HESLB yavunja rekodi, yatenga 1.06/-tr kuwakopesha wanafunzi
Idadi ya wanufaika yaongezeka, makusanyo ya mikopo yavunja rekodi huku matumizi ya teknolojia yakiboresha huduma na kuimarisha uwekezaji katika rasilimali watu.
BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imeendelea kupiga hatua kubwa katika utoaji wa mikopo, urejeshaji wa fedha na matumizi ya teknolojia, huku bajeti yake ya mwaka wa masomo 2026/27 ikifikia kiwango cha kihistoria cha Sh trilioni 1.06.
Fedha hizo zinatarajiwa kugharimia masomo ya wanafunzi wasiopungua 300,000, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kupanua fursa za elimu ya juu na kuongeza idadi ya Watanzania wenye ujuzi unaohitajika katika kukuza uchumi wa taifa.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, amesema mafanikio hayo yameifanya Bodi kuwa miongoni mwa taasisi muhimu katika utekelezaji wa mikakati ya Serikali ya kuendeleza rasilimali watu na kujenga uchumi wenye ushindani.
Dkt. Kiwia alieleza hayo Jumatatu, Oktoba 12, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati akiwasilisha taarifa ya mafanikio ya Bodi katika kipindi cha miaka mitano mbele ya wahariri wa vyombo vya habari, kwenye mkutano ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR).
Alisema katika kipindi hicho, HESLB imebadilika kutoka taasisi inayojikita zaidi katika utoaji wa mikopo na kuwa taasisi inayosimamia mnyororo mzima wa ufadhili wa wanafunzi, kuanzia maombi, uchambuzi, upangaji na malipo hadi huduma kwa wateja na urejeshaji wa mikopo.
Kwa mujibu wa Dkt. Kiwia, mabadiliko hayo yanaonesha namna Serikali inavyoendelea kutambua umuhimu wa elimu ya juu kama uwekezaji wa kimkakati katika nguvu kazi na maendeleo ya uchumi.
Bajeti ya Sh trilioni 1.06 kwa mwaka wa masomo 2026/27 ni ongezeko la asilimia 15.6 ikilinganishwa na Sh bilioni 916.7 zilizotolewa mwaka 2025/26 na kuwanufaisha wanafunzi 289,932.
Dk Kiwia alisema katika awamu ya kwanza ya upangaji wa mikopo na ruzuku iliyotangazwa Oktoba 10, 2026, jumla ya wanafunzi 165,775 walipangiwa fedha zenye thamani ya Sh bilioni 535.7.
Kati ya wanufaika hao, wanafunzi wapya 74,769 wa shahada ya kwanza walipangiwa mikopo ya Sh bilioni 246.88, huku wanafunzi 8,538 wa stashahada wakipangiwa Sh bilioni 22.9.
Aidha, wanafunzi 873 walipangiwa ruzuku ya Sh bilioni 4.5 kupitia programu ya Samia Scholarship.
Kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo, wanafunzi 79,115 wa shahada ya kwanza walipangiwa Sh bilioni 252.4, huku wanafunzi 1,554 wa stashahada wakipangiwa Sh bilioni 3.8.
Mikopo ya stashahada yapanuliwa
Moja ya mafanikio muhimu yaliyotajwa na Dkt. Kiwia ni kupanuliwa kwa mikopo hadi ngazi ya stashahada, hatua inayolenga kuongeza idadi ya vijana wenye ujuzi wa kitaalamu na kiufundi.
Mpango huo ulioanza mwaka wa masomo 2023/24 umeongeza fursa kwa wanafunzi ambao awali hawakuwa katika wigo wa kawaida wa mikopo ya elimu ya juu.
Katika mwaka wa masomo 2026/27, HESLB inatarajia kugharimia wanafunzi 24,978 wa stashahada katika fani za kipaumbele, wakiwemo wanafunzi wapya 14,000.
Upanuzi huo una umuhimu wa kiuchumi kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya wataalamu wa ngazi mbalimbali katika viwanda, huduma, teknolojia na sekta nyingine zinazochochea uzalishaji.
Sambamba na hatua hiyo, Bodi imeendelea kupanua programu maalumu za ufadhili, hususan katika masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati.
Programu ya Samia Scholarship iliyoanzishwa mwaka 2022/23 ikiwa na wanufaika 636, inatarajiwa kugharimia wanafunzi 2,738 mwaka huu, wakiwemo wapya 1,000.
Makusanyo yavunja rekodi
Katika hatua nyingine, Dkt. Kiwia alisema HESLB imepata mafanikio makubwa katika urejeshaji wa mikopo, jambo ambalo ni muhimu katika kuhakikisha fedha zinazokusanywa zinatumika kuwasaidia wanafunzi wengine.
Katika mwaka wa fedha 2025/26, Bodi ilikusanya Sh bilioni 235.5, ikiwa ni kiwango cha juu zaidi kuwahi kukusanywa tangu kuanzishwa kwake.
Makusanyo hayo yalivuka lengo la Sh bilioni 220 kwa asilimia saba.
Mafanikio hayo yanaonesha ongezeko kubwa kutoka Sh bilioni 177 zilizokusanywa mwaka 2023/24 na Sh bilioni 194 mwaka 2024/25.
Kwa ujumla, kuanzia mwaka 2005/06 hadi Juni 2026, HESLB imekusanya Sh trilioni 1.91, sawa na asilimia 69 ya Sh trilioni 2.77 za mikopo iliyoiva.
Ili kuimarisha urejeshaji, Bodi imeanzisha kampeni mbalimbali, ikiwemo Kiduchu Fresh Tunasonga, inayowahamasisha wanufaika wenye kipato kidogo kuanza kurejesha mikopo kwa kiasi wanachoweza kumudu.
Dkt. Kiwia alisisitiza kuwa urejeshaji wa mikopo ni msingi wa uendelevu wa mfuko kwa sababu fedha zinazorejeshwa zinasaidia kugharimia masomo ya vijana wengine.
Hata hivyo, alikiri kuwa bado kuna changamoto ya wanufaika wanaodaiwa takribani Sh bilioni 800 ambao hawajajitokeza kurejesha mikopo yao.
Alisema kuwafikia wahitimu wanaofanya shughuli katika sekta isiyo rasmi ni miongoni mwa changamoto zinazohitaji mikakati zaidi.
Teknolojia yaimarisha huduma
Dk Kiwia alisema matumizi ya mifumo ya kidijitali yamechangia kuongeza ufanisi, kupunguza muda wa kushughulikia maombi na kurahisisha malipo kwa wanafunzi.
Kupitia mfumo wa maombi na usimamizi wa mikopo wa OLAMS, akaunti maalumu za waombaji (SIPA), programu ya simu ya HESLB na mfumo wa malipo wa DiDiS, Bodi imeendelea kupunguza urasimu katika utoaji wa huduma.
Aidha, imeanzisha mifumo inayotumia akili unde, ikiwemo Bwanaboom na Bibiboom, inayosaidia kutoa majibu ya haraka kwa wanafunzi na wananchi wanaohitaji taarifa kuhusu mikopo.
Katika eneo la utawala bora, HESLB imepata ithibati ya kimataifa ya ISO 9001:2015 ya usimamizi wa ubora wa huduma na hati safi za ukaguzi wa hesabu katika kipindi chote cha utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Tano.
Bodi ilitekeleza asilimia 82 ya Mpango Mkakati wa 2021/22 hadi 2025/26 na kufunga asilimia 80 ya hoja za ukaguzi wa hesabu.
Pia, asilimia 72 ya waombaji mikopo waliokuwa na sifa walipangiwa mikopo.
Mwelekeo wa Dira 2050
Dkt. Kiwia alisema Mpango Mkakati wa Sita wa HESLB wa mwaka 2026/27 hadi 2030/31 unalenga kuibadilisha Bodi kuwa mfuko mpana wa kitaifa wa kugharimia elimu ya juu.
Mkakati huo unaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kuhakikisha angalau asilimia 25 ya Watanzania wanapata elimu ya juu ifikapo mwaka 2050.
Kwa mujibu wake, kufanikisha lengo hilo kutahitaji kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi, kupanua vyanzo vya fedha, kuongeza urejeshaji wa mikopo na kuendelea kuboresha mifumo ya kidijitali.
Kwa upande wa uchumi, mafanikio ya HESLB yanaonesha umuhimu wa kuwekeza katika elimu kama njia ya kuongeza uzalishaji, kukuza ajira na kujenga nguvu kazi yenye ujuzi.
Hata hivyo, changamoto kubwa inayobaki ni kuhakikisha ongezeko la wanafunzi wanaopata mikopo linaenda sambamba na ubora wa elimu, mahitaji ya soko la ajira na uwezo wa mfuko kujiendesha kwa uendelevu.
Kwa kufanya hivyo, uwekezaji katika elimu ya juu hautakuwa tu msaada kwa wanafunzi, bali pia msingi wa kujenga uchumi imara na wenye ushindani katika miaka ijayo.
Umebakiwa na makala 2 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.