Lissu aibua utata wa hati ya mashtaka, ahoji: Serikali iliyotishiwa ni ipi?
Katika hoja zake za mwisho, adai mashtaka hayajabainisha watu au chombo cha Serikali kinachodaiwa kutishiwa; Mahakama Kuu bado haijatoa uamuzi kuhusu hoja hizo

Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, ameibua hoja kuhusu namna shtaka la uhaini linalomkabili lilivyoandaliwa, akidai kuwa hati ya mashtaka haijaweka wazi watu, viongozi au chombo cha Serikali ambacho anadaiwa kuwashawishi wananchi kukitishia.
Lissu ametoa hoja hiyo wakati akiendelea kuwasilisha hoja zake za mwisho mbele ya jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu, katika hatua za mwisho za kesi hiyo.
Anakabiliwa na shtaka moja la uhaini chini ya Kifungu cha 39(2)(d) cha Kanuni ya Adhabu, linalotokana na kauli anazodaiwa kuzitoa Aprili 3, 2025 kuhusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo. Upande wa mashtaka unadai kwamba Lissu aliwashawishi wananchi kuzuia uchaguzi huo kupitia kauli zilizotolewa na kusambazwa mtandaoni.
Hata hivyo, katika hoja zake za mwisho, Lissu anapinga namna shtaka hilo lilivyoundwa na kudai kuwa halimpi maelezo ya kutosha kuhusu kosa analodaiwa kulitenda.
Moja ya hoja zake ni kwamba hati ya mashtaka inamtuhumu kuwashawishi wananchi kuitishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini hati hiyo ya mashtaka haielezi kwa undani ni sehemu gani ya Serikali au maofisa gani waliokuwa walengwa wa tishio hilo.
“Ni nani hasa niliyemtishia? Ni Rais, Waziri Mkuu, Makamu wa Rais, Polisi au nani? Ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji gani niliyemtishia?” alihoji Lissu.
‘Serikali ni pana’
Katika kujenga hoja hiyo, Lissu alirejea masharti ya Katiba ambayo, kwa tafsiri yake, yanaonesha kuwa dhana ya “serikali” ni pana.
Alidai kuwa inaweza kujumuisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, mamlaka za serikali za mitaa, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na watu wanaotekeleza majukumu ya kiserikali.
Kutokana na upana huo, Lissu alidai upande wa mashitaka ulipaswa kutaja kwa uwazi sehemu au mtu aliyelengwa ili aweze kufahamu kwa usahihi tuhuma zinazomkabili na kuandaa utetezi wake.
“Walipaswa kuniambia ni serikali ipi iliyotishiwa,” alisema Lissu kwa msisitizo.
Lissu alirejea uamuzi katika kesi ya Isdory Patrice, akisema unaunga mkono hoja kwamba mshtakiwa anapaswa kupewa maelezo ya kutosha kuhusu shitaka ili aweze kuandaa utetezi wake.
Pia alirejea uamuzi wa Mahakama Kuu katika kesi ya Freeman Mbowe, ingawa alikiri kwamba uamuzi huo hauwezi kulifunga kisheria jopo linalosikiliza kesi yake.
Hoja yake ilikuwa kwamba maelezo ya kina katika hati ya mashtaka ni muhimu katika kulinda haki ya mshtakiwa kufahamu kwa usahihi kesi anayopaswa kujibu.
Ahoji tafsiri ya ‘wananchi’
Lissu pia aliibua hoja nyingine kuhusu tofauti ya maneno yaliyotumika katika kifungu cha sheria na yale yaliyowekwa katika hati ya mashtaka.
Kwa mujibu wa hoja yake, kifungu cha sheria kinachotumika kinasema kuhusu kumshawishi “mtu au kundi la watu”, wakati hati ya mashtaka dhidi yake inazungumzia “wananchi”.
Alidai kuwa tofauti hiyo inaongeza utata kuhusu tuhuma mahsusi anayopaswa kujibu.
Ahoji pia hoja ya kuzuia uchaguzi
Hoja nyingine iliyowasilishwa na Lissu inahusu madai kwamba moja ya madhumuni ya vitendo anavyotuhumiwa navyo ilikuwa kuzuia uchaguzi.
Lissu alidai kuwa “kuzuia uchaguzi” si mojawapo ya madhumuni yanayotambuliwa katika kifungu cha sheria ya jinai ambacho ameshitakiwa nacho.
Kutokana na tafsiri hiyo, alidai kwamba ameshitakiwa kwa kitendo ambacho, kwa namna kilivyoelezwa katika hati ya mashtaka, hakikuainishwa kuwa kosa chini ya kifungu hicho.
‘Lazima nijitetee kwa kila nilicho nacho’
Wakati shauri likielekea ukingoni, upande wa mashitaka ulimkumbusha Lissu kuhusu muda uliokuwa umebaki katika ratiba ya kesi.
Lissu, hata hivyo, alisisitiza uzito wa shitaka linalomkabili na umuhimu wa kupewa nafasi ya kutosha kuwasilisha hoja zake.
“Hii ni kesi yenye adhabu ya kifo. Lazima nijitetee kwa kila nilicho nacho,” alisema.
Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru akisaidiwa na Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.
Kesi yafikia hatua za mwisho
Hoja hizo zinawasilishwa baada ya upande wa utetezi kufunga ushahidi wake Septemba 18, 2026.
Lissu alikuwa amepanga kuwaita baadhi ya viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama kuwa mashahidi, akiwemo Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna wa Polisi Ramadhani Kingai, Rais samia suluhu Hassan, Makamu wa rais wa zamani, Dkt. Phillip Mpango na waziri Mkuu wa zamani, Kassim majaliwa.
Hata hivyo, Maghakama ilizuiwa kuitwa kwa Rais Samia, Dkt. Mpango, Majaliwa na Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa.
Lakini hata wale ambao Mahakama iliruhusu waitwe hawakufika mbele ya mahakama kutokana na kukataa kumtetea Lissu.