Habari
Lissu alivyohitimisha mchuano wa ushahidi mahakamani
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amehitimisha safari ya siku tano ya kuwasilisha ushahidi wake binafsi, katika kesi ya uhaini inayomkabili.

Lissu anayekabiliwa na kesi ya uhaini namba 19605/2025 alianza utetezi wake Ijumaa - Agosti 21, 2026, ikiwa ni mwendelezo wa kesi hiyo iliyodumu kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.
Katika uamuzi wa mahakama baada ya kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka, jopo la majaji watatu wanaosikiliza kesi hiyo wakiongozwa na Jaji Jaji Dunstan Ndunguru, liliamua Lissu ana kesi ya kujibu, hatua iliyofungua njia kwa mwanasiasa huyo kuanza kujitetea. Majaji wengine ni James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.
Ijumaa iliyopita, ikiwa ni wiki moja tangu alipoanza kutoa ushahidi wake, Lissu alimaliza kwa mvutano wa kimantiki, akipambana na mawakili wa serikali ambao walitaka asipate nafasi ya kuhojiwa tena ili kusahihisha maeneo aliyoona yalikuwa na mapungufu baada ya maswali ya dodoso kutoka kwao.
Kabla ya kuhitimisha ushahidi wake ili kuruhusu kuanza kusikilizwa kwa mashahidi wangine, Lissu aliibua mabishano makali baada ya kutaka ahojiwe tena ili atoe ufafanuzi katika baadhi ya maeneo.
Ombi hilo lilipingwa vikali na kiongozi wa jopo la mawakili wa serikali, Nassor Katuga, ambaye aliieleza mahakama kuwa upande wa Jamhuri unafahamu kuhojiwa tena ni njia moja wapo ya shahidi kutoa ushahidi na ipo kisheria na ila waliomba kwa mujibu wa sheria shahidi ajikite kwenye yale maswali aliyohojiwa na asilete jambo jipya.
“Ni jinsi gani atajihoji ili kufikia lengo la kutoa ufafanuzi wa majibu yake wakati wa kuhojiwa na upande wa pili, suala ambalo tunaomba mahakama hii tuulize, shahidi ni mtu ambaye anajiwakilisha mwenyewe sasa kuhojiwa tena itafanyikaje?
“Ajiulize maswali mwenyewe na ajijibu mwenyewe kuna hatari ya kuleta ushahidi mpya kabisa maana lengo la kuhojiwa tena ni kufafanua sasa kujiuliza mwenyewe atakuwa hakimu wa mwenendo wake mwenyewe, sasa zile kanuni zetu zinakinzana na hiki...”
“Kama angekuwa na wakili sawa ila wewe mwenyewe ujiulize na ufafanue ili kuepuka mkanganyiko mahakama inaweza ikamuuliza kwa vile vipande ambavyo inaona vinahitaji ufafanuzi,” alisema Katuga.
Katuga aliwaeleza majaji katika kesi hiyo kuwa wanataka mahakama imuelekeze shahidi atoe maelezo kama itahitajika kufanya hivyo kwenye majibu yake yenye maana zaidi ya moja na siyo kufungua sababu ya kutoa uwanda wa kutoka nje ya yale ambayo yanayohitaji ufafanuzi.
Baada ya ombi hilo la Katuga, Lissu aliieleza mahakama kuwa kwa kuwa ni mwongozo, suala la kuhojiwa tena ni haki ya shahidi aliyekuwa akihojiwa na upande wa pili, ndio maana kwa mujibu wa sheria, shahidi atakuwa wa kwanza kutoa ushahidi na kama upande wa pili utamhoji na shahidi huyo akitaka kuhojiwa tena ni haki yake na kama ni haki alipaswa kunyamaza kimya.
“Wakili wa serikali mkuu anasema atajiongozaje sababu hana wakili, ukweli kwamba shahidi ndiye mshitakiwa na anajiwakilisha mwenyewe kitakachofanyika ni kurejea maswali yaliyoulizwa na majibu yake na kufafanua kwa hiyo hakuna chochote cha kutolea mwongozo sheria iko wapi, hii inaweza kuwa ni fursa ya kuingiza mambo mapya?
“Utaratibu uko wazi kama kutakuwa na mambo mapya watafanya pingamizi kwa hiyo hawapaswi kuwa na hofu ya bure sasa waheshimiwa majaji hamna mwongozo wa kutoa,” alisema Lissu.
Maelezo hayo ya Lissu yalikubaliwa na jaji ambaye alisema huo ndio mwongozo wenyewe, hatua iliyomfanya Lissu kuwaomba majaji kuwa wawe makini kwa kuwa iwapo watalazimika kutoa mwongozo kwenye jambo dogo kama hilo, inabidi wawe macho na upande wa mashtaka.
Baada ya muongozi huo wa jaji, Lissu aliendelea kutoa ufafanuzi katika baadhi ya maeneo aliyoona anahitaji kufanya hivyo, akiendelea kuulizwa maswali ya dodoso na mawakili wa serikali kila walipoona wanahitaji kufanya hivyo.
Lissu alitumia nafasi hiyo kutoa ufafanuzi wake katika kila eneo aliloona lina upungufu au alitoa majibu ambayo hayakueleweka vizuri wakati alipokuwa akitoa maelezo au kuulizwa maswali ya dodoso na mawakili wa Serikali.
Alivyojitetea
Katika siku tano za kutoa ushahidi wake, Lissu aliieleza mahakama kwa urefu kuhusu maisha yake, ikiwemo namna alivyoshiriki katika harakati za kutetea haki za watu katika maeneo mengi nchini tangu alipokuwa shule.
Lissu alitumia nafasi hiyo kueleza pia safari yake ya kiaisa na misukosuko aliyoipata ikiwemo kukamatwa, kufunguliwa kesi kila mara na hata namna alivyonusurika kuuawa wakati akiwa mbunge, baada ya watu wasiojulikana kumvamia alipokuwa katika eneo la makazi yake mjini Dodoma mwaka Septemba 2017.
Pia alieleza safari yake ya matibabu nje ya nchi na hatimaye kujikuta akiishi uhamishoni, hadi alipokutana na Rais Samia Suluhu Hassan, alivyorejea nchini na kushiriki kwenye uchaguzi mkuu wa 2020 akiwa mgombea dhidi ya John Magufuli.
Lissu pia alieleza mazungumzo waliyofanya na Rais Samia mwaka 2021 akwia nchini Ubelgiji hadi yeye na wenzake waliokuwa nje ya nchi kwa kuhofia usalama wao walipoamua kurejea nchini.
Katika kesi hiyo, Lissu aliieleza mahakama kuwa yeye atajitetea mwenyewe na alianza kwa kutoa utetezi wake huku akiwataja mashahidi wake wengine kuwa ni kiongozi mkuu wa Serikali, Rais Samia Suluhu Hassan, aliyekuwa Makamu wa Rais, Dkt. Phillip Mpango, aliyekuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob Mkunda.
Wengine ni Inspekta wa jeshi la Polisi (IGP) Camillus Wambura, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Ramadhani Kingai, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Suleiman Mombo na Kamishna wa Polisi (DCP) Ramadhani Ng'anzi.
Pia aliwataja wanaharakati kutoka nchi za Afrika Mashariki ambao ni Agather Atuhaire, Boniface Mwangi, Dkt Willy Mutunga, Martha Karua, mwandishi wa habari John Marwa, na viongozi wa Chadema ambao ni Amani Golugwa, John Heche na John Mnyika.
Baada ya Lissu kuhitimisha kutoa ushahidi wake, mahakama ilianza kusikiliza ushahidi wa mashahidi wengine wa upande wa utetezi kwa kufanya mahojiano na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika mahakamani hapo ambaye ataendelea kutoa ushidi wake leo, Jumatatu Agosti 31, 2026.
- Tundu Lissu
- Chadema
- Mahakama
- Uhaini