Latra yapanua wigo wa udhibiti, idadi ya leseni za usafiri yapaa kwa asilimia 146
Ndani ya miaka mitano, leseni za usafiri zimeongezeka kutoka 239,953 hadi 590,468, mabasi yanayofuatiliwa kwa satelaiti yamefikia 14,743 huku udhibiti ukitanuka hadi SGR, teksi mtandao na safari za mabasi za saa 24.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Idadi ya leseni za usafiri zinazotolewa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imeongezeka kwa asilimia 146.1 ndani ya miaka mitano, ikiakisi kupanuka kwa sekta ya usafiri na kuingia kwa huduma mpya zinazobadili namna Watanzania wanavyosafiri.
Takwimu za mamlaka hiyo zinaonesha leseni za magari ya abiria, mizigo na magari ya kukodi zimeongezeka kutoka 239,953 mwaka 2021/22 hadi 590,468 mwaka 2025/26 - ongezeko la leseni 350,515 na wastani wa ukuaji wa asilimia 27.2 kwa mwaka.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Dkt. Habib Suluo, wakati aliwasilisha tathmini hiyo kwa wahariri jijini Dar es Salaam Septemba 24, 2026, akieleza mafanikio ya mamlaka katika kipindi cha miaka mitano, 2021/22 hadi 2025/26.
Takwimu zilizotolewa na Dkt. Suluo zilionesha kuwa mbali na kuongezeka kwa leseni, kipindi hicho kimeshuhudia LATRA ikipanua matumizi ya teknolojia katika udhibiti, kuanzishwa kwa safari za mabasi saa 24, ukuaji wa teksi mtandao, kuimarishwa kwa mfumo wa tiketi mtandao na kuongezeka kwa jukumu lake katika usimamizi wa reli.
Magari ya kukodi yaongoza ukuaji
Ukuaji mkubwa zaidi umejitokeza katika magari ya kukodi, kundi linalojumuisha pia baadhi ya huduma zinazotolewa kwa pikipiki, bajaji na magari.
Dkt. Suluo amesema leseni za kundi hilo zimeongezeka kutoka 61,975 mwaka 2021/22 hadi 322,081 mwaka 2025/26 huku leseni za magari ya mizigo nazo zikiongezeka kutoka 143,011 hadi 238,733.
Hata hivyo, picha ni tofauti kwa magari ya abiria, ambako leseni zimepungua kutoka 34,967 mwaka 2021/22 hadi 29,654 mwaka 2025/26.
Hata hivyo, Dkt. Suluo alibainisha kuwa hilo limetokana na kukua kwa sekta ya magari ya kukodi na usafiri wa pikipiki na bajaj.
Teksi mtandao zaingia rasmi kwenye ramani
Dkt. Suluo amesema katika miaka mitano iliyopita imeshuhudiwa huduma za teksi mtandao zikijijengea nafasi katika mfumo rasmi wa udhibiti.
Hadi mwaka 2026, LATRA ilikuwa imesajili na kuidhinisha kampuni 22 za mifumo ya teksi mtandao, zikiwaunganisha watoa huduma wenye leseni hai 23,532.
Kati yao, leseni 11,407 ni za pikipiki za magurudumu mawili, 8,083 za pikipiki za magurudumu matatu na 4,042 za magari.
Mamlaka pia imepanua njia za kupata leseni za magari ya kukodi ambapo baada ya marekebisho ya kanuni mwaka 2023, kampuni, vyama vya ushirika, taasisi za umma na watu binafsi waliruhusiwa kuwa mawakala wa kutoa leseni hizo.
Katika miaka mitatu hadi 2025/26, LATRA ilikuwa imetoa vyeti kwa mawakala 100. Mawakala hao walitoa asilimia 70 ya leseni za pikipiki na kukusanya takribani TSh7.9 bilioni, huku wakilipwa kamisheni ya takribani TSh2 bilioni.
Mabasi 14,743 yafuatiliwa kwa satelaiti
Teknolojia imekuwa sehemu nyingine muhimu ya mabadiliko katika usimamizi wa sekta.
Idadi ya mabasi yaliyounganishwa katika Mfumo wa Ufuatiliaji wa Magari (VTS) imeongezeka kutoka 5,979 mwaka 2021/22 hadi 14,743 mwaka 2025/26.
Mfumo huo unatumia teknolojia ya satelaiti na GPS kufuatilia mwenendo wa mabasi na kupeleka taarifa katika kituo cha ufuatiliaji cha LATRA.
LATRA pia imepanua matumizi ya i-buttons, vitufe vinavyotambulisha madereva wanapoendesha magari yanayofuatiliwa.
Idadi ya madereva waliopewa vifaa hivyo imeongezeka kutoka 256 mwaka 2022/23 hadi 13,829 mwaka 2025/26.
Hatua hizo zimeifanya teknolojia kuwa nyenzo muhimu zaidi katika kufuatilia mwendo wa mabasi na utambulisho wa madereva badala ya kutegemea ukaguzi wa kawaida pekee.
Madereva zaidi ya 15,000 wafanyiwa mitihani
Katika kipindi cha 2022/23 hadi 2025/26, jumla ya madereva 15,547 walifanya mitihani ya kuthibitishwa na LATRA kupitia Mfumo wa Kutahini Madereva.
Kati yao, madereva 8,642 walifaulu na kuthibitishwa, sawa na wastani wa asilimia 56.
Mwaka 2025/26 pekee, madereva 6,356 walifanya mtihani na 4,079 walifaulu, kiwango cha ufaulu cha asilimia 64.
Hata hivyo, takwimu hizo pia zinaonesha eneo linalohitaji kuboreshwa. LATRA yenyewe inasema wastani wa ufaulu wa asilimia 56 unaashiria, pamoja na mambo mengine, maandalizi hafifu ya baadhi ya madereva na changamoto ya kufanya mitihani kwa kompyuta.
Wahudumu 7,216 wapitia mafunzo
Mamlaka pia imeanzisha mfumo wa mafunzo kwa wahudumu wa magari ya abiria.
Kuanzia Januari 2024 hadi Juni 2026, jumla ya wahudumu 7,216 walipata na kufaulu mafunzo yanayotolewa kupitia NIT, CBE, VETA na Chuo cha Ufundi Arusha.
Kati yao, 4,664 walikuwa wamesajiliwa LATRA na kupatiwa kadi hadi mwisho wa mwaka wa fedha 2025/26.
Tiketi mtandao yashika kasi
Katika eneo la tiketi, LATRA ilianza kutekeleza mfumo wa tiketi mtandao mwaka 2022/23 na baadaye kuunganisha huduma za mabasi na treni kupitia mfumo mkuu wa Core e-Ticketing System (CeTS).
Hadi Juni 2026, mifumo ya watoa huduma 14 wa tiketi mtandao ilikuwa imeunganishwa na LATRA. Mfumo huo unamwezesha abiria kuchagua safari, basi au treni na kulipia tiketi.
Katika miaka minne, mfumo umerekodi abiria milioni 62.18 na nauli zenye thamani ya TSh2.13 trilioni. Idadi ya abiria waliorekodiwa kwa mwaka iliongezeka kutoka milioni 7.11 mwaka 2022/23 hadi milioni 28.67 mwaka 2025/26.
Pamoja na maendeleo hayo, matumizi ya malipo ya mtandaoni bado ni madogo: asilimia 95.3 ya abiria katika kipindi hicho walilipa kwa fedha taslimu. Hivyo, digitali imepanua mfumo wa tiketi, lakini haijaondoa utegemezi mkubwa wa fedha taslimu.
Safari za saa 24 zabadilisha usafiri wa mabasi
Mageuzi mengine makubwa ni kuruhusiwa kwa mabasi ya masafa marefu kusafiri usiku na mchana.
Ratiba za saa 24 zilianza rasmi Oktoba 1, 2023 baada ya kuimarika kwa miundombinu, mawasiliano na uwezo wa kufuatilia mabasi kupitia VTS.
Kwa mujibu wa tathmini ya LATRA ya mwaka 2024/25, safari za usiku zimepunguza msongamano katika stendi na kuwapa abiria chaguo kubwa la muda wa kusafiri.
LATRA inasema mfumo huo pia umepunguza gharama za malazi kwa baadhi ya wasafiri, hasa wafanyabiashara wanaoweza kusafiri usiku na kutumia mchana kwa shughuli za uzalishaji. Kwa waendeshaji, mamlaka inasema safari hizo zimeongeza fursa za biashara na uwekezaji.
Udhibiti wa reli nao wapanuka
Ukuaji wa usafiri wa reli, ikiwemo SGR, umeongeza eneo jingine la majukumu ya LATRA.
Katika miaka mitano hadi 2025/26, mamlaka ilifanya kaguzi 275 za reli, zikihusisha miundombinu, mifumo ya ishara na mawasiliano, vichwa vya treni, mabehewa na uendeshaji. Kati ya hizo, 143 zilifanyika TRC na 132 TAZARA.
Kwa SGR, LATRA ilithibitisha ubora wa vichwa vipya 17 vya treni, mabehewa 56 ya abiria, treni 10 za umeme (EMU), injini nane za TRC na mabehewa 264 ya mizigo kabla ya kuanza kutoa huduma kwa umma.
Mamlaka pia ndiyo iliyoidhinisha nauli za daraja la uchumi za SGR zilizoanza kutumika Juni 2024, ikiwemo TSh31,000 kwa treni ya kawaida na TSh50,000 kwa treni ya express kati ya Dar es Salaam na Dodoma.