Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Tafakuri ya Bagonza

Huu ndiyo uanaharakati sasa

NAANDIKA ili kuutetea uanaharakati. Nafanya hivi kwa sababu nimeona pande mbili zinazovutana zinaweza kusababisha tupoteze kitu muhimu sana.

Jumatatu, 17 Agosti 2026 · 08:15Dakika 2 kusomaToleo 178, uk. 10

Serikali yetu inawaona wanaharakati kama magaidi, lakini inatumia ugaidi kupambana na wanaharakati. Ugaidi ni mbaya bila kujali anautumia nani.

Kwa ufupi niseme, taifa letu bado linahitaji uanaharakati katika mihimili yote mitatu. Wananchi wengi ni maskini, mifumo yetu ni kandamizi, utawala wa sheria ni dhaifu; wenye elimu na nafasi wanawatumia wananchi kama vitega uchumi vyao.

Wenye fedha wa ndani na mabeberu, wanatumia wasomi na watawala kuwaumiza wananchi walio wengi. Bado tunashabikia viongozi wenye nguvu kuliko taasisi imara.

Kwa hiyo tunahitaji kuwa na mahakama ambazo zina majaji na mahakimu walio tayari kumsaidia mtu hata kama mwanasheria wao hajaomba.

Mfano, akimwona mahabusu ana majeraha amuulize kwa nini? Akiona haki yake inapotea kwa kukosea herufi, aagize irekebishwe. Akigundua mtuhumiwa amekaa polisi muda mrefu kinyume cha sheria amwachie.

Hiyo inaitwa kwa Kiingereza – Judicial Activism, yaani uanaharakati wa kimahakama.

Huduma ya mahakama iwe kama hospitali. Ifanye kazi saa 24 kwa mahakimu na majaji kuingia kwa zamu.

Kwa hiyo tunahitaji bunge ambapo spika anayewaona wabunge wote ni sawa bila kujali vyama vyao. Awe jasiri asiyetishwa na chama atokacho. Mwenye upendo wa pekee kwa wabunge wanaohoji hata mamlaka ya spika kwa kutumia kanuni na katiba.

Tunahitaji spika awatie moyo wabunge kuandaa hoja binafsi na kutowapendelea wala kuwaonea mawaziri. Katiba iwe dira yake kuliko kanuni na maelekezo ya chama chake. Hiyo inaitwa Parliamentary Activism.

Na zaidi sana tunahitaji rais anayeagana na chama chake akiisha kuapishwa na kugeuka kuwa rais wa watu wote.

Tunamtaka rais “mjeuri” wa kukataa umangimeza wa kidola na itifaki zinazomtenga na hali halisi ya watu. Aliye tayari “kuasi” taratibu alizowekewa ili awahudumie watu. Anayeheshimu katiba na kutosuluhishwa na wala rushwa, wavunjaji wa haki za binadamu na awe rafiki wa wazalendo.

Tunamtaka kiongozi wa nchi anayeamini utakatifu wa Ikulu hautokani na usafi wake binafsi bali na imani yake kimatendo kwamba serikali ni mali ya wananchi.

Lazima ashtuke wananchi wasipohoji, akerwe wasipotendewa haki. Rais ambaye hata maadui zake watajiona salama mikononi mwake. Hiyo inaitwa Executive or State Activism.

Ieleweke kuwa bila uanaharakati mambo yatakuwa ni “biashara kama kawaida – kila siku, kila wakati.”

Harakati za kweli zitawakatisha tamaa matapeli na watu wasio waadilifu kukimbilia siasa.

Mwandishi wa safu hii ni Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe. Ni mchangiaji maalum wa safu na makala ndani ya Pambazuko.

  • Uanaharakati
  • Utawala bora
  • Mahakama

Soma Pia