Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Habari

JKT wapya ‘kujinoa’ kwa usafi Dar

Baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kueleza kuchukizwa na uchafu wa majiji, sasa wakuu wa mikoa wameanza kuhaha; wa Dar es Salaam, Albert Chalamila kaamua kutumia wahitimu wa JKT kupambana na wachafuzi.

Alhamisi, 17 Septemba 2026 · 12:38Dakika 2 kusomaToleo 182, uk. 14
Wahitimu JKT
Wahitimu JKT — Picha kutoka Maktaba ya Pambazuko

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametangaza kuwatumia vijana waliomaliza mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika kampeni ya kuimarisha usafi mkoani humo.

Akizungumza mwishoni mwa wiki siku chache tu baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuonyesha kukerwa na kukithiri kwa uchafu katika jiji hilo kuu la kibiashara nchini, Chalamila alisema vijana hao watatumika kusimamia na kuwadhibiti watu wanaotuma takataka hovyo.

Chalamila ameeleza hayo wakati akiainisha mikakati ya kushughulikia karipio alilolitoa Rais Samia kuhusu kukithiri kwa uchafu katika Jiji la Dar es Salaam na miji mingine mikubwa nchini.

Kwa upande wake, Chalamila amewaelekeza wakuu wa wilaya wote mkoani mwake kuandaa utaratibu wa kuwatumia vijana hao waliomaliza JKT kufanya shughuli hiyo.

“Nimewaeleza ma-DC kutafuta utaratibu wa haraka ili kuwawezesha vijana hao wawe wadau wakubwa wa usimamiaji wa sheria za utupaji wa taka ovyo,” amesema Chalamila.

Chalamila amesema vijana hao wa JKT watapewa rungu la kukamata watupa taka katika kila kata ya jiji analoliongoza baada ya kukamilika kwa zoezi la upatikanaji wake.

“Utaratibu huo utawekwa vizuri na mkoa na utatangaza vijana watachaguliwa kusimamia zoezi hilo ikiwemo kuwatoza faini wakiukaji wa jambo hilo,”alifafanua.

Pamoja na mambo mengine, mkuu huyo wa mkoa amemtaka kila mwananchi kwenye eneo lake kuhakikisha ana chombo maalumu cha kuhifadhi takataka, lakini pia kila mwenye gari ahakikishe ana chombo cha kutupia takataka ndani ya gari lake.

“Kila mmoja akatae kutupa taka kila mahali kwa sababu mzalishaji mkubwa wa taka ni mwananchi mwenyewe, tukienda kwa elimu hiyo ninaamini tutavuka na kila mmoja ataona fahari kukaa kwenye ardhi yetu ikiwa safi na salama,” amesema Chalamila.

Katika karipio lake alilolitoa Septemba 2, mwaka huu, Rais Samia alieleza kukasirishwa na kukemea vikali hali duni ya usafi katika Jiji la Dar es Salaam na miji mingine mikubwa nchini.

Rais Samia ambaye alieleza hayo wakati wa hafla ya kuwaapisha wakuu wa mikoa na makatibu tawala katika Ikulu Ndogo ya Tunguu, Zanzibar alieleza kutofurahishwa na mwonekano wa Jiji la Dar es Salaam akieleza namna maeneo mbalimbali ya jiji hilo hasa mitaani kulivyo kuchafu hali inayoshusha hadhi ya jiji hilo.

Aligusia pia kuhusu upendeleo wa zabuni za usafi akilaumu mifumo ya baadhi ya halmashauri kutoa zabuni za usafi kwa madiwani kama njia ya ‘kukaa nao vizuri’ wakati madiwani hao hawana uwezo wa kifedha wala vifaa vya kusimamia usafi. Aliagiza zabuni hizo zipewe wakandarasi wenye uwezo mkubwa wa kazi Kutokana na kauli hiyo ya rais, RC Chalamila pamoja na wakuu wa wilaya na madiwani walianza kufanya vikao vya mikakati na kampeni kubwa za usafi wa mazingira kila Jumamosi katika maeneo mbalimbali ya jiji ili kuondoa aibu hiyo.

  • jkt
  • chalamila
  • uchafu
  • samia

Soma Pia