Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Habari

Serikali yachunguza CT-Scan Aga Khan

SERIKALI kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), imeanza uchunguzi wa tukio la kulipuka kwa mashine ya kitabibu inayotumia miale ya Xray na teknolojia ya kompyuta kupiga picha ndani ya mwili wa binadamu (CT-Scan), kwenye Hospitali ya Aga Khan ya mjini Dar es Salaam.

Jumatatu, 24 Agosti 2026 · 06:00Dakika 2 kusomaToleo 179, uk. 15
CT-Scan Aga Khan
CT-Scan Aga Khan — Picha Kutoka Maktaba

Hatua hiyo inakuja wiki moja tu baada ya gazeti hili kufichua kadhia hiyo wiki iliyopita kwa CT-Scan kulipuka ikiwa na mgonjwa akifanyiwa uchunguzi.

Kufuatia tukio hilo, mgonjwa aliandika barua ya madai kupitia wanasheria wake, akitaka kulipwa fidia ya Shilingi milioni 350 na hospitali hiyo kubwa nchini kutokana na kudai kusababishiwa tatizo la kupumua ambalo hakuwa nalo awali.

Barua hiyo ambayo Pambazuko imeiona, ikiwa na kumbukumbu AVL/BR/2026/07/14/01, ya Julai 14, 2026, inadai kuwa fedha hizo ni fidia ya jumla kwa maumivu, mateso, msongo wa mawazo, matatizo ya kisaikolojia, mshtuko, usumbufu na hasara alizozipata kutokana na uzembe wakati akifanyiwa kipimo cha CT- Scan.

Aidha, hospitali hiyo imetakiwa kutoa dhamana ya maandishi ya kukubali kuwajibika na kugharamia gharama zote za matibabu ya sasa na yajayo, madeni na matatizo ya kiafya yatakayothibitika kuwa yametokana moja kwa moja na tukio hilo.

Taarifa zilizolifikia gazeti hili zinabainisha kuwa baada ya kuchapishwa kwa habari hiyo, maofisa wa TMDA walifuatilia suala hilo, lakini uongozi wa hospitali uliwahakikishia kuwa mashine yao ya CT-Scan na vifaa tiba vingine viko imara na havina tatizo lolote.

Meneja wa Ufuatiliaji Usalama wa Vifaa Tiba na Vitendanishi wa TMDA, David Matle, amelithibitishia gazeti hili kuwa mamlaka hiyo inalifuatilia suala hilo ili kujua ubora wa kifaa hicho.

TMDA ndio taasisi yenye mamlaka ya kudhibiti ubora wa vifaa tiba nchini.

Tukio la mashine hiyo kulipuka ikiwa na mgonjwa ndani lilitokea Juni 4, mwaka huu hospitalini hapo wakati mgonjwa ambaye ni mwanafunzi wa chuo cha teknolojia Dar es Salaam (DIT), akifanyiwa uchunguzi.

Taarifa zinaeleza kuwa, kijana huyo mwenye umri wa miaka 20, alifikishwa hospitalini hapo Juni 3, mwaka huu akikabiliwa na maumivu makali ya mwili, hivyo madaktari kuamua kumfanyia uchunguzi kwa kipimo cha ST-Scan.

Hadi leo wakati Pambazuko inachapisha habari hii, zimebaki siku tatu kumalizika muda ambao wanasheria hao wameipa Hospitali ya Aga Khan, kulipa madai ya mteja wao.

Wanasheria hao pia wanaitaka hospitali hiyo kutoa dhamana ya maandishi ya kukubali kuwajibika na kugharamia gharama zote za matibabu ya sasa na yajayo, madeni na matatizo ya kiafya yatakayothibitika kuwa yametokana moja kwa moja na tukio hilo.

Wanasheria hao wameonya kuwa endapo Hospitali ya Aga Khan itashindwa, itapuuza au kukataa kutekeleza madai hayo ndani ya muda uliowekwa, watachukua hatua za kisheria bila kutoa taarifa nyingine kwao.

  • Afya
  • TMDA
  • Aga Khan

Soma Pia