Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Afya ya Kimwili

Kwa nini viungo bandia vya msaada hutupwa?

MARA nyingi tunasikia na hata kuona wafadhili kutoka nchi zilizoendelea wakigawa viungo bandia vya bure kwa watu wenye ulemavu katika nchi zinazoendelea.

Jumatatu, 17 Agosti 2026 · 14:15Dakika 2 kusomaToleo 178, uk. 25

Kitendo hiki huonekana kama cha huruma na upendo, lakini swali la msingi tunalopaswa kujiuliza ni hili; Kwa nini sehemu kubwa ya misaada hii huishia kutupwa, kutelekezwa na kugeuka kuwa takataka?

Uchunguzi unaonyesha kuwa kutotumika kwa viungo hivi bandia hakusababishwi tu na dharau ya wapokeaji, bali ni matokeo ya mifumo isiyokidhi mahitaji halisi na mazingira ya wapokeaji.

Kwa wasomaji wa safu hii ni muhimu sana tufahamu haya; kwamba sehemu inayounganisha kiungo bandia na mwili wa binadamu inahitaji kutengenezwa kulingana na umbo halisi la mhusika.

Viungo vya msaada vilivyotumiwa tayari (mtumba) au vilivyotengenezwa kwa vipimo totauti hali inayosababisha maumivu makali, michubuko na hata majeraha kwenye ngozi.

Vilevile sehemu ya mwili iliyobaki hubadilika umbo na kupungua ukubwa kadiri muda unavyokwenda.

Kiungo cha bure kisichoweza kurekebishwa kinakuwa cha purukushani na hatimaye kuachwa.

Hata hivyo, vifaa vingi vya msaada ni vizito na havijatengenezwa kwa ajili ya hali ya hewa ya joto. Hali hii husababisha jasho jingi na kero kubwa kwa mtumiaji.

Kumpa mtu kiungo bandia kisichomtosha ni sawa na kumlazimisha kutembea siku nzima akiwa amevaa kiatu kilicho kidogo kwa namba mbili. Mwishowe, ataamua kutembea peku.

Kwa nini viungo bandia vya msaada hutupwa?

Misaada mingi hutoka nchi za Ulaya ikiwa na teknolojia ya hali ya juu au iliyoundwa kwa ajili ya mazingira ya mjini yenye miundombinu iliyoendelea.

Vifaa hivi maridadi hushindwa kuvumilia mazingira ya vijijini kwenye miinuko, tope na njia zisizo rasmi. Matokeo yake, vinavunjika haraka sana.

Mara nyingi, nchi maskini hugeuzwa sehemu ya kutupia vifaa vilivyochakaa au vilivyopitwa na wakati ambavyo havina hata viwango vya usalama.

Tatizo kubwa zaidi la misaada hii ni mtazamo wa “saidia na uondoke” (give and go). Vifaa vinatolewa bila kuwepo kwa mfumo wa usaidizi wa muda mrefu. Pindi kifaa kinapoharibika, mtumiaji kupata kipuri cha kubadilisha inakuwa ni vigumu. Na maeneo mengi ya vijijini hayana wataalamu waliosomea, ambao hukarabati, au kuwafundisha watumiaji jinsi ya kutumia viungo hivyo kwa usalama.

Dhana kwamba “cha bure hakithaminiwi”

inapotosha ukweli katika suala la viungo bandia.

Watu hawavitelekezi vifaa hivi kwa sababu vilikuwa bure, bali kwa sababu vinasababisha maumivu, havina msaada wa kiufundi, na havilingani na maisha yao ya kila siku.

Msaada wa kweli sio kuleta makontena ya vifaa vilivyotumika visivyokidhi viwango. Msaada wa kweli ni kuwekeza kwenye miundombinu ya ndani: kufundisha wataalamu wa ndani, kutengeneza viungo bandia kwa kutumia malighafi za eneo husika, na kuhakikisha huduma za marekebisho zinapatikana karibu na jamii.

Mwandishi: Emmanuel Jacob, Afisa Mfiziotherapia (Mwenyekiti wa Tanzania Physiotherapy Initiative). Simu: Instagram: Emmanuel Jacob.

  • Ulemavu
  • Afya
  • Misaada

Soma Pia