Biashara
Kielelezo cha dhamana kuboresha uwazi na uwekezaji
SERIKALI imezindua kielelezo cha viwango vya faida vya dhamana za serikali, hatua inayotarajiwa kuimarisha uwazi wa soko la fedha, kuongeza ufanisi wa maamuzi ya uwekezaji na kuvutia mitaji ya ndani na nje ya nchi.
Kielelezo hicho kilizinduliwa jijini Dar es Salaam wiki iliyopita na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar.
Akizungumza katika hafla hiyo, Tutuba alisema kupitia kielelezo hicho wawekezaji wataweza kuona na kufuatilia mwenendo wa faida halisi katika soko la upili la dhamana za serikali, jambo litakalowasaidia kufanya maamuzi ya uwekezaji kwa kuzingatia taarifa sahihi na zinazoaminika.
‘‘Kielelezo hicho kitawawezesha wawekezaji wa ndani na wa kimataifa kulinganisha viwango vya faida vya dhamana za serikali na fursa nyingine za uwekezaji ndani ya nchi, pamoja na masoko ya kikanda na kimataifa, hivyo kuongeza uwazi wa soko, kuvutia wawekezaji wa kigeni na kuimarisha ushindani wa soko la fedha nchini,”
alisema Tutuba.
Aidha, Tutuba alisema Kielelezo hicho pia kitaakisi matarajio ya soko kuhusu ukuaji wa uchumi, mfumuko wa bei na mwelekeo wa sera ya fedha, hivyo kitakuwa nyenzo muhimu kwa Benki Kuu katika kuimarisha utekelezaji wa sera ya fedha inayotegemea viwango vya riba.
‘‘Soko letu limeshuhudia ukuaji mkubwa katika kipindi cha miaka 25, ambapo mwaka 2001, dhamana za Serikali ambazo zilikuwa hazijaiva zilifikia Shilingi bilioni 499, na kuongezeka mpaka kufikia Shillingi trilioni 32.3 hivi sasa,” alisema Tutuba.
Pia alibainisha kuwa uthaminishaji wa dhamana za Serikali zinazowasilishwa na benki za biashara kama dhamana ya kupata mikopo kutoka Benki Kuu utafanyika kwa kutumia kielelezo hicho, hatua inayotarajiwa kuongeza usahihi na uwazi katika shughuli za kifedha.
Aliwashukuru wadau wote wa soko kwa ushiriki wao ambao umeiwezesha serikali kupata fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo kupitia dhamana za Serikali pamoja na kuanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050.
Alisisitiza kuwa kuna umuhimu wa Benki Kuu na Serikali kwa ujumla kuendelea kutoa elimu ya uwekezaji ili kuhakikisha soko linaendelea kukua kwa kasi na kuongeza idadi ya wawekezaji kutoka 32,631 walioko sasa kwani idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na idadi ya watu nchini.
Awali, akizungumza katika tukio hilo, Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Madeni, Wizara ya Fedha, Japhet Justine, alisema kuwa soko la hisa limeendelea kukua ambapo katika mwaka wa fedha 2025/26, thamani ya miamala iliyofanyika ilikuwa zaidi ya Shilingi trilioni 6.7.
Mkurugenzi Mtendaji wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Peter Nalitolela, alisema kuwa Kielelezo hicho kitaongeza miamala na ukwasi katika soko la dhamana na kuchochea maendeleo ya aina nyingine za mali zinazouzwa katika soko la hisa.
- BoT
- Dhamana
- Uwekezaji
- DSE