Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Habari

Mtifuano wa maslahi, madaraka jezi za Taifa Stars

Kumekuwepo na vuta-nikuvute kuhusu ubora wa jezi za Taifa Stars kati ya waziri mwenye dhamana, Makonda, mzabuni na mawazo gongana ya wadau, Pambazuko linaeleza kinaga-ubaga.

Jumapili, 20 Septemba 2026 · 21:39Dakika 6 kusoma
Mfanano wa jezi za Taifa Stars ambazo zimeibua sintofahamu.
Mfanano wa jezi za Taifa Stars ambazo zimeibua sintofahamu. — Picha ya AI ikutoka Pambazuko

MVUTANO kuhusu jezi za timu za Tanzania kwenye michuano ya kimataifa, umechukua sura mpya ambapo wadau wameubatiza jina la “mtifuano.”

Baadhi ya wadau hao wanaona kuwepo kwa vita ya maslahi, mapambano ya madaraka na wengine wakiutafsiri kuwa sehemu muhimu ya kuboresha utendaji wakati nchi ikiwa kwenye maandalizi ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2027).

Mvutano wa mawazo, mitazamo na tafsiri tofauti zilizoibua mtifuano huo zinakuja baada ya kauli ya Waziri wa Habari na Michezo, Paul Makonda, ambaye Alhamisi - Septemba 16, 2026 aliibua vuta nikuvute wakati alipotuma ujumbe kupitia ukurasa wake wa Instagram akipinga jezi za timu ya taifa zilizotangazwa na naibu wake, Khamis Mwinjuma.

Makonda aliandika; “Hii siyo jezi ya Taifa Stars. Taifa Stars kwa ubora wake hatuwezi kuwa na jezi za kiwango cha chini hivi. Acheni kutumia picha za naibu wangu, huku ofisi yangu haina taarifa. Tuheshimiane.”

Kauli iliyoonekana kuelekezwa kwa naibu wake, Hamis Mwinjuma na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Taarifa hiyo ya Makonda ilipokelewa kwa maoni na mitizamo tofauti, ambapo mwanasiasa na kiongozi mstaafu wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe aliandika kwenye ukurasa wake wa X akisema; “Mchakato wa jezi ya timu ya taifa unasimamiwa kwa utaratibu wa mikataba kati ya chama cha soka na kampuni inayotengeneza jezi…”

“Kama waziri ana kampuni nyingine anadhani ni bora zaidi kuliko ya sasa asubiri mkataba uishe.” Zitto alimtaka Makonda arudishe mawe mfukoni na kuondoa taharuki isiyo na sababu iliyotokana na ‘post’ yake.

Mwingine aliyekosoa kauli ya Makonda ni mbunge wa zamani wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo ambaye aliandika katika ukurasa wake wa X; “Naomba kufahamu jezi bora kama hizi zinapatikana wapi kwenye jimbo letu la Arusha Mjini, nami nikanunue?

Binafsi sijaona tatizo labda kama kuna mtu kanuna kwa kuwa hajashiriki kwenye mchakato wa kumpata mzabuni. Duniani kubali mengine yakupite!”

Mawazo gongana zaidi

Uchambuzi uliofanywa na Pambazuko kupitia kauli na ujumbe wa wadau wa michezo umebaini kuwepo kwa mnyukano wa kupambania maslahi kwa mizania tofauti, usimamizi wa taswira ya Tanzania na mgongano wa biashara.

Katika maandishi ya Makonda, Sandaland na wadau wengine, kila kundi linaona kuwepo kwa ulazima wa kufanikisha jambo miongoni mwa hayo yaliyoibuliwa.

Kimsingi, Makonda ameona hadhi ya Tanzania, ambayo ni miongoni mwa nchi wenyeji wa michano mikubwa ya Afcon, imedogoshwa na ubora wa jezi hizo, huku walioshinda zabuni wakiamini walifanya kazi yao, hivyo kauli ya waziri inakwamisha biashara  yao.

Pia wapo wadau wanaoamini kwamba katika sakata hili kuna kuonyeshana ubabe wa nani mwenye mamlaka zaidi; wizara, TFF katika kuamua timu za taifa zivae jezi za namna gani katika michuano ya kimataifa.

Taarifa ya wizara

Katikati ya mjadala huo, mchana wa Septemba 18, 2026 taarifa ya wizara ilisisitiza kuwa waziri wake hatambui matangazo ya jezi za Taifa Stars kutokana na mchakato wa kuzibadilisha kutoshirikisha wizara licha ya maelekezo aliyoyatoa Makonda Februari, 2026.

Taarifa hiyo kwa umma, pamoja na kutokutambua utambulisho wa jezi hizo, ilisema Makonda ataunda kamati ya kuchunguza mkataba wa utengenezaji wa jezi hizo.

“Katika maelekezo hayo, Makonda alielekeza kwamba, kwa kuwa serikali inawekeza fedha nyingi katika maandalizi ya timu za taifa zinazoshiriki mashindano ya kimataifa, na kwa kuwa Tanzania itakuwa mwenyeji wa mashindano makubwa ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2027)...”

“Kuna haja ya kuboresha jezi za timu za taifa ziakisi manufaa mapana kwa nchi,” ilisema taarifa hiyo iliyosainiwa na kaimu mkuu wa kitengo cha mawasiliano serikalini, Zaituni Mkwama.

Pambazuko linatambua kuwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ndiyo iliingia mkataba na Kampuni ya Sandaland Fashion Wear ya Dar es Salaam kutengeneza jezi hizo kwa kandarasi ya miaka mitano yenye thamani ya Shilingi bilioni tatu kuanzia mwaka 2023.

Misimamo tofauti yaibuka

Ahadi Kakore, ambaye ni mdhamini na wakala wa kusaka vipaji vya soka kwa vijana ndani na nje ya Tanzania, pamoja na kutovutiwa na ubunifu wa jezi hizo, alisema TFF ndiyo wenye mamlaka kisheria kutoa zabuni kwa kampuni za nje na za ndani kutengeneza jezi za timu za taifa, na serikali haipaswi kuingilia sana.

Mwandishi wa habari za michezo ambaye hakutaka jina liwekwe wazi amesema suala la jezi siyo jambo jepesi kama watu wanavyodhani.

“Michakato ya kupata jezi ni mirefu, inaanza kutangazwa zabuni, watu wanaleta sampuli zinakaguliwa kwa kuangalia ubora, rangi na vitu vingine vingi, baadaye mshindi anapewa ruhusa ya kutengeneza, sasa kama zilipita kote huko, leo useme hazifai, hasara hizo anazibeba nani?” amehoji.

Wadau wazungumza

Aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, amesema kuna walakini katika uandaaji wa jezi hizo za Taifa Stars, hivyo Makonda anaweza kuwa sahihi katika kile alichokieleza.

Amesema kwa kuwa Tanzania inaandaa fainali za Afcon, tayari serikali ina mkono wake katika kuhakikisha kunakuwa na mwamko wa wadau na wananchi, hivyo kujenga taswira pana ya kitaifa, suala ambalo halionekani sana katika uandaaji wa zabuni na hatua zingine.

Osiah amesema ni jambo la kushangaza kuwa waziri ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya Afcon, hajui utaratibu uliofanyika hadi jezi hizo zinazinduliwa yeye akiwa ndiye mdau muhimu kwa maana ya upande wa serikali.

“Tunapoangalia tukio la uzinduzi wa jezi ya Taifa Stars hususan katika kipindi hiki ambacho Tanzania inaandaa mashindano ya Afcon, kwa hiyo suala kama hili la uzinduzi wa jezi ya taifa lilitakiwa lifanyike kwa ukubwa wake, wadau wote wajue kuna kitu kimefanyika, lilitakiwa liwe tukio kubwa la kitaifa...”

“Lakini kwa namna lilivyofanyika, unaona kama kweli mwaliko ulienda kwa naibu waziri moja kwa moja, kama kweli waziri hakuwa na taarifa, inaleta picha kuwa alipuuzwa...”

“Lazima aone kwamba kuna nini nyuma ya pazia. Kwa mtiririko wa matukio hasa kuelekea Afcon serikali ilitakiwa ihusike moja kwa moja katika uzinduzi mkubwa ili kuweka alama,” amesema Osiah.

 Aidha, aliongeza kuwa ana uhakika uongozi wa TFF chini ya Wallace Karia hauwezi kuwa umefanya ujanjaujanja wowote kwenye suala la utoaji wa zabuni kwa kadri anavyomfahamu.

Mdau wa michezo ambaye pia amewahi kuwa msemaji wa TFF, Alfred Lucas, aliieleza Pambazuko kuwa, hatua hiyo inaibua sintofahamu katika kipindi hiki ambacho serikali inajielekeza katika kuandaa Timu ya Taifa kwa ajili ya Afcon inayotarajiwa kufanyika mwakani.

Amesema kwa miaka yote jukumu la usimamizi wa utengenezaji wa jezi za taifa limekuwa likisimamiwa kwa uhuru na TFF na serikali imekuwa ikiheshimu uhuru huo kisheria, kwa kuwa msimamizi wa moja kwa moja wa TFF ni Baraza la Michezo la Taifa (BMT).

Lucas amesema kinachoonekana kwa sasa ni kwamba huenda kwa kuwa kuna maandalizi ya Afcon ndiyo maana kumekuwa na mambo mengi yanayoingilia uhuru huo, suala ambalo linawachanganya hadi wadau wa michezo.

Mwandishi huyo ambaye sasa ni mwanasheria amesema iwapo busara ya kutosha haitatumika, suala hilo linaweza kuiingiza serikali kulipa gharama zisizo za lazima kwa kuwa tayari Sandaland aliingia mkataba na kutumia gharama kubwa kutengeneza jezi hizo, ambazo tayari zilishafikishwa madukani kwa ajili ya kuanza kuuzwa.

 Sandaland waja juu

Kabla sakata hilo halijapoa, Kampuni ya Sandaland Fashion Wear Limited imetangaza kuchukua hatua za kisheria dhidi ya kauli iliyotolewa hadharani na Makonda, kuhusu jezi za Taifa Stars.

Hatua hiyo imetangazwa kupitia tamko rasmi la kampuni hiyo Septemba 18, 2026 ambayo imesema, kauli ya Makonda iliyotolewa Septemba 16, 2026 kupitia akaunti yake ya Instagram imeathiri jina, chapa, hadhi na uhalali wa bidhaa za Sandaland katika soko.

“Kauli hiyo imezua taharuki na sintofahamu, na tayari imesababisha madhara ya kiuchumi na kwa hadhi ya kampuni. Tunao mkataba halali na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wa kutengeneza na kusambaza jezi za Taifa Stars, ambazo zimekwishatumika katika mashindano mbalimbali ya timu za taifa za wanaume na wanawake,” imeeleza taarifa hiyo.

Kutokana na hali hiyo, Sandaland imesema haitanyamaza na inakusudia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya kauli hiyo, ikidai kuwa ilitolewa kwa namna inayoweza kuichafua chapa yake.

Kampuni hiyo pia imesisitiza kuwa imejenga jina na heshima yake kwa muda mrefu na ilipewa dhamana kupitia mkataba ya kushughulikia jezi za Taifa Stars.

  • tff
  • jezi
  • afcon
  • tanzania
  • makonda
  • mpira

Soma Pia