Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Uhusiano

Mabinti lindeni thamani yenu

HABARI za leo msomaji wa safu hii ya uhusiano na karibu uweze kujipatia elimu na ujuzi mbalimbali wa masuala ya maisha.

Jumatatu, 31 Agosti 2026 · 06:00Dakika 2 kusomaToleo 180, uk. 34
Wasichana
Wasichana — Kutoka Maktaba ya Pambazuko

Wiki iliyopita nilizungumza umuhimu wa kumtanguliza Mungu mbele kwenye kila jambo unalofanya na wiki hii nitazungumza umuhimu wa binti kujua thamani yake.

Binti anapaswa kutambua thamani yake ili aweze kujenga maisha yenye mwelekeo na mafanikio.

Thamani ya binti haipimwi kwa kupendwa na wanaume wa aina tofauti au kwa namna nyingine, bali kwa kujithamini.

Katika zama za sasa mabinti wengi wamekuwa wakitumia njia za mkato pale wanapotongozwa na wanaume hasa wenye umri mkubwa 'mashuga dadi' na kuamua kujenga uhusiano nao na kusahau kuwa kufanya hivyo kunawachelewesha kutafuta maisha yao ya baadaye ya kujenga familia zao na maisha kwa ujumla.

Mabinti hao huanzisha uhusiano na wanaume hao ambao huwarubuni kwa kuwapatia zawadi kama simu, pesa na anasa ili washawishike kuwa nao na waingiapo hujichia wakati mwingine kuzaa nao.

Hali hiyo huwafanya wengi kupumbazwa na uhusiano huo usio na faida na mwisho wa siku huwafanya kushindwa kutengeneza maisha yao ya baadaye.

Kutokana na kujiingiza huko kwenye uhusiano usio na msingi na wanapotelekezwa hubaki wakilea kwa changamoto watoto waliopewa na wanaume waliokuwa na uhusiano nao na kubaki wakijuta.

Wengine hujitumbukiza kwenye uhusiano huo wakiwa shuleni na baadaye kujikuta wakipoteza masomo na muda wao.

Wengi wao hujitumbukiza kwenye mambo hayo kwa kufuata mkumbo(kuiga) kutoka kwa wengine na kusahau kuwa mwisho wa mambo hayo huwa ni mbaya.

Binti kabla hajafikia kutaka kufanya jambo lolote anatakiwa kuwa na maamuzi yake binafsi kutafakari na kufikiri kwa undani kuhusu faida na hasara zake.

Ili kutojiweka kwenye misukosuko binti anatakiwa kuepuka shinikizo lolote la marafiki au kuingia tamaa za muda mfupi katika kupata kitu fulani pia kufikiri na kuwa na uamuzi wa kukubali jambo linalomfaa na kulikataa lisilomfaa kwani hali hiyo itamsaidia kutimiza ndoto zake njema.

Binti akumbuke kuwa uamuzi wake binafsi ndiyo njia pekee inayoweza kumpatia nguvu ya kujisimamia na kujipanga bila kutegemea mtu mwingine.

Wazazi, walimu na jamii wana wajibu wa kuwakumbusha mabinti kila wakati kuhusu thamani yao na namna ya kuilinda na kujiheshimu.

Wakielewa na kujiheshimu, hawatapoteza wakati bali watajenga kesho yao iliyo bora.

Tukutane wiki ijayo.

  • Uhusiano
  • Mabinti
  • Vijana

Soma Pia