Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Habari

Mchakato tuzo anayowania Lissu

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu ameingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania tuzo kubwa na yenye heshima Ulaya inayosimamiwa na kuamuriwa na bunge la bara hilo kwa mwaka huu, 2026.

Jumatatu, 21 Septemba 2026 · 06:00Dakika 4 kusomaToleo 183, uk. 22

Tuzo hiyo maarufu inayoitwa Sakharov na iliyowahi kunyakuliwa na baadhi ya watu maarufu duniani akiwamo Nelson Mandela, aliyekuwa rais wa kwanza wa Afrika Kusini isiyokuwa ya kibaguzi, Koffi Annan aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ina mchakato mrefu ambao Pambazuko linauweka hapa bayana.

Tuzo hiyo hupewa watu au taasisi zinazochomoza zaidi kwenye utetezi wa haki za binadamu, kupigania demokrasia na uhuru wa kuzungumza.

Kupendekezwa kwa jina la Lissu bado siyo ushindi, kwani mchakato huo una hatua kadhaa zisizohusisha upigaji kura za wananchi au mitandao ya kijamii. Uamuzi wote unafanyika ndani ya taasisi za Bunge la Ulaya.

Mwingine aliyethibitishwa kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho ni taasisi ya Standing Together, ambayo ni harakati ya pamoja ya Wayahudi na Waarabu nchini Israel iliyopendekezwa na Renew Europe (RE).

Standing Together ilianzishwa na Alon-Lee Green na Rula Daood ili kufanya harakati ya kutetea usawa, haki za kijamii na suluhu ya amani kati ya Israel na Palestina.

Majina mengine yanaweza kuongezeka hadi mchakato wa uteuzi utakapofungwa rasmi.

Mpaka sasa, wagombea waliowekwa hadharani ni wawili; Lissu kutoka Tanzania na taasisi ya Standing Together. Lissu anaungwa mkono na European People’s Party (EPP) na European Conservatives and Reformists (ECR).

Pendekezo hilo kwa Lissu linapata uzito wa kisiasa ndani ya bunge la Ulaya, lakini haumhakikishii nafasi katika fainali au kuingia ‘tatu bora’ kabla ya mshindi kutangazwa.

Mshindi anavyopatikana Katika kuchagua mshindi, kura zinapigwa na viongozi wa makundi manane ya kisiasa katika Bunge la Ulaya, lakini uzito wa kura ya kila kiongozi unategemea ukubwa wa kundi lake bungeni.

Ili kufika tatu bora, kura zinapigwa na wajumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje na Kamati ya Maendeleo ya Bunge la Ulaya, ambao idadi yao ni 104. Kwa mfano, uzito wa kura ya kiongozi wa EPP ambalo ni kundi kubwa zaidi, na la kwanza kupendekeza jina la Lissu, ni mkubwa kuliko wa kiongozi wa kundi lingine lolote.

Kitu muhimu kwa sasa ni kwamba Lissu ameungwa mkono rasmi na makundi mawili tofauti ya kisiasa ndani ya Bunge la Ulaya, yaani EPP na ECR.

Tuzo ya Sakharov ni nini?

Sakharov Prize ilianzishwa na Bunge la Ulaya na kutolewa kwa mara ya kwanza mwaka 1988. Ilipewa jina la Andrei Sakharov, mwanafizikia wa Muungano wa Kisovieti (Soviet Union) aliyekuwa mmoja wa wakosoaji mashuhuri wa ukandamizaji wa kisiasa na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Washindi wa kwanza walikuwa Nelson Mandela wa Afrika Kusini na baada ya kifo chake, alifuata mwanaharakati wa Kisovieti, Anatoli Marchenko.

Tangu wakati huo, tuzo hiyo imekuwa ikitolewa kwa wanaharakati, waandishi wa habari, wafungwa wa dhamira, wanasheria, viongozi wa kisiasa, mashirika na wanaharakati mbalimbali duniani.

Mshindi hupokea pia Euro 50,000 sawa na zaidi ya Shilingi milioni 150, lakini uzito mkubwa wa tuzo hiyo ni hadhi yake ya kimataifa na kuingia katika Sakharov Prize Community.

Kwa nini Lissu?

Kupendekezwa kwa jina la Lissu kumejengwa juu ya rekodi yake kama mwanasheria, mwanasiasa wa upinzani na mtetezi wa mageuzi ya uchaguzi, utawala wa sheria na uhuru wa kisiasa Tanzania.

Wanaomuunga mkono wameeleza pia shambulio la risasi dhidi yake mwaka 2017, kurejea kwake Tanzania, kugombea urais mwaka 2020, kukamatwa kwake Aprili 2025 na kushtakiwa kwa uhaini, kosa lenye adhabu ya kifo chini ya sheria za Tanzania, kuwa ni sifa nyingine zilizomuinua Lissu.

Mgombea anapatikanaje?

Mtu au taasisi huweza kuteuliwa kwa njia mbili; mosi, anaweza kuungwa mkono na angalau wabunge 40 wa Bunge la Ulaya, au kuteuliwa moja kwa moja na kundi la kisiasa ndani ya bunge hilo.

ya wagombea ilikuwa ni Septemba 17 na baada ya hapo kuna hatua tatu muhimu.

Oktoba Mosi, 2026 wagombea watawasilishwa mbele ya kikao cha pamoja cha Kamati ya Mambo ya Nje (AFET), Kamati ya Maendeleo (DEVE), na Kamati ya Haki za Binadamu (DROI).

Oktoba 19, 2026, AFET na DEVE zitapiga kura na kuchagua wateule watatu walitakaoingia fainali.

Oktoba 22, 2026 mikutano ya marais inayojumuisha Rais wa Bunge la Ulaya na viongozi wa makundi ya kisiasa itachagua mshindi kutoka kwa watu au taaissi tatu zilizopendekezwa, na mshindi atakabidhiwa tuzo Desemba 16, 2026 huko Strasbourg, Ufaransa.

Msimamizi kampeni za Lissu Kwa sasa nguvu kubwa nyuma ya Lissu ni EPP na ECR. EPP ni moja ya makundi makubwa ya kisiasa yenye ushawishi ndani ya Bunge la Ulaya, huku ECR pia ikiwa na ushawishi wake katika masuala ya haki za binadamu na mambo ya nje.

Kwa Lissu kupata uugwaji mkono kutoka makundi mawili tofauti ya kisiasa, anaingia kwenye mchakato akiwa tayari ana msingi ndani ya bunge.

Hadi sasa, mlango wa wagombea wa mwaka 2026 bado haujafungwa rasmi kwenye orodha ya fainali.

Ushindi wa Lissu una maana gani?

Hata kabla ya kujulikana mshindi, kupendekezwa peke yake tayari kumepeleka jina la Lissu na kesi yake ya uhaini kwenye jukwaa la moja ya taasisi kubwa za kisiasa duniani.

Lakini hatua muhimu zaidi sasa si uteuzi kwa watu watatu watakaoingia fainali Oktoba 19, 2026 na Lissu akifika hapo atakuwa ameingia hatua kubwa kabisa.

Lissu atahesabika kuwa mmoja wa watu au taasisi tatu ambazo Bunge la Ulaya limeamua rasmi kuzitazama na kuzitambua kwa heshima yake kubwa zaidi katika eneo la haki za binadamu na uhuru wa mawazo.

Baada ya hapo, uamuzi wa mshindi utakuwa mikononi mwa viongozi wa makundi ya kisiasa ya bunge la Ulaya Oktoba 22, 2026.

Mkala haya yameandikwa wa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari.

  • Tundu Lissu
  • Sakharov
  • Bunge la Ulaya
  • Haki za Binadamu

Soma Pia