Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Habari Kuu

Hospitali ya Aga Khan matatani

HOSPITALI ya Aga Khan ya jijini Dar es Salaam, imeingia matatani baada ya mashine yake ya uchunguzi wa kitabibu inayotumia miale ya X-ray na teknolojia ya kompyuta kutengeneza picha za ndani ya mwili wa binadamu (CT-Scan), kulipuka huku ikiwa na mgonjwa.

Jumatatu, 17 Agosti 2026 · 06:15Dakika 6 kusomaToleo 178, uk. 6, 7 & 8

Taarifa za uhakika zilizolifikia Pambazuko, zimeeleza kuwa tukio hilo lilitokea Juni 4, 2026 hospitalini hapo wakati mgonjwa ambaye ni mwanafunzi wa Chuo cha Teknolojia cha Dar es Salaam (DIT), (jina tunalo), akiwa ndani ya mashine hiyo akipimwa tumbo.

Taarifa zinaeleza kuwa kijana huyo mwenye umri wa miaka 20, alifikishwa hospitalini hapo Juni 3, 2026 akikabiliwa na maumivu makali ya kichwa na tumbo yaliyoambatana na homa kali.

Baada ya uchunguzi, madaktari waliona umuhimu wa kupata uhakika wa ugonjwa unaomsumbua na ndipo wakaamua kumfanyia kipimo cha CT-Scan.

Baba mzazi wa kijana huyo, Godwin Rwakatare, amethibitisha kutokea kwa tukio Baba mzazi wa kijana huyo, Godwin Rwakatare, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema limemsababishia mwanaye tatizo la kupumua ambalo hakuwahi kuwa nalo awali.

Rwakatare amesema kutokana na kadhia hiyo ya kiafya, kijana wake ametoa jukumu la kufuatilia suala hilo kisheria na kutaka kulipwa fidia kwa kadhia hiyo iliyoteteresha afya ya kijana wake.

Mawakili kwa niaba ya mteja wao, wameandika barua kwa Hospitali ya Aga Khan kuhusu matakwa ya kisheria kulipwa fidia ya Shilingi milioni 350.

Pambazuko limeona nakala ya barua yenye Kumbukumbu Na.: AVL/BR/2026/07/14/01ya Julai 14, 2026 kutoka mawakili iliyosainiwa na wakili Makubi Kunju Makubi, ikielezea namna tukio lilivyotokea na hadi kufikia kutaka kulipwa fidia kwa mteja wao.

Barua hiyo ya mawakili inaeleza kuwa mteja wao – kutokana na kadhia hiyo, amepata maumivu ya mwili, mateso, msongo wa mawazo, matatizo ya kisaikolojia, mshtuko, usumbufu na hasara alizozipata kutokana na kile mawakili wanachoeleza kuwa ni hospitali kushindwa kutimiza wajibu wake wakati mteja wao akifanyiwa kipimo cha CT-Scan.

Barua hiyo ya wanasheria imeipa Hospitali ya Aga Khan siku 14 tangu siku ya kupokea barua hiyo kutekeleza madai yao, ikiwa ni pamoja na kuomba msamaha wa maandishi usio na utata kwa mteja wao kutokana na tukio hilo na mateso aliyoyapata.

Aidha, hospitali hiyo imetakiwa kutoa dhamana ya maandishi ya kukubali kuwajibika na kugharamia gharama zote za matibabu ya sasa na yajayo, madeni na matatizo ya kiafya yatakayothibitika kuwa yametokana moja kwa moja na tukio hilo.

“Mteja wetu alikuwa akipatiwa matibabu katika hospitali hiyo tarehe 4 Juni 2026 na kwamba alifika hospitalini hapo baada ya kusumbuliwa na maumivu ya kichwa ya muda mrefu pamoja na maumivu ya tumbo…”

“Tunaamini tukio hilo lilitokana na ukiukaji wa wajibu wa uangalizi wa hospitali kwa mgonjwa, kwani hospitali ina wajibu wa kisheria na kitaaluma kuhakikisha vifaa vyote vinavyotumika kwa wagonjwa vinatunzwa ipasavyo, vinapimwa mara kwa mara, ni salama na vinafaa kwa matumizi yaliyokusudiwa,” inasema sehemu ya barua hiyo.

Barua hiyo inaendelea; “Pia hospitali ina wajibu wa kuhakikisha wataalamu wenye uwezo wanapatikana ili kutoa msaada wa haraka endapo dharura itatokea.”

Wanasheria hao wameonya kuwa endapo hospitali hiyo itashindwa, itapuuza au kukataa kutekeleza madai hayo ndani ya muda uliowekwa, watachukua hatua za kisheria bila kutoa taarifa nyingine kwao.

Wamesema hatua hizo zitahusisha kufungua shauri la kudai fidia pamoja na gharama za kesi, riba na nafuu nyingine zote zinazopatikana kisheria.

Danadana za Aga Khan

Gazeti la Pambazuko limeutafuta uongozi wa hospitali hiyo kwa zaidi ya miezi miwili ili uweze kuzungumzia suala hilo, lakini liliishia kupigwa danadana.

Jumamosi Juni 6, 2026, Pambazuko lilifika Hospitali ya Aga Khan kupata ufafanuzi wa suala hilo na mmoja wa maofisa wa hospitali hiyo aliyejitambulisha kuwa ni meneja uendeshaji, alisema taasisi hiyo kamwe haiwezi kuzungumza suala hilo kwa sababu linahusu zaidi taarifa za mgonjwa.

Ofisa huyo ambaye alijitambusha kwa jina moja la Kennedy, alisema maadili ya kitabibu hayaruhusu wao kutoa taarifa yoyote kuhusu tukio lolote la mgonjwa, ikitokea hivyo basi muhusika (mgonjwa) au ndugu zake wawe wametoa idhini hiyo, vinginevyo wao hawana ruhusa hiyo.

Ofisa huyo aliwaelekeza waandishi wa habari kwa kuwapatia simu ya ofisa mwingine wa kitengo cha biashara.

Naye alipotafutwa alisema kwamba mtu pekee anayeweza kuisemea taasisi ni mtendaji mkuu ambaye wakati huo alikuwa kwenye vikao Arusha.

Hata hivyo, aliahidi kumtafuta mtendaji na kumweleza suala hilo na angerudisha majibu kwa Pambazuko siku tatu baadaye, lakini hakufanya hivyo.

Alipotafutwa baada ya siku hizo tatu, alimshauri mwandishi kwenda moja kwa moja ofisini kwa mtendaji mkuu kuweka miadi ya kuonana naye moja kwa moja.

Pambazuko lilichukua jukumu la kuandika maswali na kuyapeleka kwa mkono ofisini kwa mtendaji mkuu wa hospitali na kuyakabidhi kwa msaidizi wake aliyejitambulisha kwa jina la Orakya Danda.

Msaidizi huyo aliahidi kufikisha ujumbe huo na akawaomba waandishi wetu kutuma maswali hayo pia kwa njia ya barua pepe ambako pia alisema majibu yangetumwa huko, jambo ambalo halikufanyika hadi leo wakati habari hii inachapishwa.

Baba azungumza

Akisimulia kisa kizima cha tukio hilo, Rwakatare anasema Juni 3, 2026 alipigiwa simu na marafiki wa mwanaye wakimjulisha kwamba hali ya kijana wake, siyo nzuri, ndipo alipokwenda kumchukua chuoni na kumpeleka Hospitali ya Aga Khan.

“Walimlaza, baada ya vipimo daktari akasema ana malaria kali, kesho yake, yaani Juni 4, 2026 tuliambiwa anapaswa kupimwa tumbo kwa mashine ya Utra sound, mgonjwa alifanyiwa maandalizi ikiwa ni pamoja na kutakiwa kunywa maji mengi…”

“Hata hivyo, nilishangaa wakati wanampeleka kwenye Utra sound walibadili mwelekeo wakaenda kwenye mashine ya CT-Scan; sikuhoji zaidi, nilijipa moyo kwamba ndivyo madaktari walivyoona inafaa…”

“Muda mfupi baada ya kipimo kuanza, mashine hiyo ilipata hitilafu ghafla na kuanza kutoa moshi mwingi wakati mtoto wangu akiwa bado ndani ya mashine, alianza kukohoa mfululizo, na asingeweza kujiokoa kwa sababu alikuwa amefungwa, hivyo kusababisha kuvuta na kumeza moshi uliosababishwa na hitilafu hiyo…”

“Waliokuwa wakimhudumia walikimbia na kumwacha ndani ya mashine, nilipiga kelele, mtoeni mwanangu anakufa... ilichukua wastani wa dakika sita kabla ya msaada kufika na kukimbizwa kitengo cha dharura na alizinduka baadaye kabla ya kupelekwa wodini,” amesema.

Akiendelea kusimulia Rwakatare anasema mwanaye aliendelea kukohoa na baada ya siku moja waliruhusiwa kutoka wodini na kupangiwa siku ya kurudi tena hospitalini hapo.

Anasema kabla kuondoka alimfuata mtendaji mkuu wa hospitali hiyo na kumwuuliza kinachoendelea baada ya tukio hilo hatari kwa mwanaye. “Katika hali ambayo sikuitarajia, mkuu huyo alinijibu tu kwamba mtoto wangu amepata mshtuko tu na haoni tatizo lolote. Sikukubalina na uamuzi huo, nilimweleza suala hilo nitalifikisha kwenye vyombo vya habari na kwenye haki za kisheria,” anasema Rwakatare.

Mgonjwa atibiwa kwingine

Juni 11, 2026, baba wa mtoto alialikwa hospitalini hapo kwa ajili ya majadiliano kuhusu tukio hilo na uwezekano wa kulimaliza kwa njia ya mazungumzo.

Anasema katika kikao hicho ambacho pia kilihusisha wanasheria wake, hawakufikia muafaka wowote.

Hata hivyo, anasema badala ya uongozi wa hospitali kukubali kuwajibika kwa madhara yaliyotokana na tukio hilo, walipendekeza kumtibu mgonjwa kwa masharti kwamba gharama za matibabu zilipwe na mgonjwa mwenyewe.

Kutokana na hali hiyo, Rwakatare alilazimika kutafuta ushauri, vipimo na matibabu katika hospitali zingine kwa gharama zake binafsi.

Alizitaja hospitali hizo kuwa ni Amana, Apolo, Besta na Furaha zote za Dar es Salaam na kote huko wamebaini mtoto wake, amepata tatizo la kupumua kutokana na moshi.

Ripoti ya CT-Scan yazua maswali

Wanasheria hao pia wameibua maswali kuhusu ripoti ya CT Scan iliyotolewa na hospitali hiyo ya Aga Khan baada ya tukio hilo.

Kwa mujibu wa barua hiyo, licha ya mashine kupata hitilafu na kipimo kukatizwa, hospitali ilitoa ripoti iliyosema kuwa uchunguzi ulikuwa umekamilika na kwamba hakukuwa na tatizo lililoonekana katika eneo la tumbo.

Wanasheria hao wamesema hali hiyo inazua wasiwasi kuhusu usahihi, uaminifu na uadilifu wa ripoti hiyo ya kitabibu.

Mmoja wa wanasheria ambaye hakutaka jina lake litajwe alikiri kampuni yao kuwapelekea barua ya madai Hospitali ya Aga Khan, ambapo amesema wanamwakilisha mteja wao ambaye anaona hospitali hiyo haikutimiza majukumu yake kwa mujibu wa taaluma husika.

  • Aga Khan
  • Afya
  • CT-Scan
  • Fidia

Soma Pia