Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Kona ya Dkt. Bisimba

Hakuna ugaidi au kuna viashiria? Tumwamini nani?

KUNA kauli ambazo zimetolewa na viongozi wawili katika wizara moja, tena ndani ya kipindi kifupi.

Jumatatu, 10 Agosti 2026 · 06:15Dakika 3 kusomaToleo 177, uk. 11

Waziri wa Mambo ya Ndani, Patrobas Katambi alisema hakuna ugaidi nchini, bali kunaweza kuwa na viashiria vya matendo ya kigaidi.

Waziri Katambi alisema haya wakati akijaribu kufafanua suala la kukamatwa watu na akajaribu kuonyesha jinsi ambavyo hakuna mtu aliye juu ya sheria na tunaongozwa na Katiba, Sheria ya Kanuni ya Adhabu na hata Sheria ya Ugaidi.

Katika maelezo yake, akaweka msisitizo kuwa Tanzania hakuna ugaidi.

Lakini kabla yake tuliisikia kauli ya Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, akisema hadi wakati huo jeshi hilo lilikuwa limewakamata watu 130 kwa tuhuma zinazohusiana na ugaidi.

Katika maelezo yake Misime alieleza wapo waliokamatwa na vilipuzi na wako waliosikika wakila njama ya kuua viongozi wa serikali, kuwanyang’anya polisi silaha, kuharibu miundombinu ya umeme na kukata miti ili kuwazuia polisi wasifike kwa urahisi kutoa msaada.

Na kwa kuonyesha kuwa Jeshi la Polisi linajua jambo linalolifanya katika suala hili la ugaidi tayari limeshawafikisha watu 36 mahakamani kwa tuhuma za ugaidi. Hadi hatua hiyo, hapo suala la ugaidi hauwezi kulichukulia kama propaganda tu, kwani limeshachukuliwa hatua kisheria.

Hapa mwananchi aamini kauli ipi? Waliamini Jeshi la Polisi ambalo limeshachukua hatua za kukabiliana na ugaidi au tumwamini waziri ambaye anasisitiza kuwa hakuna ugaidi!

Kama tukimwamini waziri, ina maana kuwa Jeshi la Polisi limewakamata watu kwa tuhuma ambazo hazipo!

Lakini Jeshi la Polisi limeshawafikisha watu mahakamani kwa tuhuma za ugaidi. Siamini kuwa chombo hiki mahiri katika ulinzi wa sheria kinaweza kuchukua hatua kali kama hii kwa kuzingatia tu kuwa kuna viashiria.

Umma unahitaji ufafanuzi utakaoondoa mkanganyiko hasa kwa kuwa ugaidi ni jambo hatari sana.

Hili ni tishio kubwa, siyo hapa nchini tu bali hata kwa wageni ambao wanaitembelea nchi yetu kama watalii, wanafunzi, watafiti, wafanyabiashara, viongozi au wawekezaji.

Suala la ugaidi ni zito kiusalama nchini na duniani, ambalo hapa nchini lina sheria mahsusi. Katika kuongelea masuala ya kiusalama katika taifa tahadhari kubwa inahitajika katika utoaji wa taarifa.

Kauli zinazotoka kwa viongozi zinatakiwa ziwe zinazoweza kujenga imani, kutoa mwelekeo mmoja na kuhakikisha wananchi wanaelewa hali halisi bila kupatwa na hofu wala kupotoswa.

Unahitajika uwepo wa uwazi unaofaa na mawasiliano yanayowiana kwani hilo nalo ni sehemu ya usalama.

Tukiangalia pia upande mwingine kwa hawa wageni nchini, wawekezaji na hata wadau wa maendeleo uthabiti wa taarifa zilizo rasmi ni jambo la muhimu na la msingi sana.

Unapotoka ujumbe unaoonekana kutofautiana au usioonekana bayana kimaana na kimantiki yanaweza kuzuka maswali kwao ni ipi hali halisi ya usalama katika nchi.

Taswira ya nchi hujengwa siyo kwa hali ya usalama ilivyo, bali pia kwa namna mamlaka zinavyowasiliana kuhusu hali hiyo.

Kwa hali kama hizi mamlaka inapaswa kuelezea kwa uwazi tofauti zilizopo kati ya ‘viashiria vya ugaidi’ ‘tuhuma za ugaidi’ na ‘uwepo wa ugaidi. ’ Umuhimu wa ufafanuzi huu ni kuwawezesha wananchi kuelewa kinachoendelea na waweze kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa msingi wa taarifa sahihi na zinazoeleweka.

Ukiangalia hizo ni dhana tofauti kabisa zinazopaswa kuangaliwa kwa vile hayo ni mambo tofauti kabisa kisheria na hata kiusalama.

Katika masuala nyeti kiasi hiki, kauli zinazolingana na zinazofafanua hali halisi siyo jambo la hiari, ni sehemu ya kujenga imani ya umma kwa muktadha wa kulinda maslahi ya taifa.

Mwandishi wa safu hii ya kila wiki, ni mwanaharakati wa demokrasia, haki za binadamu na mwanazuoni wa falsafa ya sheria. Anapatikana kwa namba.

  • Ugaidi
  • Usalama
  • Haki za binadamu

Soma Pia