Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Habari

Pambazuko laripoti, Samia akerwa uchafu Dar

MIEZI michache baada ya gazeti hili kuandika habari za uchunguzi kuhusu uchafu na ubovu wa mifereji ya majitaka inavyohatarisha afya za watu, hatimaye Rais Samia Suluhu Hassan ameonyesha kukerwa na hali hiyo katika Jiji la Dar es Salaam.

Jumatatu, 7 Septemba 2026 · 06:00Dakika 2 kusomaToleo 181, uk. 14

Mbali na Rais Samia, Spika wa Bunge, Mussa Zungu, naye alizungumzia suala hilo la uchafu katika jiji hilo kubwa la kibiashara nchini, akiwaonya watendaji wa Tamisemi kwa mwenendo usioridhisha unaoshindwa kuwabana watu kutunza usafi wa mazingira.

Onyo la Rais Samia.

Akizungumza wiki iliyopita wakati akiwaapisha viongozi wateule Ikulu Ndogo ya Tunguu, Zanzibar, Rais Samia alilizungumzia suala hilo licha ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, kutokuwepo kwenye hafla hiyo.

Katika suala hilo, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa kusafisha mitaro na kuondoa taka zinazozuia mtiririko wa maji.

Mkuu huyo wa nchi, akaelezea namna baadhi ya mitaro ilivyojaa uchafu huku ikizibwa na marundo ya viroba vya taka ngumu, hali inayosababisha kuziba na kuzuia maji kupita.

Alitoa kauli hiyo wakati akisisitiza umuhimu wa mamlaka mbalimbali kufanya maandalizi ya kukabiliana na madhara ya mvua kubwa za el nino zinazotabiriwa kuanza kunyesha mwishoni mwa mwezi huu katika mikoa kadhaa nchini.

Watalaamu wameshaeleza kuwa mvua hizo zinaweza kusababisha mafuriko katika maeneo kadhaa nchini hivyo serikali imezitaka mamlaka katika ngazi mbalimbali kuhakikisha maandalizi yanafanyika kukabiliana na madhara ya hali hiyo.

Katika hotuba yake, Rais Samia alisema wananchi pia wana mchango katika tatizo hilo kwa kutupa taka kwenye mitaro, hivyo amewataka kubadili tabia na kushirikiana katika kuweka mazingira safi.

Rais Samia pia alieleza kusikitishwa kwake na hali ya usafi katika baadhi ya miji nchini, hususan Dar es Salaam, akisema haipendezi kuona taka zikiwa mitaani.

Makala ya Pambazuko.

Makala ya uchunguzi kuhusu uchafu wa mazingira, ilichapwa na gazeti hili Machi 23, 2026, ambayo ilijikita zaidi katika eneo la Mwenge, Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Gazeti hili katika uchunguzi wake wa takribani miezi mitatu iliwahoji wananchi wa eneo hilo la Mwenge, ambapo walieleza wasiwasi wao wa kukumbwa na magonjwa ya kuambukizwa kutokana na ubovu mkubwa wa mfumo wa maji taka.

Mrundikano wa taka katika mitaro unasababisha mifumo ya majitaka kupasuka mara kwa mara na kusababisha athari kubwa kiafya na katika mazingira.

Gazeti hili pia ilichunguza na kubaini kuwa miundombinu ya maji taka katika eneo la Mwenge ilijengwa zaidi ya miaka 50 iliyopita na bado haijawahi kufanyiwa ukarabati mkubwa, kupanuliwa au kuwekewa mifumo mipya.

Gazeti hili pia ilibaini kuwa tatizo hilo la kupasuka mara kwa mara kwa mashimo ya maji taka, linatokana na miundombinu kuzidiwa kutokana na idadi ya watu kuongezeka.

Makala hiyo ni moja ya makala bora zilizoteuliwa kwa ajili ya Tuzo za Samia Kalamu Awards na sasa iko kwenye hatua ya kupigiwa kura kupitia kiunganishi hiki; https://samiaawards.tz/mshiriki/260251.

  • Usafi
  • Dar es Salaam
  • Samia Suluhu Hassan
  • Afya

Soma Pia