Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Uchumi & Biashara

Urari wa biashara EAC waimarika

Mauzo ya nje ya Afrika Mashariki yaliongezeka kwa kasi kuliko uagizaji wa bidhaa katika robo ya pili ya mwaka 2026, na kuiwezesha kanda kupata ziada ya biashara ya dola milioni 300.

Jumatatu, 21 Septemba 2026 · 06:00Dakika 4 kusomaToleo 183, uk. 18

THAMANI ya biashara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) iliongezeka kwa asilimia 37 na kufikia dola bilioni 52.3 katika robo ya pili ya mwaka 2026, ikichochewa na ongezeko kubwa la mauzo ya nje.

Mwenendo huo umeisaidia Afrika Mashariki kuondokana na nakisi ya biashara ya karibu dola bilioni moja iliyorekodiwa mwaka mmoja uliopita.

Hayo yamebainishwa kupitia taarifa ya hivi karibuni ya takwimu za robo mwaka kwenye mwenendo wa uchumi wa eneo hilo iliyotolewa na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Taarifa hiyo inaonyesha kuwa mauzo ya nje yaliongezeka kwa asilimia 41.3 na kufikia dola bilioni 26.3 katika kipindi cha Aprili hadi Juni, yakizidi kasi ya ongezeko la bidhaa zilizoagizwa kutoka nje, ambazo zilipanda kwa asilimia 32.9 hadi dola bilioni 26.

Hali hiyo iliifanya EAC kupata ziada ya biashara ya dola milioni 300, ikilinganishwa na nakisi ya dola milioni 945.3 katika kipindi kama hicho mwaka 2025.

Takwimu hizo zinaashiria kuimarika kwa biashara ya nje ya EAC wakati jumuiya hiyo yenye nchi wanachama nane ikiendelea kutumia ukubwa wa soko lake, miundombinu ya kikanda na mikataba ya biashara kuharakisha ukuaji wa viwanda na kuvutia uwekezaji.

Hata hivyo, katikati ya ukuaji huo mkubwa kuna changamoto kadhaa.

Moja ya changamoto hizo ni ongezeko la mauzo ya nje bado linategemea kwa kiwango kikubwa madini.

Changamoto nyingine ni kuwa biashara baina ya nchi wanachama wa EAC, licha ya kuongezeka, imeendelea kuwa na sehemu ndogo katika mauzo yote ya nje ya jumuiya.

Masoko ya Afrika muhimu Nchi nyingine za Afrika zimeendelea kuwa masoko muhimu kwa bidhaa zinazozalishwa Afrika Mashariki.

Taarifa hiyo inaonyesha kuwa mauzo ya EAC kwenda nchi nyingine za Afrika yaliongezeka kwa asilimia 44.3 hadi dola bilioni 7.2, sawa na ongezeko la asilimia 27.5 ya mauzo yote ya nje ya Jumuiya.

Mauzo kwenda nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) yaliongezeka kwa asilimia 50.8 hadi dola bilioni 5.1, huku mauzo kwenda nchi za Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (Comesa) yakiongezeka kwa asilimia 48.3 na kufikia dola bilioni 3.1 kwa jumla.

Ukuaji huo unaonyesha umuhimu wa masoko ya Afrika kwa biashara za Afrika Mashariki wakati bara hilo likielekea kwenye muunganiko mkubwa zaidi wa kibiashara kupitia Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA).

Taarifa inaonyesha pia kuwa biashara ndani ya EAC nayo iliimarika. Mauzo baina ya nchi wanachama yaliongezeka kwa asilimia 33.2 na kufikia dola bilioni 3.2.

Hata hivyo, sehemu ya mauzo hayo katika mauzo yote ya EAC ilishuka kutoka asilimia 12.8 katika robo ya pili ya 2025 hadi asilimia 12.1 mwaka 2026.

Hata hivyo, taarifa inabainisha kuwa hii haimaanishi kuwa biashara baina ya nchi wanachama ilipungua. Badala yake, mauzo kwenda masoko ya nje ya EAC yaliongezeka kwa kasi zaidi.

Kwa watunga sera wa kanda, hata hivyo, kiwango hicho kidogo cha biashara ya ndani ya EAC kinaendelea kuwa jambo muhimu, kwa kuwa moja ya malengo makuu ya mtangamano wa kikanda ni kujenga soko kubwa linalowezesha kampuni kuzalisha bidhaa katika nchi moja mwanachama na kuziuza kwa urahisi katika nchi nyingine za Jumuiya.

Biashara na China yachomoza Taarifa hiyo inabainisha kuwa China imeendelea kuwa mhimili mkubwa wa ukuaji wa mauzo ya nje ya EAC.

Mauzo ya EAC kwenda China yalikaribia kuongezeka mara mbili, kutoka dola bilioni 5.7 hadi dola bilioni 10.7 kati ya robo ya pili ya 2025 na kipindi kama hicho mwaka 2026.

Ukuaji huo ulichangiwa kwa kiasi kikubwa na mauzo ya madini na malighafi nyingine.

Bidhaa zilizoagizwa kutoka China nazo ziliongezeka kwa kiasi kikubwa, kutoka dola bilioni 4.7 hadi dola bilioni 7.1.

Falme za Kiarabu (UAE) na Afrika Kusini zilikuwa miongoni mwa masoko mengine makubwa ya bidhaa za EAC, huku India, UAE, goni mwa vyanzo vikuu vya bidhaa zinazoagizwa na nchi za jumuiya.

Takwimu hizo zinaonyesha kuongezeka kwa ushiriki wa Afrika Mashariki katika biashara ya kimataifa, lakini pia zinaibua swali muhimu kuhusu aina ya bidhaa ambazo kanda inauza nje.

Shaba na metali za thamani zilichangia asilimia 61.9 ya mauzo yote ya nje, kutoka asilimia 58.7 mwaka mmoja uliopita.

Kahawa, chai na viungo viliendelea kuwa bidhaa muhimu za kilimo zinazouzwa nje, wakati bidhaa za petroli ziliongoza kwa thamani miongoni mwa bidhaa zilizoagizwa kutoka nje, sambamba na mashine, vifaa vya usafiri na pembejeo za viwandani.

Kuongezeka kwa utegemezi wa madini kunamaanisha kuwa ziada ya biashara haiwezi kutafsiriwa moja kwa moja kuwa ishara ya kuimarika kwa ushindani wa viwanda vya kanda.

Bei za bidhaa ghafi na mahitaji ya madini katika soko la dunia yanaweza kubadilika kwa kasi, hivyo kuyaweka katika mazingira hatarishi mataifa yanayoyategemea kwa kiwango kikubwa.

Kwa hiyo, fursa kubwa ya muda mrefu ni kugeuza ukuaji wa biashara kuwa kichocheo cha uchakataji wa malighafi na uzalishaji wa bidhaa viwandani ndani ya kanda.

  • EAC
  • Biashara
  • Uchumi
  • Afrika Mashariki

Soma Pia