Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Hoja Yangu

Kwa nini tunapenda uzinduzi kuliko matokeo?

CAG, Dkt. Charles Kichere KUNA jambo moja ambalo Tanzania tunapaswa kuanza kulitafakari upya. Kwa nini tunafurahia sana kuzindua miradi, lakini wakati mwingine tunasahau kuuliza matokeo yake?

Jumatatu, 14 Septemba 2026 · 06:00Dakika 2 kusomaToleo 182, uk. 27

Kuweka jiwe la msingi, kukata utepe, kupiga picha na kutoa hotuba ni sehemu ya kawaida ya utekelezaji wa miradi, lakini maendeleo ya kweli hayapimwi kwa ukubwa wa sherehe ya uzinduzi.

Yanapimwa kwa namna mradi unavyobadili maisha ya wananchi.

Hili siyo suala la hisia. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa fedha 2024/25 imeonyesha changamoto kubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Kwa mfano, miradi 47 yenye thamani ya Shilingi bilioni 105.56 katika mamlaka za serikali za mitaa ilichelewa zaidi ya muda wa mikataba au ilisimama kwa zaidi ya siku 90. Huku miradi 671 yenye thamani ya Shilingi bilioni 79.17 katika halmashauri 47 ilikuwa haijakamilika.

Hii ndiyo sehemu ambayo mjadala wetu unapaswa kuanzia. Mradi wa shule unaweza kuzinduliwa kwa mbwembwe, lakini kama madarasa hayatoshi, maabara haifanyi kazi au wanafunzi hawapati mazingira bora ya kujifunzia, tunapaswa kujiuliza kama tumefikia lengo.

Au hospitali inaweza kuzinduliwa, lakini kama haina vifaa, haina watumishi au haina dawa za kutosha, jengo pekee haliwezi kuitwa mafanikio kamili. Hii ndiyo Hoja Yangu.

Vivyo hivyo, barabara inaweza kukamilishwa na kuzinduliwa, lakini kama baada ya muda mfupi inaanza kuharibika kwa sababu ya ubora duni wa ujenzi, swali halipaswi kuwa nani alizindua, bali kwa nini fedha za wananchi hazijaleta thamani iliyokusudiwa? Hii ndiyo Hoja Yangu.

Hata katika miradi mikubwa, changamoto hii ipo. CAG alibaini, kwa mfano, madai ya wakandarasi yaliyocheleweshwa kulipwa katika miradi mbalimbali, yakiwamo Sh14.05 bilioni katika Dodoma City Outer Dual Carriageway Ring Road na Shilingi bilioni 11.75 katika mradi wa maji.

Tatizo si kuwa na miradi mingi. Tatizo ni kuhakikisha kila shilingi iliyowekezwa inazalisha thamani inayokusudiwa. Hii ndiyo Hoja Yangu.

Hapa ndipo tunapohitaji kubadili pia utamaduni wetu wa kushangilia mafanikio. Wananchi wanapaswa kupewa taarifa si tu wakati mradi unapozinduliwa, bali pia kuhusu gharama yake, muda uliopangwa kukamilika, changamoto zilizojitokeza na faida ambayo wananchi wanatarajiwa kupata. Hii ndiyo Hoja Yangu.

Tunapaswa kubadilisha namna tunavyopima mafanikio. Badala ya kuuliza, “Umezindua miradi mingapi?”, tuulize, “Miradi hiyo imekamilika mingapi? Inafanya kazi? Wananchi wananufaika kwa kiasi gani?” Hii ndiyo Hoja Yangu.

Hapo ndipo uwajibikaji unapokuwa na maana. Serikali, viongozi na taasisi zetu wanastahili pongezi kwa miradi inayotekelezwa, lakini pongezi hizo hazipaswi kuwa mwisho wa safari.

Uzinduzi ni mwanzo; matokeo ndiyo ushindi.

Tanzania inahitaji utamaduni mpya wa maendeleo, utamaduni unaopima si ukubwa wa jukwaa la uzinduzi, bali ukubwa wa mabadiliko yanayobaki baada ya wageni kuondoka.

Kwa sababu hatimaye, mwananchi hahitaji picha ya kiongozi akikata utepe. Anahitaji kuona maisha yake yamebadilika. Hii ndiyo Hoja Yangu.

Rashid Mtagaluka ni mwandishi wa habari.

  • Uongozi
  • Uwajibikaji
  • Maendeleo

Soma Pia