Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Habari

Jamii Africa yaleta suluhisho haki ya habari kwa kila mtu

Pamoja na teknolojia ya mawasiliano kukua zaidi duniani, lakini wapo baadhi ya watu wanakosa haki ya kupata habari kwa kuwa hawana vifaa aghali, sasa Jamii Africa imekuja na utatuzi wa jambo hilo.

Jumatano, 30 Septemba 2026 · 12:20Dakika 2 kusoma

MTANZANIA mwenye simu ya kawaida (Kiswaswadu), sasa anaweza kuuliza swali kwa sauti na kupata jibu kutoka mfumo wa akili unde bila kutumia intaneti au simu janja.

Huduma hiyo, inayoitwa AVA (Ask Viamo Anything), imezinduliwa jijini Dar es Salaam na Jamii Africa kwa kushirikiana na kampuni ya teknolojia ya Viamo kutoka Canada.

Uzinduzi ulifanyika Septemba 29, 2026, ukihudhuriwa na wadau wa habari, asasi za kiraia na sekta ya teknolojia. Balozi wa Canada nchini Tanzania, Emily Burns, alikuwa mgeni rasmi.

Jamii Africa inaeleza kuwa mtumiaji wa AVA hupiga simu, huuliza swali kwa sauti na kusikiliza jibu linalotolewa na mfumo wa AI. Njia hiyo inalenga kuwafikia pia wananchi ambao hawatumii huduma za intaneti au hawamiliki simu janja.

Mkuu wa Programu wa Jamii Africa, Ziada Seukindo, alisema mradi huo ni sehemu ya juhudi za kuwezesha watu kupata taarifa sahihi na za kuaminika.

Alisema upatikanaji wa taarifa hizo unaweza kuwasaidia kufanya maamuzi kuhusu mambo yanayowagusa katika maisha ya kila siku.

Mkurugenzi wa Jamii Africa, Maxence Melo, alisema tofauti ya uwezo wa kutumia teknolojia na kumiliki vifaa vya mawasiliano, ikiwamo simu, kumewaacha baadhi ya wananchi nyuma katika kupata taarifa.

Melo alisema AVA inalenga kupunguza pengo hilo kwa kuwapa watu wa mijini na vijijini nafasi ya kuuliza maswali kwa kutumia simu walizonazo.

Alisema shirika hilo linakusudia kupanua wigo wa huduma kupitia ushirikiano na vyombo vya habari, serikali, asasi za kiraia, kampuni za simu na watengenezaji wa maudhui.

Balozi Burns aliipongeza Jamii Africa na Viamo kwa kuanzisha huduma hiyo. Alisema kutumia njia za kidijitali zinazofikika kwa urahisi kunaweza kusaidia wananchi kupata taarifa wanazozihitaji.

Uzinduzi wa AVA unaweka mkazo katika namna taarifa zinazotolewa kwa msaada wa AI zinavyoweza kufikishwa kwa watu wasioweza kuwa na simu janja.

Jamii Africa na Viamo wanataka kuona kwamba kila mtu anapata haki ya taarifa na majibu kwa maswali yake kwa kutumia simu ya kawaida bila kutegemea intaneti.

  • jamii africa
  • viamo
  • maxence melo
  • habari
  • tanzania

Soma Pia