Habari
Madola yakamia amani ya Tanzania
Jumuiya ya Madola bado ina jambo na Tanzania na safari hii inapenda kuona amani, maridhiano na umoja vikitamalaki kama Pambazuko inavyoeleza.

UHURU wa vyombo vya habari na maridhiano Tanzania, vimeendelea kuwa masuala muhimu katika mwendelezo wa vikao vya Kundi la Mawaziri la Jumuiya ya Madola (CMAG).
Kundi hilo limeendelea kuisisitiza Serikali ya Tanzania kuona umuhimu wa kuchukua hatua muhimu kwenye maeneo hayo.
Katika kikao chake cha 74 kilichofanyika Septemba 20, 2026, kundi hilo limeitaka Serikali ya Tanzania kuona umuhimu wa kuimarisha maridhiano ya kisiasa, kulinda uhuru wa kiraia na vyombo vya habari, pamoja na kuhakikisha haki inatendeka katika kesi ambazo bado hazijakamilika.
Kikao hicho kilihitimishwa kwa kundi hilo kuamua kuendelea kuiweka Tanzania kwenye ajenda yake rasmi.
Mawaziri washiriki wameeleza kuwa pamoja na kutambua maendeleo yaliyopatikana katika baadhi ya maeneo, bado kuna haja ya kuchukua hatua zaidi ili kufikia matarajio yaliyowekwa na kundi hilo.
“CMAG imeendeela kusisitiza umuhimu wa kuendeleza mchakato jumuishi wa vyama vya siasa unaosimamiwa kwa njia inayoaminika, kulinda uhuru wa kiraia, kisiasa na wa vyombo vya habari, pamoja na kuhakikisha taratibu za haki, kwa wakati na zenye uwazi katika kushughulikia kesi ambazo bado hazijamalizika.
“Pia imesisitiza kuwepo kwa mifumo inayoaminika ya uwajibikaji, utoaji wa haki na fidia stahiki kwa watu walioathirika,” imeeleza taarifa ya CMAG.
Katika mkutano huo, CMAG ilifanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo, pamoja na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Prof. Palamagamba Kabudi.
Kundi hilo lilitambua ushirikiano wa Tanzania na Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, mazungumzo yaliyofanyika hivi karibuni na vyama vya siasa, pamoja na hatua zinazochukuliwa kuelekea maridhiano Zanzibar, likisema mambo hayo ni msingi mzuri wa kupiga hatua zaidi.
Hata hivyo, CMAG ilikumbusha masharti manne yaliyoainishwa katika mkutano wake wa 71 wa Desemba 2025, pamoja na matarajio yenye muda maalumu yaliyowekwa katika mkutano wake wa 73 wa Julai 2026.
Kutokana na hali hiyo, kundi hilo limeihimiza Serikali ya Tanzania kukubaliana mapema tarehe ya ziara ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, ili aweze kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan na wadau wengine.
CMAG ilisema itaendelea kuiweka Tanzania kwenye ajenda yake rasmi, hatua inayomaanisha kuwa masuala yanayohusu nchi hiyo yataendelea kufuatiliwa katika mikutano yake.
Pole kifo cha mume wa Samia Katika mkutano huo, CMAG ilikaa kimya kwa dakika moja kwa heshima ya marehemu Hafidh Ameir Hassan, mume wa Rais Samia Suluhu Hassan, aliyefariki dunia Septemba 7, 2026.
Kundi hilo pia lilisisitiza dhamira yake ya kulinda na kuendeleza misingi ya kisiasa ya Jumuiya ya Madola, kama ilivyoainishwa katika mkataba wa jumuiya hiyo.
CMAG pia imeipongeza Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola kwa juhudi zake za kuendeleza mazungumzo yenye kujenga na kuimarisha uaminifu miongoni mwa nchi wanachama.
Mkuu wa Jumuiya ya Madola, ni Mfalme Charles III.
Umebakiwa na makala 2 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.
- madola
- uchaguzi
- lissu
- tanzania