Habari
Hofu yatanda ajali ya chopa ikihisiwa kumuua Chivayo
Taarifa za kifo cha bilionea wa Zimbabwe, Wicknell Chivayo, zinaendelea kusambaa, ingawa serikali wala familia yake bado hawajathibitisha. Pambazuko tunaiandika kwa uangalifu na utegemezi wa habari za vyombo vingine.
BILIONEA maarufu wa Zimbabwe, Wicknell Chivayo, anatajwa kuwa miongoni mwa watu waliofariki dunia baada ya chopa waliyokuwa wakisafiria kupata ajali.
Taarifa kutoka mamlaka za Serikali ya Zimbabwe zinaeleza kuwa chopa hiyo ilianguka jioni ya leo- Septemba 30 katika eneo la Marondera.
Hata hivyo, hadi wakati wa kuandaa habari hii, mamlaka za Zimbabwe hazijamtaja Chivayo kuwa miongoni mwa waliokuwamo, ingawa mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari vimetangaza kufariki kwake.
Msemaji wa Serikali ya Zimbabwe, Nick Mangwana, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema hakuna aliyenusurika.
Mangwana amesema miongoni mwa waliokuwamo alikuwa mfanyabiashara mashuhuri, lakini hakutaja jina lake.
Polisi wamesema ajali ilitokea karibu saa 11 jioni kwa saa za Zimbabwe na kwamba maelezo zaidi yangetolewa baada ya wahudumu wa dharura kufika eneo la tukio.
Serikali imesema Jeshi la Polisi litatangaza majina ya wahanga baadaye. Kwa sasa, familia na umma wanasubiri taarifa hiyo ili kujua kwa uhakika nani walikuwa kwenye chopa.
Taarifa za mwanzo pia zinatofautiana kuhusu idadi ya watu waliokuwamo; polisi walisema walikuwa sita, ilhali taarifa iliyonukuliwa na Shirika la Habari la Reuters la Uingereza inataja mfanyabiashara, abiria wengine wanne na marubani wawili.
Chivayo amekuwa bilionea mwenye kutajwa zaidi kupata utajiri wake kwa njia zinazolezwa kuwa tata, huku akionekana kuwa na ukaribu mkubwa na viongozi wengi wa Afrika Mashariki na Kati.
Pambazuko Digital inaendelea kufuatilia hatua kwa hatua kuhusu ajali hiyo na hasa taarifa za kifo cha Chivayo.
- ajali
- chopa
- chivayo
- bilionea
- zimbabwe