Makala
Pengo elimu afya ya uzazi tishio ustawi wa vijana - II
KATIKA sehemu ya kwanza ya makala haya tuliona jinsi ukosefu wa elimu sahihi ya afya ya uzazi unavyoathiri makundi ya vijana katika Mkoa wa dodoma.

Wengi hudhani kuwa hali kama hiyo huwaathiri tu vijana ambao hawana elimu kubwa, lakini uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa hata vijana wenye elimu kubwa nao wameathirika na hali hiyo.
Katika Chuo Kikuu cha Dodoma hali haikuwa tofauti.
Wanafunzi waliozungumza na mwandishi wa Makala haya walisema elimu ya afya ya uzazi hupatikana zaidi kupitia makongamano na semina zinazoratibiwa na wadau mbalimbali, lakini washiriki ni wachache.
Mwanafunzi mmoja wa UDOM anasema; “Mara nyingi wanaopata nafasi ni viongozi wa wanafunzi au waliopo kwenye Klabu za Jinsia (Gender Club). Wanafunzi wengi hawafiki kabisa.”
Wanafunzi wengi wanasema kuwa hali hiyo imewafanya vijana wengi kutegemea taarifa kutoka kwa marafiki na mitandao ya kijamii kuliko wataalamu wa afya.
Wataalamu wa afya wanaonya kuwa pengo la elimu ya afya ya uzazi lina athari zinazozidi mimba za utotoni pekee.
Pengo hilo pia linaongeza maambukizi ya magonjwa ya zinaa, changamoto za afya ya akili, utoaji mimba usio salama pamoja na kusitishwa kwa masomo kwa baadhi ya vijana.
Dodoma matokeo hayaonekani
Serikali kupitia Mpango wa Kitaifa wa Uzazi wa Mpango (National Family Planning Costed Implementation Plan; 2019–2023) inautaja Mkoa wa Dodoma kuwa miongoni mwa maeneo ya kipaumbele katika kupanua elimu ya afya ya uzazi na kuongeza upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango.
Hata hivyo, uchunguzi huu unaonyesha vijana katika Makulu, Iyumbu, Ntyuka, Ng'ong'ona na hata Chuo Kikuu cha Dodoma bado wanategemea kampeni za muda mfupi kupata elimu ya afya ya uzazi badala ya kuwa na mfumo endelevu wa elimu.
Daktari mmoja anasema; “Elimu ya afya ya uzazi siyo elimu ya kuzuia mimba pekee, ni elimu ya kumwezesha kijana kufanya uamuzi sahihi kuhusu mwili wake, afya yake na maisha yake.”
Mahojiano ya wadau mbalimbali yamebainisha kuwa changamoto kubwa siyo ukosefu wa sera wala sheria kwa kuwa zipo.
Tanzania imekuwa na Sheria ya Afya ya Umma ya mwaka 2009, Sheria ya Kudhibiti VVU na Ukimwi ya mwaka 2008 pamoja na National Adolescent Friendly Health Services Guidelines zinazotaka vituo vya afya kutoa huduma rafiki kwa vijana.
Miongozo hiyo inasisitiza huduma zinazolinda faragha, utu na usiri wa vijana.
Hata hivyo, uchunguzi huu unaonyesha kuwa utekelezaji wa matakwa haya ya kisheria bado una upungufu mkubwa.
Kwa nchi inayotarajia kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kuendelea kuwaacha vijana wakitegemea taarifa kutoka kwa marafiki na mitandao ya kijamii kuhusu afya ya uzazi kunaweza kuwa na gharama kubwa zaidi kuliko inavyoonekana leo.
Gharama za ukimya
Madhara ya pengo hili hayaishii kwenye mimba za utotoni pekee.
Takwimu za kitaifa zinaonyesha Tanzania bado inapoteza wastani wa akina mama 233 kwa kila vizazi hai 100,000. Wataalamu wanaeleza kuwa vijana waliopata ujauzito bila maandalizi huwa katika kundi lenye hatari kubwa ya kupata matatizo ya uzazi.
Aidha, Sensa ya mwaka 2022 inaonyesha kuwa asilimia 63.2 ya wasichana wa vijijini wenye umri wa miaka 15 hadi 17 waliopata ujauzito hulazimika kuacha shule, jambo linalopunguza fursa zao za elimu na kipato.
Ushahidi uliokusanywa katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma unaonyesha kuwa changamoto kubwa si ukosefu wa sheria wala sera. Tatizo ni kushindwa kuzitekeleza kwa kiwango kinachoweza kuwafikia vijana wote.
Wakati vijana ni zaidi ya theluthi moja ya wakazi wa Mkoa wa Dodoma, zaidi ya asilimia 60 bado wana uelewa mdogo wa afya ya uzazi, huku karibu msichana mmoja kati ya watatu akiwa tayari amewahi kupata ujauzito.
Takwimu hizi zinaonyesha kuwa gharama ya kutowekeza katika elimu ya afya ya uzazi si ya mtu mmoja mmoja, bali ni ya jamii na taifa kwa ujumla.
Bila mfumo endelevu wa elimu, huduma rafiki kwa vijana na uwajibikaji wa viongozi katika kusimamia utekelezaji wa sheria zilizopo, Dodoma itaendelea kupoteza kizazi cha vijana kinachopaswa kuwa nguvu kazi ya maendeleo.
Tuendako
Ushahidi uliokusanywa katika Jiji la Dodoma kupitia mahojiano na watu mbalimbali unaonyesha kuwa changamoto haipo katika ukosefu wa sheria wala sera, bali katika pengo la utekelezaji.
Wakati takribani msichana mmoja kati ya watatu tayari amewahi kupata ujauzito na zaidi ya asilimia 60 ya vijana wakionyesha uelewa mdogo kuhusu afya ya uzazi, wataalamu wanaamini suluhisho linahitaji elimu endelevu, huduma rafiki kwa vijana na uwekezaji wa muda mrefu badala ya kampeni za msimu.
Bila hatua hizo, pengo la elimu ya afya ya uzazi litaendelea kuzalisha kizazi kinachoingia utu uzima bila taarifa sahihi za kufanya uamuzi unaogusa afya, elimu na mustakabali wa maisha yao.
Mwandishi ni mwanafunzi wa shahada ya uandishi wa habari katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
- Afya ya uzazi
- Vijana
- Dodoma
- Elimu