Habari Kuu
Mgomo wa madereva wa mabasi janga, lavuruga uchumi, ratiba
Hakika usafiri wa abiria na mizigo ni nguzo muhimu ya kuimarisha uchumi. Hilo limedhihirika tangu jana wakati madereva wa mabasi walipogoma kufanya safari kutoka Dar es Salaam, Pambazuko linaeleza zaidi.
MABASI yaliyopaswa kuondoka Dar es Salaam kwenda mikoani yalibaki yameegeshwa katika Stendi ya Magufuli, Mbezi, Septemba 29, 2026, baada ya madereva kusitisha safari.
Abiria waliokuwa na tiketi walijikuta wakisubiri bila kujua lini wangeondoka, huku shughuli za usafirishaji na biashara zikivurugika.
“Nipo hapa tangu saa 12 asubuhi nataka kwenda Songea, lakini sijui mwafaka wangu kwa sababu, hata dereva wa basi langu simuoni,” alisema abiria Monica Salehe, akinukuliwa na Pambazuko Digital. Alilalamikia kukatiwa tiketi wakati safari haikuwa na uhakika.
Mgomo huo uliathiri mzunguko wa fedha katika sekta ya usafiri. Wamiliki wa mabasi walikosa mapato ya safari zilizokwama, huku biashara zinazotegemea abiria vituoni na usafirishaji wa bidhaa zikikabiliwa na kuchelewa kwa huduma.
Madereva walilalamikia faini, kufungiwa leseni na mfumo wa kukata pointi kwa makosa ya barabarani. Dereva Halfan Hakimu alisema; “Hatutaki kugoma, imetubidi kugoma tuna njaa na familia zetu wanatutegemea.” Baadhi ya wasafiri walirejea nyumbani, huku wengine wakibadili mipango ya kazi na safari.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Patrobas Katambi, alifika stendi hiyo na kuagiza suala la pointi lisitishwe ili malalamiko yashughulikiwe.
“Kama kuna mtu aliyekatwa pointi, nileteeni majina haraka sana ofisini kwangu,” alisema, akisisitiza kuwa hakuna dereva aliyepaswa kuadhibiwa kwa mfumo huo.
Awali, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Polisi, Awadh Juma Haji, alisema mfumo wa pointi bado haujaanza kutekelezwa.
“Mpaka sasa hakuna dereva ambaye leseni yake imeondolewa kwa kukatwa pointi,” alisema. Polisi pia ilionya dhidi ya kuwazuia madereva wanaotaka kuendelea na safari.
Mvutano huo ulionyesha jinsi usafiri wa mikoani ulivyo muhimu kwa uchumi wa kila siku. Basi linapokwama Dar es Salaam, siyo abiria pekee anayepoteza muda, bali mipango mingi hukwama ikiwamo safari za kazi, miadi na mizigo inayotarajiwa kufika mikoani nayo huchelewa.
"Serikali na madereva wanahitaji suluhu inayolinda usalama barabarani bila kuwaacha wasafiri wakilipia gharama za mgogoro," alisikika abiria mwingine aliyekataa kuandikwa jina wala kupigwa picha.
Taarifa zilizofikia Pambazuko Digital mchana wa leo - Septemba 30, zinaeleza kuwa mgomo huo umesitishwa baada ya serikali kuingilia kati.
- mgomo
- madereva
- dar
- safari