi Mtendaji wa DSE, Peter Nalitolela, amesema mwenendo huo unaonyesha kuimarika kwa imani ya wawekezaji kwa kampuni zilizoorodheshwa nchini na kuvutia zaidi kwa soko la Tanzania. Kwa mujibu wa Nalitolela, ongezeko kubwa la thamani ya NMB baada ya mgawanyo wa hisa kwa uwiano wa 1:10 limekuwa miongoni mwa vichocheo muhimu vya kupanda kwa thamani ya jumla ya DSE.

Soma Pia