Habari Kuu
Dunia yatilia shaka hukumu ya Lissu
Tundu Lissu aliyeibwaga serikali kwenye kosa la uhaini, lakini akatiwa hatiani kwa kosa la uchochezi, sasa ana siku ya pili akiwa gerezani. Hukumu yake imezua mgongano wa kimantiki, mazingira na sheria yenyewe. Soma namna dunia ilivyoipokea.

HUKUMU ya kifungo cha miaka minne jela iliyotolewa na Mahakama Kuu kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, imezalisha gumzo na mijadala karibu duniani kote.
Kinachojadiliwa na hata kuandikwa kwa barua, waraka na ujumbe kwenye mitandao ya jamii, kinabeba ujumbe wa kutilia shaka hukumu ya Lissu
Hukumu hiyo ilitolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam Novemba 6, 2026.
Taasisi na mashirika ya kimataifa, watu mashuhuri, vyama vya siasa vimetoa mtazamo wao kuhusu hukumu hiyo, huku uzito ukiwekwa kwenye kapu la shaka kwamba huenda kuna "shinikizo la siasa."
Maoni ya wengi yanajikita katika madai kwamba mazingira ya sasa ya kuendesha siasa nchini Tanzania yamegubikwa na "mkono wa chuma wa dola" kukwamisha ustawi wa siasa za ushindani, huku vyama vya upinzani, hasa Chadema kikibinywa zaidi.
Mbali na kunyooshea kidole kwa madai ya kutumika kwa dola kukwamisha upinzani, pia baadhi wanatuhumu mahakama kuwa njia nyingine ya kukandamiza wapinzani, ingawa madai haya yamekuwa yakikanushwa na serikali.
Katika hukumu hiyo ya Lissu, pamoja na kuonekana kubeba mjadala mzito kuhusu hati ya mashitaka kuwa na kosa la uhaini, ambalo mahakama haikuona hatia, bali kosa la uchochezi halikuwa kwenye hati hiyo.
Hukumu hiyo ya Lissu ilielezwa na majaji kwamba ilitolewa kwa mtuhumiwa ikiwa ni kosa dogo lililobainishwa na mahakama ndani ya kosa kubwa lililobebwa na hati ya mashitaka.
Bunge la Ulaya (EU)
Taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Ulaya, David McAllister iliyotolewa juzi - Jumamosi Novemba 7, 2026, imekosoa kitendo cha kumfungulia Lissu mashitaka ya uhaini kutokana na matamshi aliyotoa katika mkutano wa kisiasa, akidai mageuzi ya kisheria ili kuufanya uchaguzi kuwa huru na wa haki.
McAllister amesema kesi ya aina hiyo ni kizuizi kikubwa na kisicho na uwiano dhidi ya uhuru wa kujieleza, ambacho hakiwezi kuhalalishwa kwa namna yoyote.
“Kumshitaki na kumwandama mwanasiasa wa upinzani ni shambulio la moja kwa moja dhidi ya misingi ya demokrasia na haki ya msingi ya kutoa maoni yanayopingana na msimamo wa mamlaka,” inasema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imesema kuwa Lissu kuwekwa mahabusu kwa zaidi ya mwaka mmoja ni moja ya matukio yaliyobainishwa na Kundi Kazi la Umoja wa Mataifa kuhusu watu wanaozuiliwa kiholela nchini, jambo linalozidi kuonesha kutokuwapo kwa haki katika shauri lake.
“Jana (Ijumaa), Mahakama ya Tanzania ilimtia hatiani Tundu Lissu kwa kosa la uchochezi na kumwachia huru dhidi ya shitaka la uhaini. Lissu ni miongoni mwa waliowania tuzo ya Sakharov mwaka huu, jambo linaloonyesha kutambuliwa na Bunge la Ulaya kwa mapambano yake ya ujasiri katika kutetea uhuru wa mawazo na misingi ya kidemokrasia”amesema McAllister.
Ameainisha kuwa yaliyojiri yanadhihirisha kuwa kesi hiyo haikuwa na msingi wa haki na ilikuwa na misukumo ya kisiasa, ikithibitishwa na Lissu kuwekwa mahabusu kwa zaidi ya siku 500 kwa kosa ambalo hakulitenda.
Kupitia azimio lake, Novemba 27, 2025, Bunge la Ulaya lililaani hatua za Lissu kufunguliwa kesi ya uhaini, kuzuiliwa kwake kiholela na kwa misingi ya kisiasa na kutaka aachiliwe huru mara moja na bila masharti yoyote.
Wanasheria Marekani waibuka
Chama cha Wanasheria nchini Marekani (ABA), kupitia Kituo chake cha Haki za Binadamu (ABA CHR), kimeainisha mfululizo wa mapungufu makubwa ya kisheria katika hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania dhidi ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.
Katika tathmini yake iliyotolewa Novemba 2026, ABA CHR imebainisha kuwa ingawa mahakama ilimuondolea Lissu shtaka la uhaini (treason) kosa linaloweza kupelekea adhabu ya kifo na lililomfanya akae mahabusu kwa zaidi ya miezi 18 ilimtia hatiani kwa kosa la uchochezi chini ya Kifungu cha 390 cha Sheria ya Makosa ya Jinai na kumhukumu kifungo cha miaka mine jela.
Kituo hicho kimesisitiza kuwa hatua ya kumtia hatiani kwa kosa ambalo halikuwepo kabisa kwenye hati ya mashtaka ya awali inaibua utata mzito wa kiutaratibu na kuminya haki ya msingi ya mtuhumiwa kujitetea.
ABA CHR imeeleza kuwa mapungufu haya mapya yanashabihiana na kasoro ilizoainisha kwenye ripoti yake ya Aprili 2026, Preliminary Analysis of Fair Trial Issues: Case against Tundu Lissu (Tanzania).
Katika ripoti hiyo, wanasheria hao wa Marekani walikosoa vikali matumizi ya mashahidi wa siri waliotoa ushahidi wakiwa ndani ya masanduku ya mbao yaliyofungwa, hatua iliyomnyima Lissu na mawakili wake uwezo wa kutathmini uaminifu wa mashahidi hao—misingi inayoviuka Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kisiasa na Kijamii (ICCPR).
Amnesty International
Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International limelaani hukumu ya kifungo cha miaka minne jela dhidi ya kiongozi huyo wa upinzani nchini, likisema maamuzi hayo ni matokeo ya mchakato uliokosa haki tangu mwanzo.
Akizungumza baada ya Lissu kutiwa hatiani kwa kosa la uchochezi, Mkurugenzi wa Amnesty International Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Tigere Chagutah, alisema Lissu hakupaswa kukamatwa, kufikishwa mahakamani wala kutiwa hatiani.
Shirika hilo limesema mwenendo wa kesi hiyo ulikumbwa na ukiukwaji wa haki ya kupata usikilizwaji wa haki, likidai kuwa Lissu alinyimwa fursa ya kuwasiliana kwa siri na mawakili wake jambo lililomlazimu kujitetea mwenyewe.
“Matangazo ya moja kwa moja ya mwenendo wa kesi yalikatizwa, huku waangalizi wa kimataifa wa kesi hiyo wakikamatwa, kudaiwa kuteswa na baadaye kufukuzwa nchini.
“Tundu Lissu aliwekwa katika mazingira yasiyofaa ya mahabusu, akihifadhiwa katika selo ya wafungwa wa adhabu ya kifo na akiwa na upatikanaji mdogo wa huduma za kidini.
Amnesty International imetoa mwito kwa mamlaka za Tanzania kufuta hukumu na adhabu dhidi ya Lissu, kumuachilia huru bila masharti na kusitisha matumizi ya sheria za uhaini na sheria nyingine za usalama dhidi ya wakosoaji wa serikali sambamba na kuheshimu haki za uhuru wa kujieleza na kukusanyika kwa amani.
IDU watoa neno
Muungano wa kimataifa wa vyama vya siasa vinavyoegemea misingi ya demokrasia, uhuru, utawala wa sheria na uchumi huria (IDU) katika taarifa yake Novemba 6, 2026, pamoja na kutoa pole kwa familia ya Lissu, imezitaka serikali za nchi za kidemokrasia, Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kutokubali matokeo ya hukumu hiyo dhidi ya Lissu kama suluhu au mwafaka.
“Kumfunga kiongozi wa upinzani kwa kosa ambalo hakuwahi kushtakiwa nalo kunapaswa kuwa na athari kubwa katika mahusiano yao na Tanzania. IDU inasimama imara pamoja na washirika wake katika Umoja wa Demokrasia Afrika (Democracy Union of Africa – DUA), Tundu Lissu, Chadema na Watanzania wote katika harakati zao za kuhakikisha wanapata haki ya kuchagua serikali yao kwa uhuru,” inasema taarifa hiyo.
Martha Karua
Mwanaharakati, mwanasheria na mwanasiasa maarufu nchini Kenya, Martha Karua, amepinga vikali Lissu kuhukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka minne kwa kosa la uchochezi, akidai kuwa hukumu hiyo ni ya upotoshaji wa haki na anapaswa kuachiliwa huru mara moja.
Martha ambaye pia ni mwanasheria na kiongozi wa Chama cha People's Liberation Party (PLP) nchini Kenya, amelaani hukumu hiyo akielezea kuwa imejaa upotoshaji mkubwa wa haki na kutaka aachiliwe mara moja.
Profesa Anna Tibaijuka
Mwanasiasa maarufu nchini, Profesa Anna Tibaijuka ameandika kwenye ukurasa wake wa X kwamba, kesi ya Lissu inafanana na kesi iliyofunguliwa na wakoloni mwaka 1958 dhidi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Profesa Tibaijuka, ambaye amewahi kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, pamoja na mambo mengine, amesema hata hivyo kuwa kama ilivyotokea mwa Mwalimu, hukumu ya jinai dhidi ya kiongozi wa kisiasa si lazima iwe mwisho wa safari yake ya kisiasa; bali historia inaonesha umuhimu wa kuendeleza majadiliano badala ya mapambano na vurugu.
Lissu alikamatwa Aprili 9, 2025 baada ya kufanya mkutano wa kisiasa mjini Mbinga, mkoani Ruvuma na siku iliyofuata alishtakiwa kwa kosa la uhaini kuhusiana na kauli na machapisho yaliyohusiana na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Vyombo vya habari vya nje vilivyoripoti hukumu ya Lissu kwa maoni tofauti ni pamoja na Global News Agencies ya Toronto Canada, Xinhua News Agency ya China na Intentiona Broadcasters &Outlets, Aljazeera na TRT Afrika. Vingine ni Club of Mozambique na Region & Specialized Media.
Mashirika ya kiraia Kenya
Mashirika ya kiraia ya Kenya (CSOs), ambazo ni taasisi za kisheria na wanaharakati mashuhuri wamelaani vikali hukumu hiyo, wakiitaja kuwa ni hatua inayochochewa kisiasa na inayolenga kudhoofisha demokrasia.
Wanaharakati hao wa Kenya na mashirika ya kiraia ya kikanda wamepinga hukumu ya Lissu ya kosa la uchochezi wakiitaja siku hiyo kuwa ni ya giza kwa demokrasia.
Katika taarifa yao mwishoni mwa wiki, wamesema hukumu hiyo ni sehemu ya mvutano wa muda mrefu kati ya watetezi wa haki za binadamu nchini Kenya na Serikali ya Tanzania kuhusu mwenendo wa kesi ya Lissu.
Edwin Sifuna
Seneta wa Kaunti ya Nairobi kupitia chama cha ODM, Edwin Sifuna, amesema kushindwa kwa mashtaka ya uhaini dhidi ya Lissu ni jambo la kuleta faraja kwa watetezi wa demokrasia duniani.
“Mashtaka hayo hayakupaswa kuwasilishwa mahakamani tangu mwanzo. Kosa pekee la Lissu lilikuwa kutoa wito wa kufanyika kwa mageuzi ya msingi katika mfumo wa uchaguzi nchini Tanzania ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa haki na usawa.
Wakili Mwabukusi
Rais wa Chama cha wanasheria wa Tanganyika (TLS), Bonifasi Mwabukusi, aliandika katika mitandao ya kijamii saa chache baada ya Lissu kupangua kesi ya uhaini lakini akahukumiwa kwa kosa la uchochezi.
“Kesi ya Lissu imelingana na kesi ya Yesu. Pilato hakuona hatia kabisa wakadai kuhusu (Yesu) kujiita mfalme, wengine wakasema alisema atalivunja hekalu, lakini Pilato hakuona hatia.
“Mke wa Pilato akamwambia muachie mtu huyu hana hatia yoyote, basi kuwaridhisha Wayahudi na wakuu wa makuhani akatafuta tafuta kosa na adhabu ya viboko, lakini baadaye kwa hofu ya shinikizo la kisiasa akawakabidhi Yesu wakamsulubishe wakijua imekwisha; kumbe ndiyo ngoma inaanza,” aliandika wakili huyo bila kufafanua zaidi.
Askofu Bagonza
Askofu wa Kanisa na Kiinjili la Kilutheriw Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Askofu Dkt. Benson Bagonza amesema hukumu iliyotolewa na Mahakama kuu ya Tanzania dhidi ya Lissu haichochei maridhiano.
Alitoa maoni hayo wakati akihojiwa na SAUT Media, ambapo alisema kulikuwa na fursa nzuri kumfanya Lissu na chama chake waweze kusongelea meza ya maridhiano.
Bob Wine anena
Rais wa chama cha NUP, nchini Uganda, Robert Kyagulany maarufu Bob Wine amesema uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania wa kumwachia huru Lissu dhidi ya mashtaka ya uhaini yaliyokuwa na misukumo ya kisiasa ni ushindi dhidi ya moja ya silaha kubwa zaidi zinazotumiwa na dola kuwatisha na kuwanyamazisha wapinzani.
Umebakiwa na makala 2 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.
- Lissu
- Hukumu
- Mahakama Kuu
- Wanasheria
- Tanzania
- Kifungo