Habari Kuu
Utafiti: Kunywa chai ya moto sana kwachochea saratani
Ugonjwa wa saratani (kansa) umeendelea kuwa tishio huku wataalamu wakibaini vyanzo vyake kama Pambazuko linavyoweza kueleza zaidi kutokana na utafiti wa kisayansi.

IMEBAINIKA kuwepo kwa uhusiano wa moja kwa moja kati ya unywaji wa vimiminika vyenye joto kali sana na saratani ya umio; yaani mrija unaounganisha koo na tumbo.
Hayo yamebainishwa na watafiti kutoka Chuo cha Oxford nchini Uingereza, ambapo waliwafuatilia watu milioni moja katika utafiti huo.
Ufuatiliaji huo umekuja na matokeo yanayoonyesha kuwa watu wanaokunywa vinywaji vyenye joto kali sana walikuwa na hatari iliyoongezeka mara tatu ya kupata saratani hiyo.
Utafiti huo, ambao umechapishwa katika jarida la International Journal of Cancer, umebainisha kuwa kinywaji chochote chenye joto la nyuzi joto 65 au zaidi, kina uwezekano wa kuleta hatari hiyo ya afya kwa mtumiaji.
Kwa mujibu wa utafiti huo, kinywaji chenye mvuke wa joto kali kinaweza kuharibu utando wa seli wa bomba la chakula kuelekea tumboni. Kunywa vinywaji vya moto zaidi kwa mara sita au zaidi kwa siku, pia huongeza hatari hiyo, kulingana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wanaume na wanawake 977,282 wa umri wa kati; miaka 24 hadi 45.
Chai inayotayarishwa mara tu maji yanapochemka kikamilifu huwa na joto linalokaribia kiwango cha kuchemka, yaani nyuzi joto 100 na inapomiminwa kwenye kikombe, joto hilo hupungua hadi kufikia takriban nyuzi joto 90 au 95.
Hospitali ya Muhimbili yanena
Ofisa Lishe kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Kitengo cha MOI, Dkt. Zainab Tindi, anasema kunywa chai ya moto au vinywaji vya moto hakuleti saratani moja kwa moja, lakini Shirika la Afya Duniani (WHO) kupitia wakala wa utafiti juu ya saratani, limeweka wazi kwamba kunywa vinywaji vya moto sana mara nyingi kunaweza kusababisha jeraha la joto au uvimbe kwenye koo.
Dkt. Tindi ameliambia Pambazuko kuwa hilo pia linasababisha kupunguza kinga ya ute kwenye koo, hivyo vitu kadhaa vitaongeza hatari ya kupata saratani ya koo kwa sababu ukuta wa kinga ukiondoka viambata sumu ni rahisi kusababisha saratani.
“Chronic inflamation (mcharuko endelevu) unaweza badili tabia za chembe hai na kuongeza hatari ya kutengeneza saratani,” anasema Dkt. Tindi. Anasema inashauriwa kuwa vinywaji vya moto vitumike vikiwa na nyuzi joto 60°C ambayo ndio joto la kutengeneza chakula.
“Njia rahisi ni kama kinywaji au chai inakuunguza sehemu ya mbele ya ulimi, ipooze kwanza na unapotenga chai ikae walau dakika 3 hadi 5 ndio unywe ili ishuke joto kufikia 60°C,” anasema Dkt. Tindi.
Ushauri uliotolewa ni kusubiri kwa dakika chache kabla ya kunywa ili kinywaji hicho kipoe na kufikia kiwango cha joto salama zaidi. Shirika la Kutafiti Saratani la Uingereza (Cancer Research UK) linasema ni vigumu kubainisha muda kamili ambao kinywaji cha moto kinapaswa kuachwa ili kipoe.
“Lakini ikiwa una wasiwasi, tunashauri usubiri hadi kinywaji kiwe katika hali nzuri ya kunyweka badala ya kukinywa kikiwa bado cha moto sana,” lilisema shirika hilo.
Watafiti wanasema matokeo hayo, kutoka kwa utafiti wa takribani watu milioni moja, yanafanya hili kuwa jambo kubwa zaidi hadi sasa, katika kubaini uhusiano huo.
Katika utafiti huo, watu waliokunywa vinywaji vya moto sana walikuwa na hatari ya kupata saratani mara tatu zaidi kuliko wale wanaokunywa chai au kahawa ambayo siyo moto sana au vuguvugu, ingawa wataalamu wanasisitiza kwamba nafasi za jumla za kupata saratani hii ni ndogo.
Mtafiti mkuu na mtaalamu wa magonjwa yanayotokana na lishe katika Taasisi ya Afya – Chuo Kikuu cha Oxford nchini Uingereza, Dkt. Keren Papier amesema utafiti uliofanywa Amerika Kusini ambako watu wengi hunywa kinywaji cha mitishamba cha moto sana, tayari umeonyesha uhusiano kama huo kati ya vinywaji vya moto na saratani ya njia ya chakula.
“Utafiti zaidi unahitajika sasa ili kubaini viwango kamili vya joto la vinywaji vinavyohusishwa na hatari hii iliyoongezeka,” amesema Dkt. Papier.
Utafiti mwingine uliohusisha vijana 118 waliojaribu aina mbalimbali za kahawa nyeusi uligundua kuwa wengi wao waliona vinywaji hivyo kuwa vya moto kupita kiasi pale tu joto lake lilipofikia nyuzi joto 70 au zaidi.
Kulingana na mtengenezaji mmoja wa vikombe vya kahawa, kiwango bora cha joto kwa kahawa ya moto wakati wa safari ni kati ya nyuzi joto 49 na 60.
Kwa mujibu wa kampuni ya MTPak Coffee, iwapo mtengenezaji wa kahawa anataka ibaki na joto kwa muda mrefu zaidi, kama mteja akiomba iwe ya moto zaidi inaweza kutolewa ikiwa na joto la zaidi ya nyuzi joto 82.
Watafiti wanadokeza kuwa takriban kisa kimoja au viwili kati ya kila visa 10 vya saratani ya umio vinaweza kuepukika iwapo watu wataacha kunywa vinywaji vya moto sana.
Saratani ya umio ni nadra, lakini inaathiri maelfu ya watu kwa mwaka. Nchini Uingereza, takriban asilimia 1 ya watu wako katika hatari ya kupatikana kuwa na aina hii ya saratani.
Nchi hiyo ina idadi ya watu wanaofikia milioni 70.5 na asilimia moja ni watu zaidi ya 700,000. Pia kuna sababu nyingine, kama vile uvutaji sigara, ambazo huleta hatari kubwa zaidi ya kupata saratani ya umio.
Fiona Osgun kutoka shirika la kutafiti saratani anasema shirika lake lililofadhili utafiti huo, limebaini kuwa njia muhimu zaidi za kupunguza hatari ya aina hii ya saratani ni kutovuta sigara na kupunguza unywaji wa pombe na kuepuka vinywaji vya moto sana.
Dalili za saratani ya umio zinaweza kujumuisha kiungulia, tatizo la usagaji wa chakula au maumivu ya koo au kifua, pamoja na kupungua kwa uzito.
- saratani
- muhimbili
- afya
- kansa