Tafakuri ya Bagonza
Jaji mkuu na mahakama zetu
MHESHIMIWA Jaji Mkuu George Masaju, kwa mara kadhaa ametoa maelekezo mbalimbali kwa watendaji wa mhimili wa mahakama na kwa umma mzima.
Siku chache zilizopita ametoa onyo kwamba “hawataruhusu watu kuidharau mahakama.”
Kwa heshima na unyenyekevu nampongeza kwa jitihada anazofanya, lakini namuomba sana apitie maoni yangu haya.
Wananchi wa kawaida hawawezi kuidharau mahakama kamwe. Watanzania hawa ninaowajua na yeye anawajua, wanaiheshimu na kuiogopa mahakama.
Utitiri wa kesi na subira ya wananchi kusubiri haki inayocheleweshwa, ni ushahidi kuwa wananchi hawaidharau mahakama, bali wanaiheshimu hata bila uwepo wa sababu ya kufanya hivyo.
Tatizo walilo nalo wananchi ni imani ndogo kwa mhimili huo. Imani imeshuka sana na walio wengi ama wanajichukulia sheria mkononi au wanatafuta fedha kununua haki zao. Kutoiamini mahakama ni tofauti na kuidharau.
Mahakama zetu zinadharauliwa na makundi mawili yaani; serikali na watendaji wa mahakama. Serikali inaidharau mahakama ama kwa kuiingilia, kudharau uamuzi wake na kutolipa maslahi stahiki, na raslimali na nyenzo za kufanyia kazi.
Watendaji (majaji, mahakimu na watendakazi wengine) wanaweza ama wanaidharau au kuidharaulisha mahakama. Zaidi wanaweza kuwa wanafanya yote mawili kwa wakati mmoja.
Urasimu, umaskini, ujinga na “kujiona” (indispensability) kwa watumishi wa vyombo vya utoaji haki, ni baadhi ya vikwazo vinavyomomonyoa imani ya wananchi kwa mahakama.
Hapa nashauri Masaju asimame upande wa “wajinga” wanaolipa kodi inayoendesha mahakama badala ya matamshi yanayowalinda wanaowaringia wananchi.
Mara kadhaa Jaji Mkuu Masaju, labda bila kukusudia amelumbana na wana harakati wa haki za binadamu na utawala wa sheria, akielekea kuonyesha ubaya wa uanaharakati.
Nina hakika, heshima na fahari ya mahakama mahali popote, hutokana na mahakama kuchukua msimamo imara wa kiharakati (judicial activism) katika kutetea ukuu wa katiba na sheria. Jaji mkuu wetu asiuonee haya uanaharakati.
Katika mfumo ambamo mihimili ya mahakama na bunge imefanywa dhaifu mbele ya mhimili wa serikali, mahakama inalo jukumu zito la kutetea upekee na uhuru wake bila kujali madhara na gharama zake.
Wanaoitesa na kuibagaza mahakama huko serikalini ni wateja wa baadaye wa mahakama hiyo watakaotamani iwe huru na inayotenda haki.
Bila kulinganishwa na mhimili wowote, mahakama inalo jukumu “lisilo la kuagizwa” katika kulinda utakatifu, uhuru na weledi wa mahakama.
Kiongozi wa jukumu hili ni jaji mkuu. Namuombea Masaju asiwe na udhuru, asichoke, asiogope kuitwa mwana harakati na asione aibu kutetea uhuru wa mahakama ambalo ni kimbilio la wanyonge wengi.
Jaji Masaju ajiepushe kutetea “kutokukosea”
kwa mahakama na ashupalie uhuru wa mahakama na kamwe si uhuru wa mahakimu wala majaji.
Mwandishi wa safu hii ni Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe. Ni mchangiaji maalum wa safu na makala ndani ya Pambazuko.
Umebakiwa na makala 2 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.
- Mahakama
- George Masaju
- Haki