Hoja Yangu
Kaulimbiu za Nane Nane zipimwe kwa matokeo
KILA mwaka ifikapo Agosti 8, Watanzania hushuhudia Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima (Nane Nane) yakifunguliwa kwa kaulimbiu mpya inayolenga kuhamasisha maendeleo ya kilimo, mifugo na uvuvi.
Kaulimbiu za miaka tofauti zimehimiza matumizi ya teknolojia, kuongeza uzalishaji, kuongeza thamani ya mazao na kutafuta masoko, lakini swali muhimu ni hili; baada ya maonyesho kuhitimishwa, kaulimbiu hizo huendelea kuishi au hubaki kuwa kumbukumbu za hotuba na mabango?
Kaulimbiu ya mwaka huu inayosisitiza uzalishaji wenye tija na upatikanaji wa masoko ni ujumbe unaopaswa kuwahusu Watanzania wote, siyo wakulima, wafugaji na wavuvi pekee. Katika uchumi wa sasa, kila mtu ni mzalishaji wa bidhaa au huduma.
Fundi seremala anatafuta soko la samani zake, mshonaji anahitaji wateja, mwandishi wa habari anauza maarifa yake, msanii anahitaji soko la kazi zake, na mjasiriamali anahitaji wanunuzi wa bidhaa zake. Hivyo, kaulimbiu hiyo ni mwongozo wa uchumi wa kila siku, si wa wiki ya maonesho pekee.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), sekta ya kilimo inachangia takribani asilimia 26 ya Pato la Taifa na inaajiri zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania. Takwimu hizi zinaonyesha kuwa maendeleo ya sekta hii yana athari kubwa kwa uchumi wa nchi.
Hata hivyo, changamoto ya masoko bado inaendelea kuwakabili wazalishaji wengi. Mara kwa mara tumeshuhudia nyanya, vitunguu, mahindi na mazao mengine yakiharibika mashambani au kuuzwa kwa bei ya hasara kutokana na ukosefu wa masoko ya uhakika.
Hali hii inaonyesha kuwa uzalishaji pekee hautoshi; soko ndilo linalokamilisha thamani ya jasho la mkulima.
Ndiyo maana kuna haja ya kubadili namna tunavyoangalia kaulimbiu za Nane Nane. Badala ya kuziona kama kauli za msimu, zigeuzwe kuwa dira ya utekelezaji inayopimwa kila mwaka.
Serikali inapozindua kaulimbiu mpya, iwe pia inaweka hadharani tathmini ya kaulimbiu iliyopita. Je, malengo yake yalifikiwa kwa kiwango gani? Ni wakulima wangapi walipata masoko mapya? Ni mazao yapi yaliongezwa thamani? Ni ajira ngapi ziliongezeka kutokana na utekelezaji wa kaulimbiu hiyo?
Bila majibu ya maswali hayo, wananchi watabaki kusikia kaulimbiu mpya kila mwaka bila kuona matokeo yake.
Vilevile, kaulimbiu hizi zinapaswa kuwafikia zaidi vijana. Kilimo cha kisasa siyo jembe pekee, kinahitaji ubunifu, matumizi ya teknolojia, uchakataji wa mazao, biashara mtandao na utafutaji wa masoko ya ndani na nje ya nchi. Hapo ndipo kaulimbiu zinapogeuka kuwa fursa za uchumi badala ya maneno ya maadhimisho.
Nane Nane ni zaidi ya maonyesho, ni jukwaa la kutathmini tulikotoka na kupanga tunakokwenda. Kaulimbiu zitakuwa na maana pale zitakapopimwa kwa matokeo halisi, siyo kwa uzuri wa maneno yake.
Maendeleo ya kilimo hayajengwi na kaulimbiu mpya kila Agosti, bali na utekelezaji unaopimika, unaowajibisha na unaomletea mwananchi kipato na maisha bora.
Rashid Mtagaluka ni mwandishi wa habari na anapatikana kwa simu nambari na email; mtagaluka@gmail.com.
- Nane Nane
- Kilimo
- Masoko