Habari
Jukwaa la wakuu wa mamlaka muhimu kwa uchumi imara
Muhimili mkuu wa uchumi wa nchi nyingi ni taasisi, mashirika na kampuni zinazochochea shughuli za maendeleo, sasa wakuu wake wanakutana kujadili masuala mbalimbali ya kuimarisha ustawi wa Tanzania.

SERIKALI imesema Jukwaa la Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma (C-CEOs Forum) 2026, unaotarajiwa kuwakutanisha viongozi kutoka mashirika zaidi ya 300 ya umma, pamoja na sekta binafsi ni muhimu kuimarisha utendaji.
Jukwaa hilo linaloanza leo - Septemba 28 hadi 30, 2026 - likijumuisha wadau wengine zaidi ya 700, ni muhimu katika kuimarisha utendaji, tija na mchango wa mashirika hayo katika utekelezaji wa Dira 2050.
Jukwaa hilo linaloratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR), ni mwendelezo wa kufanyika ikiwa ni awamu ya nne kufanyika tangu kuanzishwa kwake mwaka 2023.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Ijumaa - Septemba 25, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Gabriel Makalla, alisema kuwakutanisha viongozi wa mashirika ya umma katika jukwaa moja kunatoa fursa ya kujenga uelewa wa pamoja, kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano kwa lengo la kuongeza tija na mchango wa mashirika hayo katika maendeleo ya taifa.
Amesema ni muhimu mashirika ya umma kuhakikisha mipango na shughuli zao zinaendana na malengo ya Dira 2050, ili rasilimali na uwekezaji unaosimamiwa na serikali uweze kuzalisha matokeo yenye thamani zaidi kwa uchumi na wananchi.
Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, alisema utekelezaji wa Dira 2050 unahitaji mabadiliko katika namna mashirika ya umma yanavyotazama utendaji wao, kutoka kwenye kuendesha taasisi na shughuli zake kwenda kwenye kuzalisha matokeo yanayopimika na yenye thamani kwa Taifa.
Mchechu alisema ufanisi wa juu unapaswa kuonekana katika uwezo wa Mashirika kutumia rasilimali na uwekezaji waliokabidhiwa kwa tija, kujenga ushindani, kuimarisha uimara wa kifedha na kutoa huduma zenye ubora, huku yakichangia kikamilifu katika ukuaji wa uchumi.
Mchechu alisema thamani ya uwekezaji wa serikali katika mashirika na kampuni zake imeongezeka kutoka Shilingi trilioni 67.95 mwaka 2020/21 hadi trilioni 92.28 mwaka 2024/25, sawa na ongezeko la asilimia 35.8, hali inayoongeza umuhimu wa kuhakikisha uwekezaji huo unazalisha matokeo makubwa zaidi.
Alisema matokeo hayo hayawezi kupimwa kwa gawio pekee, bali yanapaswa kuangaliwa kwa upana kupitia tija, ubora wa huduma, ufanisi wa matumizi ya rasilimali, uimara wa kifedha, ubunifu, matumizi ya teknolojia, uwezo wa kushindana na athari ya taasisi katika uchumi.
Alisema mashirika ya umma yanapaswa kujenga uwezo wa kubadilika kulingana na mazingira ya uchumi, teknolojia na mahitaji ya wananchi, huku uongozi na bodi zikibeba jukumu muhimu la kuweka mwelekeo wa utendaji na uwajibikaji.
- otr
- kodi
- serikali
- uchumi