Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Uchumi & Biashara

Mradi wa LNG watikisa dunia

HAUJAANZA rasmi lakini mradi wa kuchakata gesi asilia (LNG) ambao umepangwa kujengwa Lindi, Tanzania, unaitikisa dunia.

Jumatatu, 7 Septemba 2026 · 06:00Dakika 2 kusomaToleo 181, uk. 18

Habari zilizochapishwa hivi karibuni zimeuorodhesha mradi huo miongoni mwa miradi mikubwa sana duniani ambayo inaangaliwa na kufuatiliwa kwa karibu zaidi na China, Ulaya na Marekani.

Mradi huo wa kuchakata LNG nchini Tanzania unakadiriwa kugharimu dola za Marekani bilioni 42 (zaidi ya Shilingi trililioni 105).

Miradi mingine mikubwa ni pamoja na mradi wa kusafisha mafuta ghafi wenye thamani ya dola bilioni 17 Nigeria, ikiwa ni uwekezaji wa tajiri namba moja Afrika, Aliko Dangote, na mradi wa bomba la gesi kati ya Nigeria na Morocco wenye thamani ya dola za Marekani bilioni 25. Mwingine ni ujenzi wa kiwanja kipya cha ndege nchini Ethiopia.

Wachambuzi wa masuala ya uchumi na uwekezaji wanaeleza kuwa miradi hiyo italeta mabadiliko makubwa siyo tu Afrika, bali duniani katika nyanja za nishati, usafiri wa anga, michezo na kuiweka Afrika kama mshindani katika ngazi ya dunia.

Moja kati ya mambo makubwa yanayoangaliwa kupitia miradi hii ni uwezo wake wa kugeuza uwekezaji kuwa ajira za kudumu, kuinua uchumi na kupanua biashara za kikanda.

Kwa upande mwingine, wachambuzi wanasubiri kuona iwapo miradi hiyo inaweza kulikomboa bara la Afrika kutoka kwenye matatizo yake sugu ikiwemo ukosefu wa nishati na gharama kubwa za usafiri na usafirishaji kwa kutegemea mafuta yanayoagizwa nje ya bara hilo.

Wachumi wanaamini kuwa iwapo miradi hiyo itatekelezwa kwa weledi, ina uwezo mkubwa wa kuleta mapinduzi katika nyanja nyingi ikiwemo nishati, usafiri wa anga, biashara na mnyororo wa madini.

Akiba ya gesi Tanzania.

Mradi huo unatajwa kwamba utakuwa chanzo cha kuvutia wawekezaji wa kimataifa kutokana na Tanzania kuwa na akiba kubwa ya gesi asilia ambayo tayari imeshagunduliwa.

Siku za hivi karibuni mradi huo umeanza kuwaamsha wawekezaji, hasa baada ya vita vya Marekani na Iran, vinavyosababisha kufungwa kwa lango la Hormuz, ambalo hutumika kupitisha sehemu kubwa ya mafuta yanayotoka nchi za Ghuba. Mradi huo wa LNG unaonekana sasa kuwa kama mbadala wa utegemezi wa mafuta na hivyo kushika macho ya wawekezaji wakubwa duniani katika eneo la nishati.

Usafishaji mafuta.

Tajiri namba moja Afrika, Aliko Dangote yupo katika mchakato wa kujenga kiwanda kikubwa cha kusafisha mafuta ghafi katika eneo la Afrika Mashariki.

Kiwanda hiki kinatarajiwa kuleta mapinduzi katika eneo la nishati kwani kitawezesha nchi za Afrika Mashariki kuipata nishati hiyo kwa uhakika na kwa bei nafuu.

Kiwanda hicho kinachotarajiwa kuwa na uwezo wa kusafisha mapipa 700,000 kwa siku, kimepangwa kujengwa huko Lamu nchini Kenya, kikiwa ni kiwanda kikubwa cha aina hiyo nje ya Nigeria.

Umebakiwa na makala 2 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.

  • LNG
  • Gesi asilia
  • Lindi
  • Uwekezaji

Soma Pia