Tafakuri ya Bagonza
Serikali haina na wala haiendi eda
PAMOJA na kwamba nimeshawasilisha salaam zangu za pole kwa mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na familia yake kutokana na msiba walioupata, napenda kwa mara nyingine kuwatakia faraja na subra wakati wote wa msiba.
Ninakujua kufiwa na mwenza na kwa hili sina masikhara. Tunayaonja mauti kwa kufa na kufiwa.
KunamjadalaunaendeleakuhusuMheshimiwa Rais (Mjane) kwenda eda au la? Wanasheria wamesema na viongozi wa dini wamesema pia. Mimi niliye kiboko wa Wajaluo, natafakari mjadala huu kwa tahadhari.
Nijuavyo na kuamini; Rais anaweza kwenda eda lakini serikali haina na haiendi eda.
Serikali yetu si mume au mke wa mtu yeyote.
Kwa hiyo haiwezi kufiwa. Haina dini kwa hiyo haiwezi kwenda Eda.
Viongozi wa serikali wanaweza kuwa na wenza na kuwa na dini, lakini ni zao siyo za serikali. Wenza wa viongozi wa serikali siyo wenza wa serikali kwa sababu serikali haioi wala kuolewa.
Tusijifanye Wajaluo kwa kuchanganya katiba ya nchi na misahafu yetu ya dini. Misahafu inatufanya kuiheshimu katiba; siyo katiba inayofufanya tuifuate misahafu.
Duniani humu kuna dini zinafundisha kuwa mume akifa anazikwa pamoja na mkewe akiwa hai. Je, mkewe akiwa ni rais wa nchi akafiwa na mmewe itakuwaje?
Kuna dini ya Wajaluo inayoruhusu mume kumtandika mkewe hadharani. Je, tutavumilia kumwona rais wetu aliyeolewa na Mjaluo akitandikwa hadharani kwa mujibu wa dini ya Kijaluo? Serikali kutokuwa na dini ni salama yetu wote.
Huku kwetu misiba huwa ni jukwaa la kumaliza migogoro katika ukoo na familia. Ni wakati wa kusikilizana na kusameheana. Si mnajua msibani kila mtu ni mwigizaji halisi?!
Tuigize maridhiano ya kweli basi!
Mwandishi wa safu hii ni Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe. Ni mchangiaji maalum wa safu na makala ndani ya Pambazuko.
- Utawala
- Uwajibikaji