Habari
Matumaini matibabu selimundu yapatikana
KILA siku Rahma Abdallah hulazimika kufikiria jambo moja muhimu kabla ya mambo mengine; ‘dawa yake.’ Rahma, ambaye anaishi Chanika, Dar es Salaam, ni mmoja wa watu wanaoishi na ugonjwa wa selimundu (sickle cell) ambao humlazimisha mgonjwa kuishi kwa kutegemea dawa ya ‘hydroxyurea’ kusaidia kudhibiti athari za ugonjwa huo.
Kwa siku analazimika kutumia vidonge viwili vya dawa hiyo, ambapo kila kidonge hununua kwa Shilingi 2,000.
“Ni changamoto sana, hasa unapokuwa huna kazi na unategemea ndugu,” anasema katika mahojiano ya Pambazuko.
Kwa wagonjwa wengi wa selimundu, hydroxyurea siyo dawa ya kawaida tu, inaweza kuwa sehemu muhimu ya maisha yao, hususan kusaidia kupunguza baadhi ya madhara na vipindi vya maumivu makali vinavyoweza kujirudia.
Ndiyo maana taarifa za Senegal kuanza uzalishaji wa dawa hiyo zimepokelewa kwa matumaini mapya miongoni mwa baadhi ya watu wanaoishi na ugonjwa huo na wadau wa afya Afrika.
Dawa hiyo, inayofahamika kwa jina la kitaalamu Drepaf, inayozalishwa nchini Senegal na kampuni ya dawa ya Teranga Pharma, kwa ushirikiano na taasisi ya Drep Afrique. Dawa hiyo ni ainasafu (generic) ya hydroxyurea.
“Senegal kuanza utengenezaji wa dawa za selimundu ni hatua nzuri, kwa sababu bei ya dawa inaweza ikashuka na zinaweza kupatikana kwa wingi,” anasema Rahma.
Matumaini kwa Afrika.
Daktari Collin Kanza kutoka Kituo cha Matibabu ya Selimundu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, anasema hatua iliyofikiwa na Senegal ni mafanikio makubwa kwa mapambano dhidi ya ugonjwa huo barani Afrika.
“Ni hatua kubwa sana. Senegal ina wagonjwa wachache wa selimundu ikilinganishwa na baadhi ya nchi nyingine za Afrika, lakini imeweza kufanya jambo hili kubwa...”
“Sisi Tanzania tuna uhitaji mkubwa zaidi wa dawa hizi. Ni wazi tunalo la kujifunza na kuiga mfano kutoka kwao,” anasema Dkt. Kanza.
Tanzania inashika nafasi ya nne duniani na ya tatu Afrika kwa idadi kubwa ya wagonjwa wa selimundu, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).
Takwimu za Wizara ya Afya zinaeleza kila mwaka kuna watoto 11,000 hadi 14,000 wanaozaliwa na ugonjwa huo nchini Tanzania.
Matibabu ya ugonjwa huu wa kurithi ni ya muda mrefu, hivyo, kupatikana kwa dawa kwa urahisi na kwa gharama nafuu kunaweza kuleta tofauti kubwa katika maisha ya wagonjwa na familia zao.
Hatua ya Senegal pia inafungua mjadala mpana kuhusu uwezo wa Afrika kuwekeza katika uzalishaji wa dawa muhimu zinazohitajika kwa watu wake.
Kwa sasa baadhi ya dawa zinazotumiwa na wagonjwa wa selimundu nchini zinapatikana kupitia uzalishaji na mifumo ya usambazaji kutoka nje ya Afrika, ikiwamo hii ya hydroxyurea.
Iwapo uzalishaji wa hydroxyurea utaongezeka barani Afrika na dawa hiyo kusambazwa katika nchi nyingine, matumaini ya wagonjwa wengi ni kwamba gharama inaweza kushuka na upatikanaji wake kuongezeka.
Bima ya afya.
Wizara ya Afya iliingiza dawa hii katika orodha ya dawa zinazopatikana ndani ya bima ya afya.
Kwa Felister John, mzazi wa shujaa wa selimundu anayeishi Kigoma, kuwa na bima ya afya kwa mtoto wake kumeleta mabadiliko makubwa. Anasema kabla ya bima hiyo familia yake ilipitia changamoto kubwa kwa sababu alilazimika kutoa fedha nyingi kutoka mfukoni kununua dawa na gharamia nyingine za matibabu.
Hata hivyo, kwa familia ambazo hazina uwezo wa kugharamia bima, mzigo wa matibabu ya selimundu unaweza kuwa mkubwa zaidi.
Julieth Mombuli ni miongoni mwa wale wanaopambana kila siku kuhakikisha mtoto wake anapata dawa.
“Mimi ndiye baba na mimi ndiye mama, baba yake alikataa kwamba huyu si mtoto wake, nilimpata kwa mwanaume mwingine nje ya ndoa, jambo ambalo si la kweli...”
“Hivyo, sina jinsi ya kufanya. Naumia, lakini ni mwanangu siwezi kumuacha akiteseka peke yake. Ninafanya biashara ndogondogo, kuna wakati nalazimika kujinyima ili angalau mwanangu apate dawa,” anasimulia kwa uchungu.
Anasema mwanawe anapotumia dawa ya hydroxyurea hupata nafuu kubwa, humsaidia kupunguza vipindi vya maumivu makali vinavyojirudia mara kwa mara.
Kwa Julieth, kutafuta fedha za dawa ni sehemu ya mapambano ya kila siku ya kumlea mtoto anayeishi na selimundu.
Mahitaji ni makubwa.
Veronica Mrema, Ofisa Habari wa Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Selimundu Tanzania (SCDPCT), anasema jumuiya hiyo imekuwa ikisaidia baadhi ya watoto wanaoishi na ugonjwa huo kupata bima ya afya.
“Mahitaji bado ni makubwa. Ila tangu Januari mwaka huu hadi sasa, tumeweza kuwakatia bima ya afya watoto 36 tu kwa kushirikiana na mdau mmoja aliyetuunga mkono.
“Orodha tuliyonayo bado tuna wengine wengi ambao hatujaweza kuwafikia kwa sababu uhitaji ni mkubwa, tuna wagonjwa zaidi ya 300 na asilimia kubwa ni wahitaji,” anasema.
Anasema kwa muktadha huo, hatua ya Senegal kuanza uzalishaji wa hydroxyurea ni hatua inayostahili pongezi kubwa na ina maana kubwa katika mapambano dhidi ya selimundu.
“Kwa hatua ambayo Senegal imeweza kufikia, imetuletea faraja kubwa. Ni hatua kubwa, na mashujaa, wazazi na walezi wameipokea kwa furaha kubwa,” anasema.
Bei itashuka?
Watu wanaoishi na selimundu nchini wana matumaini kwamba iwapo Senegal itafikia uwezo wa kuzalisha dawa kwa kiwango cha kutosheleza na kuisambaza katika nchi nyingine za Afrika, ikiwamo Tanzania, gharama za ununuzi zinaweza kupungua kwa kiasi kikubwa.
Kwa Rahma, ambaye kwa sasa hununua vidonge viwili kwa siku, matumaini hayo yana maana kubwa.
Umebakiwa na makala 2 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.
- Selimundu
- Afya
- Senegal
- Dawa