Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Afya ya Kimwili

Kwa nini watumiaji wa ‘wheelchair’ husukumwa?

MARA nyingi ukitembea mtaani, hasa mijini, utaona mtu aliyeketi kwenye kiti-mwendo (wheelchair), anasukumwa na mtu mwingine.

Jumatatu, 24 Agosti 2026 · 06:00Dakika 2 kusomaToleo 179, uk. 25

Inaonekana kama kitendo cha kutoa msaada au wema wa kawaida, lakini ukichunguza kwa undani, taswira hii inafichua ukweli mchungu kuwa tumeruhusu dhana potofu na miundombinu mibovu kumpokonya mtumiaji wa kiti-mwendo uhuru wake.

Kimsingi, kiti-mwendo hakikubuniwa ili kumfanya mtu awe tegemezi wa kusukumwa kila mahali; ilibuniwa kuwa chombo cha kumfanya mtu ajitegemee na atembee kwa uhuru wake mwenyewe. Lakini kwa nini kila tunayemwona mjini leo anasukumwa?

Kwa wasomaji wa gazeti la Pambazuko makala hii imeangazia baadhi ya sababu zinazopelekea jambo hili angalau kwa ufupi ambazo ni pamoja na mchanganyiko wa mazingira magumu, sababu za kiafya, au wakati mwingine, ukosefu wa uelewa wa kijamii.

Mazingira yasiyofikika: Mitaa yetu imejaa ngazi ndefu, barabara zisizo na sehemu rasmi ya kushika (ramps), miundombinu mibovu na kando za barabara zilizoinuka mno. Katika mazingira kama haya, kujisukuma mwenyewe inakuwa vigumu.

Uchovu wa kimwili; kujisukuma mwenyewe kunahitaji nguvu kubwa ya mikono na kifua.

Mtu anaposafiri umbali mrefu katikati ya mji, akiwa anatumia manual wheelchair, uchovu unamlazimu kutafuta msaada.

Hali za kiafya na majeraha; Watu wenye hali kama vile kupooza mikono, kiwiliwili na miguu, ugonjwa wa mfumo wa fahamu (Multiple Sclerosis), au wale wanaouguza majeraha ya muda mfupi, wanaweza kukosa uwezo wa kutosha wa mikono au nguvu za kujisukuma.

Pamoja na kwamba kutoa msaada ni jambo la kiutu, kuna tatizo kubwa linalojitokeza mara kwa mara: watu kuwasukuma watumiaji wa viti mwendo na wakati mwingine bila hata kuwaomba ridhaa au idhini.

Kitendo hiki kinachukuliwa na wengi kama wema, lakini katika ulimwengu wa kisasa na haki za watu wenye ulemavu, ni ukiukaji mkubwa wa mipaka ya mtu.

Kiukweli ni muhimu jamii ifahamu kumsukuma mtumiaji wa kiti mwendo hupoteza uhuru wake kujiamulia.

Unamnyima mtu haki ya kuchagua wapi aende, kwa kasi gani, na kwa wakati gani. Vilevile, humfanya mtu aonekane kama mtoto.

Kitendo hiki kinajenga taswira kwamba mtu mwenye ulemavu ni dhaifu, hawezi kujifanyia maamuzi, na anahitaji “kusaidiwa” kila wakati.

Ni wakati sasa wa kubadili mtazamo wetu kama jamii. Usawa wa kweli sio tu kutoa msaada; ni kutengeneza mazingira yanayomwezesha kila mtu kujitegemea na kuheshimu utu na mipaka ya kila binaadamu.

Mwandishi: Emmanuel Jacob, Ofisa Mfiziotherapia (Mwenyekiti wa Tanzania Physiotherapy Initiative). Simu: Instagram: Emmanuel Jacob

  • Ulemavu
  • Afya

Soma Pia