Hoja Yangu
Tusiipime serikali kwa kelele za mitandaoni
MITANDAO ya kijamii imebadilisha namna wananchi wanavyopokea na kutafsiri taarifa za serikali.

Leo, mtu anaweza kuamka asubuhi na kukutana na hoja nzito inayolenga serikali, taasisi au kiongozi fulani, na ndani ya muda mfupi hoja hiyo ikawa mjadala wa kitaifa. Hapa ndipo ninapoona serikali inahitaji kuwekeza zaidi katika mawasiliano ya umma.
Siyo kwamba, kila kinachoandikwa dhidi ya serikali ni uongo. Vivyo hivyo, siyo kila kinachoandikwa dhidi yake ni kweli.
Tatizo linakuja pale ambapo taarifa inapowekwa hadharani, serikali inachelewa kutoa ufafanuzi, huku wananchi wakiachwa wajijengee uelewa kupitia mitandao ya kijamii.
Mfano mzuri ni hoja mbalimbali zinazojadiliwa sasa kuhusu serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, zikiwamo suala la Tundu Lissu, matukio ya Oktoba 29, Katiba Mpya na madai kwamba serikali imejikita zaidi katika kushughulika na wapinzani kuliko matatizo ya wananchi.
Hoja hizi zinahitaji majibu, lakini si majibu ya hasira. Serikali inapokosolewa, jambo la kwanza siyo kumshambulia mkosoaji. Jambo la kwanza ni kujiuliza: Hoja hii ina ukweli kiasi gani? Tuna data gani? Na wananchi wanahitaji kujua nini?
Hapo ndipo mawasiliano ya serikali yanapokuwa muhimu. Serikali inapokuwa na taarifa sahihi, inapaswa kuzifikisha kwa wananchi kwa lugha rahisi na kwa wakati.
Inapokosewa, isisite kurekebisha taarifa. Inapokosolewa kwa jambo lenye msingi, ieleze hatua inayochukua. Na inapofanya vizuri, ieleze matokeo ya kazi hiyo badala ya kutegemea wananchi watajua wenyewe.
Mawasiliano mazuri siyo kuficha changamoto au kujibu kila mkosoaji. Ni kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu kinachofanywa na serikali, sababu za hatua zinazochukuliwa na matokeo yanayopatikana.
Serikali inapoweka wazi taarifa zake, inapunguza nafasi ya uvumi, upotoshaji na tafsiri zinazoweza kupotosha uhalisia.
Kwa upande mwingine, wananchi nao wanapaswa kujifunza kutenganisha taarifa na propaganda. Si kila ujumbe unaosambaa kwa kasi ni ukweli, na si kila ujumbe unaoikosoa serikali unatokana na chuki.
Vyombo vya habari na waandishi nao wana wajibu wa kuchunguza taarifa, kuthibitisha takwimu na kutoa nafasi kwa pande zinazohusika kabla ya kujenga hitimisho.
Hoja Yangu wiki hii ni kwamba, tusiipime serikali kwa kelele za mitandaoni pekee. Wala tusiipime kwa sifa za wafuasi wake. Badala yake, tuipime kwa kazi inayofanya na namna kazi hiyo inavyobadili maisha ya wananchi.
Aidha, tuipime kwa huduma zinazowafikia wananchi, kwa ajira zinazopatikana, kwa ubora wa elimu na afya, kwa maji, nishati na miundombinu. Tuipime pia kwa uwezo wake wa kusikiliza wananchi, kukubali pale inapokosea na kurekebisha pale inapobidi.
Kwa sababu hatimaye, serikali haipaswi kuogopa ukosoaji. Ukosoaji wenye hoja unaweza kuwa kioo kinachoonesha maeneo yanayohitaji kurekebishwa.
Serikali bora ni ile inayoweza kusikiliza ukosoaji, kujibu kwa ukweli, kujirekebisha inapobidi na kuendelea kufanya kazi.
Rashid Mtagaluka ni mwandishi wa habari.
- Mitandao ya kijamii
- Mawasiliano ya serikali
- Uwajibikaji