Habari
Hospitali Aga Khan yazidi kubanwa
HOSPITALI ya Aga Khan ya jijini Dar es Salaam imezidi kubanwa na mgonjwa anayedai kupata madhara ya kiafya baada ya kutokea hitilafu katika mashine ya uchunguzi wa kitabibu inayotumia miale ya Xray na teknolojia ya kompyuta kutengeneza picha za ndani ya mwili wa binadamu (CT-Scan), iliyolipuka wakati mgonjwa huyo akiwa ndani yake.
Mdai, ambaye ni mwanafunzi wa Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT) (jina lake tunalihifadhi kwa sasa), aliipa siku 14 Hospitali ya Aga Khan kujibu wito wa kushiriki katika mazungumzo ya usuluhishi wa nje ya mahakama kutokana na madai ya tukio la hitilafu ya mashine ya CT-Scan lililomkumba wakati akifanyiwa uchunguzi hospitalini hapo Juni 4, 2026.
Agosti, 2026 Pambazuko lilizungumza na baba mzazi wa kijana huyo, Godwin Rwakatale, ambaye alikiri kutokea kwa tukio hilo ambapo alisema limemsababishia mwanawe tatizo la kupumua ambalo hakuwahi kuwa nalo awali.
Rwakatale alisema kutokana na kadhia hiyo ya kiafya, mwanawe ametoa jukumu kwa wanasheria wake kuidai Hospitali ya Aga Khan fidia ya Shilingi milioni 350. Hata hivyo, hosptali hiyo haijatekeleza madai hayo hadi leo wakati gazeti hili linaanza kusambazwa saa 6:01 usiku.
Kwa mujibu wa Rwakatale, hospitali hiyo imekaa kimya bila kujibu chochote hatua iliyomfanya mwanawe kuwaagiza wanasheria wake kuwaandikia barua nyingine kwa ajili ya kutafuta suluhisho la mgogoro huo kabla ya hatua zaidi za kwenda mahakamani.
Pambazuko limeona barua ya Mendez Consultancy & Agency, iliyosainiwa na wakili wake, Mathiew Y. Ngaga, kupitia barua ya Septemba 14, 2026 yenye kumbukumbu MCA/BR/2026/09/3, ambayo inasema mteja wao yuko tayari kutafuta suluhu ya amani kabla ya kuanzishwa kwa shauri rasmi mahakamani.
Barua hiyo inaitaka Hospitali ya Aga Khan kushiriki mazungumzo ya usuluhishi wa nje ya mahakama kuhusu madai ya majeraha aliyopata baada ya kutokea hitilafu katika mashine hiyo Juni 4, 2026.
Aidha, wanasheria hao wameitaka Hospitali ya Aga Khan kutoa majibu ndani ya siku 14 tangu kupokea barua hiyo, ikieleza iwapo iko tayari kushiriki katika mazungumzo ya usuluhishi na kuteua wawakilishi wenye mamlaka ya kujadiliana na kufikia makubaliano.
Aidha, barua hiyo ambayo imekuwa ya pili katika kipindi cha miezi miwili kwenda Hospitali ya Aga Khan, pia imeibua maswali kuhusu usalama wa mashine husika, matengenezo yake, namna ilivyokuwa ikiendeshwa pamoja na taratibu za kukabiliana na dharura wakati wa tukio.
Hoja zinazopendekezwa Pamoja na mambo mengine, wanasheria hao wanapendekeza Hospitali ya Aga Khan kuchunguza mazingira yaliyosababisha hitilafu ya mashine ya CT Scan Juni 4, 2026, aina na kiwango cha majeraha na matatizo ya kiafya yanayodaiwa kusababishwa na tukio hilo, gharama za matibabu ambazo tayari zimelipwa na mahitaji ya matibabu ya baadaye.
Mengine ni kuhusu fidia kwa maumivu, mateso, usumbufu, msongo wa kihisia na hasara nyingine zinazodaiwa, hatua za kurekebisha hali hiyo, dhamana au maelezo rasmi, pamoja na masharti mengine yatakayokubalika na pande zote kwa ajili ya kumaliza mgogoro huo.
Katika barua hiyo, kampuni hiyo pia imeitaka Hospitali ya Aga Khan kutoa nyaraka na taarifa zinazohusiana na tukio hilo ili kuwezesha mazungumzo yenye msingi wa taarifa kamili.
Nyaraka hizo ni pamoja na taarifa za tukio na ripoti za matukio ya Juni 4, 2026; ripoti za uchunguzi wa ndani na matokeo yake, iwapo zipo; pamoja na kumbukumbu za matengenezo, ukaguzi, upangaji wa vipimo vya mashine, huduma na marekebisho ya CTScan kwa kipindi husika.
Aidha, wameomba video za CCTV na kumbukumbu nyingine za kielektroniki zinazohusiana na eneo, tarehe na muda wa tukio, iwapo zinapatikana, pamoja na nyaraka nyingine zinazoweza kusaidia kubaini mazingira yaliyosababisha tukio hilo.
Umebakiwa na makala 2 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.
- Aga Khan
- Afya
- Hospitali