Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Habari

Lishe shuleni yatokomeza utoro Meatu

HALMASHAURI ya Wilaya ya Meatu, mkoani Simiyu, kwa kushirikiana na Taasisi ya Uhifadhi ya Friedkin Conservation Fund (FCF), imepunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la utoro shuleni kupitia Mpango wa Lishe Bure Shuleni.

Jumatatu, 21 Septemba 2026 · 06:00Dakika 2 kusomaToleo 183, uk. 29

Mpango huo unaotekelezwa katika Shule ya Msingi Makao, umekuwa suluhisho la moja kwa moja kwa changamoto iliyokuwa ikikwamisha maendeleo ya elimu, ambapo baadhi ya familia zililazimika kuwaacha watoto nyumbani kufanya kazi badala ya kwenda shule kutokana na uhaba wa chakula.

Ofisa Kitengo cha Miradi wa Friedkin, Baraka Mabula, amesema wanafunzi 1,092, wakiwamo wavulana 534 na wasichana 585, hupata chakula cha mchana kila siku ya masomo, jambo ambalo limebadili mwenendo wa mahudhurio shuleni.

Mabula amesema takwimu za miaka minne zinaonyesha utoro umeshuka kutoka asilimia 30 hadi asilimia mbili mwaka 2025.

Amesema kupungua kwa utoro kwa kiwango hicho ni ushahidi wa mabadiliko yaliyotokana na upatikanaji wa chakula shuleni, huku taarifa za walimu zikionesha pia kuimarika kwa ufaulu wa wanafunzi.

“Chakula cha uhakika shuleni hakijaboresha mahudhurio pekee, bali pia kimeleta mabadiliko chanya katika ufaulu wa wanafunzi,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Fauzia Ngatumbura, amesema mradi huo umekuwa mfano kwa wilaya hiyo na Mkoa wa Simiyu, akieleza kuwa unaonyesha mchango wa shughuli za uhifadhi katika maendeleo ya jamii.

Amesema Friedkin, kupitia kampuni zake zinazowekeza katika shughuli za uhifadhi, ikiwamo Mwiba Holdings, imechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya elimu wilayani humo.

“Siyo tu wanatoa chakula, bali katika maeneo mengine wamejenga madarasa na nyumba za walimu, na pia wametoa baiskeli zinazowasaidia watoto kufika shule kwa wakati,” amesema.

Mbunge wa Kisesa, Musa Godfrey Mbuga, amesema mchango wa Friedkin na Mwiba katika maendeleo ya wilaya hiyo ni mkubwa, akitaja pia fursa za ufadhili wa masomo zinazotolewa kwa wanafunzi.

“Mwiba kupitia miradi ya uwekezaji ya SWI- CA wanatoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa Meatu. Tunaomba wapanue zaidi huduma hii kwani ina faida kubwa,” amesema.

Meneja wa Miradi wa Friedkin, Aurelia Mtui, amesema mpango huo ni sehemu ya jitihada za kuunganisha maendeleo ya jamii na uhifadhi wa mazingira na wanyamapori.

Amesema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na jamii kuleta maendeleo, huku ikiitaka jamii kuendelea kuhifadhi mazingira na kulinda wanyamapori.

Kwa upande wake, Ofisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Elizabeth Kiraya, amesema mafanikio ya mpango huo yanapaswa kuigwa katika maeneo mengine.

Kiraya amewataka wazazi na wawekezaji kuanzisha miradi kama hiyo katika vijiji vingine ili kutokomeza zaidi utoro na kuongeza fursa za elimu kwa watoto.

Amesema Halmashauri itaendelea kuhamasisha ushirikiano wa wadau ili kupanua mpango huo katika shule nyingine, ikisisitiza kuwa elimu bora huanza na mtoto mwenye afya na aliyeshiba.

  • Elimu
  • Lishe
  • Friedkin
  • Meatu
  • Simiyu

Soma Pia