Hoja Yangu
Kizimkazi: Kutoka siku ya mtaa hadi jukwaa la taifa
KUNA matukio huanza kama wazo dogo la jamii, lakini baadaye hukua na kuwa sehemu ya utambulisho mpana wa taifa. Tamasha la Kizimkazi ni miongoni mwa mifano hiyo.

Kilichoanza mwaka 2015/2016 kama tukio la kuwaaga wananchi wa Kizimkazi baada ya Dk.
Samia Suluhu Hassan kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa urais, baadaye kikajulikana kama Samia Day, kisha Kizimkazi Day, leo ni tamasha linalovuka mipaka ya eneo hilo.
Mwaka 2020 liliingia rasmi katika sura ya tamasha, likipanua maudhui yake kutoka utamaduni kwenda utalii, uwekezaji na maendeleo ya jamii.
Hapo ndipo nguvu kubwa ya Kizimkazi ilipo. Si tena suala la wakazi wa Kizimkazi kujikusanya kwa ajili ya kusherehekea utamaduni wao, bali ni jukwaa linalowakutanisha wananchi kutoka Zanzibar na Tanzania Bara, wafanyabiashara, wawekezaji, taasisi za Serikali, wasanii na wageni kutoka nje ya nchi.
Rais Samia mwenyewe mwaka 2024 alieleza kuwa tamasha hilo limekua kutoka tukio la jamii hadi kuwa la kitaifa na kuelekea kimataifa.
Tamasha la mwaka huu limeendelea kuthibitisha mwelekeo huo. Limeambatana na uzinduzi wa miradi tisa ya maendeleo, ikiwamo kituo cha mafunzo ya ufundi, mradi wa maji, uwanja wa watoto na maboresho ya miundombinu ya jamii.
Hii inaonesha kuwa tamasha linaweza kuwa zaidi ya burudani; linaweza kuwa chombo cha kuunganisha sherehe na maendeleo.
Lakini mafanikio yake makubwa zaidi yanapaswa kupimwa kwa kile kinachobaki baada ya muziki kuzimwa na wageni kuondoka. Je, wafanyabiashara wadogo wanapata soko? Je, vijana wanapata ajira na ujuzi? Je, utalii wa Kusini Unguja unaongezeka? Je, wawekezaji wanaona fursa mpya?
Haya ndiyo maswali muhimu kwa sasa.
Kizimkazi tayari imeonyesha kuwa utamaduni unaweza kuwa mtaji wa uchumi. Maonesho Samia akiwa na mwanamuziki wa Uganda, Jose Chameleon kwenye Tamasha la Kizimkazi.
sho, michezo, muziki, vyakula vya asili, utalii na shughuli za baharini vinaweza kuunganisha historia ya eneo na fursa za kisasa.
Ushiriki wa wageni na wasanii kutoka nchi jirani, ikiwamo Uganda, unaonesha pia uwezo wa Kizimkazi kuwa daraja la mwingiliano wa kitamaduni Afrika Mashariki.
Kwa hiyo, Kizimkazi haipaswi kubaki kuwa tamasha la siku chache. Inapaswa kujengwa kuwa brand ya utalii na utamaduni ya Tanzania, yenye kalenda ya mwaka mzima, kuvutia wawekezaji na kuhakikisha wananchi wa eneo husika ndio wanakuwa wanufaika wakuu.
Kutoka Samia Day hadi Kizimkazi Festival, safari hii imetufundisha jambo moja; wazo dogo la jamii linaweza kuwa jukwaa kubwa la taifa, ikiwa linaendelezwa kwa maono na tija.
Rashid Mtagaluka ni mwandishi wa habari na anapatikana kwa simu nambari na email; mtagaluka@gmail.com.
- Kizimkazi
- Utalii
- Zanzibar