Afya ya Kimwili
Ni kweli watu wenye ulemavu hufichwa?
KATIKA jamii nyingi barani Afrika, ni nadra sana kuwaona watu wenye ulemavu wakijumuika kikamilifu kwenye maeneo ya umma.

Takwimu za kitaifa zinaonyesha kuwa nchini Tanzania kuwa takribani asilimia tisa hadi 11 ya wananchi wanaishi na aina fulani ya changamoto ya kiutendaji au ulemavu.
Tukiangalia idadi hii kubwa inabidi tujiulize; je, kweli tunawaona wakishiriki kikamilifu katika shughuli za kila siku za kijamii na kiuchumi, au wanaendelea kuachwa nyuma?
Kutokuonekana huku siyo kwa bahati mbaya, bali ni matokeo ya mfumo wa kijamii unaoendelea kuwatenga na kuwaficha ndani ya nyumba.
Mtazamo huu unachochewa na imani potofu za kiutamaduni pamoja na ukosefu wa miundombinu rafiki.
Wiki hii tunaangazia sababu ambazo zinasababisha watu wenye ulemavu kufichwa, ni muhimu kwa wasomaji wa safu hii wafahamu;
Kizuizi kikubwa kinachowafanya watu wenye ulemavu wakataliwe kuonekana hadharani ni unyanyapaa uliokita mizizi.
Katika jamii nyingi, ulemavu bado unahusishwa na ushirikina ukionekana kama laana, adhabu kutoka kwa mababu, au matokeo ya uchawi na dhambi zilizofanywa na familia.
Imani hizi huleta aibu kubwa kwa familia husika. Wasiwasi wa kupoteza heshima, kuharibu fursa za ndoa kwa wanafamilia wengine, na hofu ya kutengwa na jamii huwalazimisha wazazi au walezi kuwafungia ndani ndugu zao wenye ulemavu.
Badala ya kupewa fursa ya kuendelea, wanalazimika kuishi maisha ya kujificha ili kuepuka maneno ya kashfa na kutengwa na majirani.
Sababu nyingine ni zile zinazohusisha zaidi changamoto za miundombinu na uchumi;
Mbali na mtazamo wa kijamii, miundombinu isiyo rafiki inafanya ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu kuwa ndoto isiyofikiwa.
Barabara nyingi, vyombo vya usafiri wa umma, majengo ya serikali na shule hazina njia za viti vya kulia (ramps), au alama za sauti kwa wenye ulemavu wa kuona na kusikia. Hali hii inamfanya mtu mwenye ulemavu kuwa mfungwa wa mazingira yake mwenyewe.
Umaskini pia unachangia kwa kiasi kikubwa. Vifaa saidizi kama viti vya kulia, magongo, au vifaa vya kusikia vina gharama kubwa ambazo familia nyingi hazimudu.
Bila msaada au ruzuku kutoka serikalini, familia zilizojikita katika umaskini hazina uwezo wa kutoa huduma hizi. Matokeo yake, huduma za afya na elimu zinabaki kuwa starehe badala ya haki ya msingi.
Ili kuondokana na hali hii ya unyanyapaa na ubaguzi, ni lazima jamii ibadili mtazamo wake. Ulemavu si laana wala aibu, bali ni utofauti wa kibinadamu unaohitaji fursa sawa.
Mwandishi: Emmanuel Jacob, Afisa Mfizioterapia (Mwenyekiti wa Tanzania Physiotherapy Initiative).
- Ulemavu
- Afya
- Unyanyapaa
- Miundombinu