Makala ya Afya
Kudamka kunavyokatiza umakini wa watoto
KUWAHI shule alfajiri ni sehemu ya maisha ya kila siku kwa wanafunzi wengi. Baadhi yao huamka mapema kujiandaa, kutembea umbali mrefu au kutumia usafiri wa umma.
Ingawa wazazi na walimu huona utaratibu huo kuwa njia ya kujenga nidhamu, uwajibikaji na kuheshimu muda, unaibua swali muhimu; Je, ratiba za shule zinazingatia afya na mahitaji ya usingizi ya mtoto?
Baadhi ya wanafunzi wa Mkoa wa Songwe wanasema hushindwa kuzingatia masomo kutokana na uchovu. Huamka saa 11 alfajiri baada ya kuchelewa kulala kwa sababu ya muda mrefu wanaotumia shuleni na majukumu ya nyumbani.
Marry Ayubu Kinyamagoha, mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Tunduma, anasema hutoka shuleni saa 12 jioni. Akifika nyumbani huwasaidia wazazi kuandaa chakula hadi saa nne usiku, kisha huamka saa 11 alfajiri. Ratiba hiyo humpa takribani saa saba tu za usingizi.
Laban Zakaria, mwanafunzi wa shule hiyo, anasema kuamka mapema baada ya kulala usiku humfanya asinzie darasani na kushindwa kufuatilia mafundisho vizuri.
Pia anakabiliwa na hatari ya kukimbizwa na mbwa ambao hawajafungiwa wakati anapoelekea shuleni alfajiri.
Kwa mujibu wa takwimu za Vituo vya Marekani vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa, CDC, watoto wenye miaka sita hadi 12 wanahitaji saa tisa hadi 12 za usingizi kila baada ya saa 24, huku vijana wa miaka 13 hadi 18 wakihitaji saa nane hadi 10.
Kukosa usingizi wa kutosha huhusishwa na matatizo ya umakini, tabia, afya ya akili na ufaulu.
Mapitio ya utafiti yaliyochapishwa mwaka 2016 katika jarida la Sleep Medicine Reviews yalibaini kuwa kuchelewesha muda wa kuanza shule kwa dakika 25 hadi 60 kuliongeza usingizi wa vijana kwa dakika 25 hadi 77 kwa usiku wa siku za masomo.
Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma, Dkt. Abdulazack Haji anasema usingizi wa muda mfupi huathiri uwezo wa kufikiri, umakini, kumbukumbu na utatuzi wa matatizo.
Kwamba unaweza pia kusababisha mabadiliko ya hisia, ikiwamo mtoto kukasirika bila sababu.
“Usingizi wa kutosha ni muhimu kwa ukuaji, afya ya akili, kumbukumbu na uwezo wa kuzingatia.
Mtoto anayeamka mapema lazima apate muda wa kutosha wa kulala,” anasema.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Tunduma, Tutindaga Mwakibete, anasema uchovu huonekana darasani kupitia kusinzia, kupungua kwa umakini na uwezo mdogo wa kukumbuka.
Shuleni kwake hali hiyo hujitokeza zaidi katika masomo ya mchana kutokana na njaa, lakini pia na usingizi kwa kuwa watoto wanachelewa kulala wanapofika nyumbani. Anawashauri wazazi kuacha watoto walale mapema na pia kuchangia chakula shuleni ili kupunguza uchovu.
Wazazi wanashauriwa kupanga muda wa kazi za shule na majukumu ya nyumbani, kupunguza matumizi ya simu, televisheni na michezo ya video kabla ya kulala, na kuweka muda maalumu wa mtoto kupanda kitandani kulala.
Shule nazo zinapaswa kuangalia zaidi ya mahudhurio na kuchelewa. Ushirikiano wa wazazi, walimu, wataalamu wa afya na watunga sera unahitajika kusawazisha nidhamu, safari, chakula na usingizi.
Sasa swali kubwa si kama mtoto amewahi shule pekee, bali kama amelala vya kutosha kujifunza vizuri na kulinda afya yake.
- Afya
- Watoto
- Elimu