Hoja Yangu
Wapangaji wanapobadilishana, nyumba haipaswi kubomoka
MABADILIKO ya viongozi katika nchi yoyote ni jambo la kawaida. Leo mtu anaweza kuwa madarakani, kesho asiwepo. Leo anaweza kushika nafasi kubwa, kesho nafasi hiyo ikawa mikononi mwa mwingine. Huo ndio uzuri na wakati mwingine ugumu wa uongozi wa kisiasa.
Lakini swali muhimu si nani ameondoka au nani ameingia. Swali ni je, taasisi inabaki imara baada ya mtu (kiongozi) kuondoka?
Tukio la kujiuzulu kwa aliyekuwa Makamu wa Rais, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, na baadaye kupatikana kwa Deogratius Ndejembi kushika nafasi hiyo, limetukumbusha jambo moja kubwa kuhusu uongozi wetu.
Jambo lenyewe ni kwamba, kumbe nchi haiwezi kujengwa kwa kutegemea mtu mmoja. Na kiongozi mzuri si yule anayefanya taasisi ionekane imara kwa sababu yupo, bali yule anayesaidia kujenga mfumo ambao utaendelea kuwa imara hata yeye akiwa hayupo.
Hapa ndipo tunapaswa kujiuliza kama Tanzania tunajenga taasisi zinazowatumikia viongozi, au viongozi wanaotumikia taasisi? Na ndipo Hoja Yangu wiki hii ilipojikita. Kwamba, tunahitaji viongozi wanaoondoka na kuiacha taasisi na uimara wake.
Mabadiliko ya uongozi yasitafsiriwe kila mara kama tetemeko la kisiasa. Kama mifumo yetu ni imara, kuondoka kwa kiongozi mmoja hakupaswi kusababisha hofu kwamba mambo yote yatabadilika. Hapana!
Viongozi wanakuja na kuondoka, lakini Katiba, serikali, bunge, mahakama na taasisi nyingine za umma vinapaswa kubaki.
Jambo lingine muhimu ni kuhakikisha kuwa mabadiliko ya viongozi hayaathiri mwendelezo wa sera na mipango ya maendeleo. Wananchi hawapaswi kuanza upya kila mara kiongozi anapobadilika. Serikali si mradi wa mtu binafsi; ni chombo kinachoendelea kuhudumia wananchi, licha ya mabadiliko ya wanaokiongoza.
Aidha, viongozi wanapaswa kujenga mazingira ya kuwaachia madaraka kwa heshima.
Kuondoka si kushindwa, na kuingia madarakani si ushindi wa mtu binafsi. Vyote ni sehemu ya mzunguko wa uongozi unaopaswa kuheshimu taasisi na maslahi mapana ya taifa.
Ni muhimu pia kujenga utamaduni ambao kiongozi anaweza kuondoka madarakani bila kuonekana kama ameangusha nchi. Na zaidi, anayechukua nafasi yake asionekane kama ameingia kwenye ofisi iliyokuwa mali ya mtangulizi wake. Ofisi ni ya wananchi, si ya mtu.
Hili ni somo muhimu kwa wanasiasa wetu.
Mamlaka ni dhamana, si urithi. Nafasi ni ya muda, lakini taasisi ni ya kudumu.
Tanzania inahitaji viongozi wanaojua kwamba historia haitawakumbuka kwa muda waliokaa madarakani pekee, bali pia kwa aina ya taasisi walizoacha nyuma yao.
Kwa hiyo, tusitumie mabadiliko ya viongozi kujenga hofu. Tuitumie kama nafasi ya kupima uimara wa mifumo yetu na uwezo wa taifa kuendelea mbele bila kutegemea umaarufu au nguvu ya mtu mmoja.
Kwa sababu mwisho wa yote, viongozi ni wasafiri, taasisi ni nyumba. Wasafiri wanapobadilishana, nyumba haipaswi kubomoka.
Rashid Mtagaluka ni mwandishi wa habari.
Umebakiwa na makala 2 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.
- Uongozi
- Taasisi
- Utumishi wa umma