Afya ya Kimwili
Fiziotherapia huimarisha maisha, uhuru
KATIKA jamii nyingi hasa Afrika, ulemavu huonekana kama kikwazo kinachomzuia mtu kuishi maisha yenye tija na furaha.
Ukweli ni kwamba, ulemavu sio mwisho wa maisha au kikomo cha ndoto za mtu.
Huduma za fiziotherapia (wengi huita mama cheza) zina mchango mkubwa na wa kipekee katika kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanapata fursa ya kufurahia ubora wa maisha, kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi.
Kwa mtu anayeishi na ulemavu iwe wa kuzaliwa, uliotokana na ajali au ugonjwa kama vile kiharusi (stroke), wataalamu hutumia mbinu za kisayansi, mazoezi maalum na vifaa saidizi ili kusaidia mwili kurejesha uwezo wake.
Kwa wasomaji wa gazeti la Pambazuko makala haya yanaangazia baadhi ya faida katika maeneo.
Kwanza, kurahisisha uwezo wa kutembea na kupunguza maumivu. Mazoezi ya viungo husaidia kuongeza nguvu za misuli, kuboresha uratibu wa mfumo wa fahamu na viungo, pamoja na kupunguza maumivu ya muda mrefu yanayoweza kumpata mtu mwenye ulemavu.
Pili, kujenga uhuru na kujitegemea, kupitia tiba hii, mtu hufundishwa mbinu mpya za kufanya mambo ya kila siku kama vile kujivalisha, kula, au kutoka sehemu moja kwenda nyingine bila kulazimika kutegemea msaada wa wengine muda wote.
Tatu, kuzuia madhara mengine ya kiafya: Mtu anayetumia kiti cha magurudumu au aliye kitandani kwa muda mrefu yuko katika hatari ya kupata vidonda vya kukaa (bedsores), kupinda kwa mifupa (contractures), na matatizo ya mzunguko wa damu.
Fiziotherapia huzuia changamoto hizi kabla hazijatokea.
Nne, kukuza afya ya akili na kujiamini.
Uwezo wa kujisogeza na kufanya mambo binafsi huongeza kujiamini, kupunguza msongo wa mawazo au mshtuko wa nafsi na kuwapa watu wenye ulemavu matumaini ya siku zijaye.
Huduma imara hupunguza kwa kiasi kikubwa utegemezi wa muda mrefu kwa kuwasaidia watu wenye ulemavu kukuza uwezo wao wa kimwili, kujiamini, na kujitegemea.
Hii ina maana kwamba, ingawa watu wenye ulemavu wataendelea kuwepo katika jamii zetu, hawapaswi kuonekana kama ombaomba au mzigo, bali kama wajumbe wenye uwezo wa kujitegemea.
Fiziotherapia sasa inaleta mabadiliko makubwa ya mtazamo kutoka kwenye dhana ya kutegemea matibabu ya hospitalini pekee, hadi kumwezesha mtu binafsi kupata uhuru na uwezo wa kumudu maisha yake ya kila siku.
Kama inavyosisitizwa katika kaulimbiu za kimataifa za afya, kila mtu ana haki ya kuishi maisha hai na yenye ubora.
Fiziotherapia si tu huduma ya matibabu bali ni daraja linalowavusha watu wenye ulemavu kutoka kwenye utegemezi na kuwafikisha kwenye uhuru na utu wao.
Mwandishi: Emmanuel Jacob, Afisa Mfiziotherapia (Mwenyekiti wa Tanzania Physiotherapy Initiative).
Umebakiwa na makala 2 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.
- Ulemavu
- Afya
- Fiziotherapia