Uhusiano
Siri yako ni mali yako
HABARI za wiki hii msomaji wangu wa safu ya uhusiano. Karibu tushiriki elimu na ushauri kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu eneo hilo.
Leo nitaeleza umuhimu wa kutomshirikisha rafiki mambo yako ya ndani.
Urafiki ni mzuri na hakika ni baraka, lakini siyo kila mlango wa moyo wako unapaswa kuwa wazi kwa kila mtu.
Leo watu wengi wameumizwa na rafiki wa karibu.
Kuna unayemwambia ndoto yako na kesho yake ndoto hiyo ikawa utani wa mtaa.
Mwingine unaweza kumwambia shida ya kifedha na wiki moja baadaye ikawa soga mezani yako ni mali yako ni kwa watu wasiomhusu.
Mwingine unaweza kumwamini na kumpa namba za siri ya akaunti yako na baada ya muda ukaibiwa.
Hili linatokea kwa sababu tatu kuu; kwanza kuna watu ambao kinywa chao hakiwezi kukaa kimya. Unachokwambia leo kwa siri, kesho kinaweza kuenea kwenye vikundi vya WhatsApp, TikTok na kwingine.
Jambo jingine ni wivu; hapa unaweza kukuta rafiki anayejua maendeleo yako akatabasamu na wewe, lakini moyoni akatamani usiendelee na wakati mwingine akijua mipango yako yote mikubwa anaweza kuikwamisha kimya kimya bila wewe kujua.
Pia kuna suala la ugomvi; inawezekana leo akawa rafiki na kesho mkawa maadui na ile habari uliyompa wakati mkiwa mmeshibana kwa uaminifu inageuka kuwa silaha ya kukupiga.
Hii haina maana kuwa na shaka na watu wote au kuishi kama kifungoni.
Kuna mambo yako ambayo si lazima kila mtu ayajue. Mipango yako ya kifedha, udhaifu wako wa ndani, na siri za familia yako ni mali binafsi. Mpe mtu kiasi cha imani anachostahili, usimpe kila kitu.
Mjaribu kwanza na mambo madogo. Kama hawezi kuyahifadhi, basi usimpe makubwa.
Kumbuka kanuni moja; maji yakimwagika hayazoleki. Neno likitoka kinywani mwako halirudi. Linda amani yako kwa kujua pa kusema na pa kukaa kimya.
Urafiki wa kweli hauvunjiki kwa sababu umeka kimya. Badala yake unaimarika zaidi kwa sababu una mipaka na heshima.
Linda hekima yako, linda siri yako na hakikisha urafiki wako na mwingine unakuwa na mipaka Tukutane wiki ijayo.
Kwa maoni na ushauri: hellen2ngoromera@ gmail.com Au simu: 0715 88 67 49.
- Uhusiano
- Urafiki
- Ushauri