Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Latra yataka sekta ya usafiri kujipanga kwa malipo ya kielektroniki

Mkurugenzi wa LATRA, Dkt. Habib Suluo, asema miundombinu inaboreshwa, lakini watoa huduma lazima waendane na teknolojia; bodaboda, bajaji na magari ya kukodi yazidi kubadili sura ya usafiri nchini

Alhamisi, 24 Septemba 2026 · 13:05Dakika 3 kusoma
Hata daladala nazo zinatakiwa kulipisha abiria nauli kwa mifumo ya kielektroniki.
Hata daladala nazo zinatakiwa kulipisha abiria nauli kwa mifumo ya kielektroniki.

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imetaka watoa huduma za usafiri nchini kuanza kujiandaa kwa matumizi mapana ya mifumo ya kielektroniki katika malipo ya nauli, ada na tozo, ikisema ujenzi wa miundombinu pekee hautoshi bila mifumo bora ya uendeshaji na huduma.

Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Dkt. Habib Suluo, amesema hayo leo, Septemba 24, 2026, alipokutana na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam na kueleza mwenendo wa sekta na utendaji wa mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Akieleza hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya sekta ya usafiri, Dkt. Suluo alisema Tanzania imeendelea kuwekeza katika miundombinu, lakini changamoto inayofuata ni kuhakikisha mifumo ya uendeshaji na watoa huduma wanaendana na kasi ya mabadiliko hayo.

“Kwa lugha rahisi tunaweza kusema, ‘hardware is ready, but what about software?’” alisema.

Kauli hiyo, kwa mujibu wake, ina maana kwamba kuwa na miundombinu mizuri pekee hakutoshi ikiwa mifumo ya uendeshaji, teknolojia na watoa huduma hawajajiandaa kuitumia kwa ufanisi.

Nauli za kielektroniki

Moja ya maeneo ambayo LATRA inataka wadau kuanza kujiandaa nayo ni kuhamia katika miamala ya kielektroniki.

Dkt. Suluo alisema watoa huduma wanapaswa kufahamu matakwa ya kisheria yanayohusu miamala hiyo na kuanza kufanya maandalizi ya mifumo itakayowawezesha kuyatekeleza.

Kwa sekta ya usafiri ardhini, mabadiliko hayo yanagusa malipo ya ada na tozo pamoja na nauli zinazolipwa na abiria.

Katika wasilisho lake, Dkt. Suluoalibainisha kuwa bado wapo abiria ambao wanalipia tiketi zao kwa fedha taslimu.

Kwa mujibu wa takwimu ambazo LATRA imezikusanya, kuanzia mwaka 2022/23 hadi mwaka wa fedhga uliopita, jumla ya watu milioni 62.2 walisafiri wka mabasi nchini na kulipa nauli ya jumla ya shilingi trilioni 2.13.

“Kati ya kiasi hicho cha fedha kilichokusanya shilingi trilioni 1.9 zililipwa kama fedha taslimu wakati ipo mifumo ya kufanya malipo ya kielektroniki,” alibainisha Dkt. Suluo.

LATRA imewataka wadau kusoma na kuelewa masharti yanayowahusu na kufanya maandalizi mapema badala ya kusubiri utekelezaji uwakute bila mifumo inayohitajika.

Bodaboda na bajaji zabadili soko

Wakati teknolojia ikitarajiwa kubadili namna abiria wanavyolipia huduma, LATRA inasema muundo wenyewe wa soko la usafiri ardhini nao umebadilika kwa kiasi kikubwa.

Mamlaka hiyo inasimamia makundi matatu makuu ya vyombo vya usafiri: magari ya abiria (PSV), magari ya mizigo (GSV) na magari ya kukodi.

Kwa mujibu wa Dkt. Suluo, ukuaji wa magari ya kawaida ya abiria umekabiliwa na ushindani unaotokana na kuongezeka kwa matumizi ya magari binafsi pamoja na bodaboda na bajaji.

“Vyombo hivyo vimepanua chaguo la usafiri kwa wananchi, lakini wakati huohuo vimebadili mazingira ya ushindani kwa waendeshaji wa mabasi,” anasema Dkt. Suluo.

Mabadiliko makubwa zaidi yanaonekana katika kundi la magari ya kukodi ambako LATRA imeshuhudia ongezeko la leseni.

Kundi hilo linajumuisha bodaboda, bajaji, teksi, magari ya shule, magari ya watalii na baadhi ya magari yanayotoa huduma maalumu, ikiwemo kusafirisha abiria kwenda na kutoka viwanja vya ndege.

Baadhi ya aina za magari ambazo hapo awali zilihesabiwa katika makundi mengine sasa zimejumuishwa katika kundi la magari ya kukodi, jambo ambalo pia limechangia ukuaji unaoonekana katika takwimu za leseni.

Usafiri ni zaidi ya basi

Dkt. Suluo alisema umuhimu wa sekta ya usafiri haupaswi kupimwa kwa idadi ya magari pekee kwa sababu ina uhusiano wa moja kwa moja na shughuli nyingine nyingi za uchumi.

Msafiri wa masafa marefu, kwa mfano, anaweza kuhitaji hoteli, chakula, teksi au gari la kukodi na huduma nyingine anapokuwa safarini au anapofika anakokwenda.

Hivyo, mabadiliko katika sekta ya usafiri yana athari katika hoteli, migahawa, utalii na biashara nyingine zinazotegemea mtiririko wa watu.

Kwa mtazamo huo, ukuaji wa usafiri unaweza kufungua fursa za biashara katika mnyororo mpana zaidi kuliko kampuni za mabasi pekee.

Wananchi watakiwa kuwa sehemu ya usimamizi

Pamoja na kuimarisha mifumo yake ya udhibiti, LATRA imewataka wananchi kushiriki katika kuboresha sekta hiyo kwa kutoa taarifa wanapokutana na ukiukwaji au huduma zisizokidhi viwango.

Dkt. Suluo alisema taarifa zinazowasilishwa kwa mamlaka hufanyiwa kazi kwa kufuata taratibu zilizowekwa.

Lengo, alisema, ni kuhakikisha abiria wanapata huduma salama, bora na zenye ufanisi.

Soma Pia