Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Afya ya Kimwili

Usimfanyie masaji ya nguvu mgonjwa wa kiharusi

KIHARUSI ni dharura kubwa ya kitiba inayotokea pale mzunguko wa damu kwenda kwenye ubongo unapokatika au pale mshipa wa damu unapopasuka.

Jumatatu, 14 Septemba 2026 · 03:00Dakika 2 kusomaToleo 182, uk. 25

KIHARUSI ni dharura kubwa ya kitiba inayotokea pale mzunguko wa damu kwenda kwenye ubongo unapokatika au pale mshipa wa damu unapopasuka.

Katika jamii zetu, mara nyingi mgonjwa anapopooza kutokana na kiharusi, ndugu hukimbilia kumfanyia ukandaji (masaji) wakati mwingine kwa nguvu sehemu mbalimbali za mwili huku wakiamini itarudisha utendaji kazi wa misuli na mwili.

Hata hivyo, jambo hili linaweza kuleta madhara kwa mgonjwa badala ya kumsaidia.

Mara mtu anapopata kiharusi, mabadiliko hutokea kwenye mishipa ya damu inayopeleka damu kwenye ubongo ambayo inakuwa imepasuka au kuvimba.

Katika hali hii tunahitaji muda wa kupona na kurejea kwenye hali yake. Na taarifa zinazotoka maeneo mbalimbali kwa mfano sauti, miguso, au mitetemo ni muhimu ikawa kwenye hali ambayo inachochea uponyaji.

Kukanda kwa nguvu au kwa kina (deep, vigorous massage) kunaweza kusababisha kuvimba kutokana na damu kuvilia (blood clots) na maumivu makali kwenye viungo mbalimbali.

Usilazimishe, badala ya kutumia nguvu nyingi, wataalamu hushauri kutumia mbinyo kidogo na wa upole sana (light pressure) ili kuepuka kuongeza msongo kwenye mishipa ya damu.

Kwa safu yetu wiki hii, tutaangalia kuhusu dhana potofu zilizosambaa kwenye jamii kuhusu massage hasa kwa wagonjwa wiliopatwa na kiharusi:

Dhana potofu ya kwanza; Masaji peke yake inaweza “kutibu” au kurejesha utendaji kazi wa kimwili baada ya kiharusi. Ukweli ni kwamba; Masaji ni tiba ya ziada tu (complementary therapy).

Hainusuru wala kurejesha mfumo wa neva ulioharibika, na haiwezi kuchukua nafasi ya mbinu kama tiba ya mazoezi (physical therapy), tiba kwa vitendo (occupational therapy), au tiba inayomwezesha mgonjwa kuzungumza tena (speech therapy).

Dhana potofu ya pili; Masaji ya nguvu na ya kina “inaondosha” kukaza na kukakamaa kwa misuli. Ukweli ni kwamba; Kukakamaa au kukaza kwa misuli (spasticity), kulazimisha massage ya nguvu au kuvuta misuli kwa nguvu kunaweza kusababisha majeraha makubwa kwenye tishu.

Kukabiliana na hali hii ya kukakamaa au kukaza inahitaji mbinu za taratibu, pamoja na matibabu ya dawa, na mazoezi maalum kutoka kwa mfiziotherapia.

Dhana potofu ya tatu; Lazima usubiri muda unaofaa na kushauriwa kitaalamu (kama wiki sita) kabla ya kuanza masaji. Ukweli ni kwamba; hakuna kanuni moja ya muda kwa kila mtu. Ili kuanza inategemea sana na utulivu wa afya ya mgonjwa, aina ya kiharusi, na idhini ya daktari.

Hata hivyo, masaji haipaswi kufanyika kabisa wakati bado mgonjwa akiwa katika hali mbaya na isiyostahimilika (acute stroke).

Dhana potofu ya nne; Masaji inatoa “sumu” mwilini. Ukweli ni kwamba; kulingana na Chama cha Tiba ya Massage cha Marekani (American Massage Therapy Association), hakuna ushahidi wa kisayansi unaothibitisha kuwa masaji inatoa sumu kutoka kwenye misuli kwenda kwenye mzunguko wa damu.

Masaji hapaswi kutazamwa kama muujiza wa kurejesha viungo vilivyopooza. Njia salama zaidi ya kumsaidia mgonjwa wa kiharusi ni kufuata mpango wa matibabu uliowekwa na madaktari na kufanya mazoezi ya tiba viungo na mazoezi (physiotherapy) chini ya usimamizi wa wataalamu waliosomea kazi hiyo.

Mwandishi: Emmanuel Jacob, Afisa Mfiziotherapia (Mwenyekiti wa Tanzania Physiotherapy Initiative).

Umebakiwa na makala 2 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.

  • Kiharusi
  • Afya
  • Masaji
  • Fiziotherapia

Soma Pia