Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Habari

THRDC: Haki, suluhu kesi ya Lissu viharakishwe

MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), umetoa mapendekezo kuhusu hatma ya kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, ukitaka hatua zichukuliwe haraka kuimarisha haki, utawala wa sheria na maridhiano ya kitaifa.

Jumatatu, 24 Agosti 2026 · 06:00Dakika 1 kusomaToleo 179, uk. 16
Olengurumwa
Olengurumwa — Na Mpigapicha Wetu

Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kusudio la kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Katika tamko lao, THRDC imeiomba Mahakama kuhakikisha shauri hilo linasikilizwa na kuamuliwa kwa haraka, kupunguza ucheleweshaji na kusimamia kwa umakini maombi ya kuahirisha kesi.

Akizungumza na waandishi wa habari wiki iliyopita, Mratibu wa Taifa wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, amesema mapendekezo hayo yametokana na ufuatiliaji wa mwenendo wa kesi hiyo uliofanywa na mtandao huo.

“Tunaitaka serikali kutumia mifumo ya kisheria iliyopo, ikiwemo mamlaka ya DPP inapofaa, kutafuta suluhisho la shauri la Lissu kwa kuzingatia haki, umoja wa kitaifa na mshikamano wa kijamii,”amesema Olengurumwa.

Olengurumwa amesema mazungumzo na maridhiano ni muhimu katika kutatua changamoto, ikiwemo suala la Katiba Mpya.

Pia amesema katika uchambuzi wake mtandao huo ulibaini changamoto kadhaa katika mwenendo wa kesi hiyo inayomkabili Lissu baada ya kufanya ufuatiliaji kuanzia Aprili 9, 2025 hadi Agosti 19, 2026.

Olengurumwa amesema timu ya ufuatiliaji wa awali ukiongozwa na Mkuu wa Idara ya Utetezi wa THRDC, Paul Kisabo, imesema ufuatiliaji huo ulihusisha hatua mbalimbali za mchakato wa haki jinai, ikiwemo kukamatwa na kufikishwa mahakamani.

Pia mazingira ya kizuizini, upatikanaji wa uwakilishi wa kisheria, mawasiliano na familia, ushiriki wa umma na waangalizi, mwenendo wa upande wa mashtaka pamoja na kuahirishwa kwa kesi.

THRDC imesema ilibaini kuwa Lissu alipokamatwa Mbinga mkoani Ruvuma Aprili 9, 2025, hakuelezwa sababu za kukamatwa kwake wakati huo wala alipokuwa akisafirishwa hadi Dar es Salaam.

“Alijulishwa mashtaka baada ya kufikishwa Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam Aprili 10, 2025…”

“Akafikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu siku moja baada ya kukamatwa, ambapo shtaka la uhaini lilisomwa na kufafanuliwa kwake, ingawa hakutakiwa kujibu kwa kuwa mahakama hiyo haikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo,”amesema Olengurumwa.

  • Tundu Lissu
  • Haki za binadamu
  • THRDC

Soma Pia