Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Tanzia

Mama Fatma Karume, mwanamke aliyeacha alama Zanzibar

Watanzania wamepoteza moja ya alama na nguzo ya kupigania usawa wa wanawake na maendeleo ya familia, Mama Fatma Karume, aliyekuwa mke wa rais wa kwanza wa Zanzibar, ungana na Pambazuko kumlilia kwa kutambua mchango wake katika historia ya visiwa hivyo.

Jumanne, 22 Septemba 2026 · 06:56Dakika 2 kusoma
Mama Fatma Karume
Mama Fatma Karume — Picha kutoka Maktaba ya Pambazuko.

ZANZIBAR imegubikwa na majonzi kufuatia kifo cha Mama Fatma Karume, mjane wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, aliyefariki dunia Jumatatu, Septemba 21, 2026. Anatarajiwa kuzikwa leo, Jumatano – Septemba 22, huko Unguja.

Maziko yake yatafanyika kwenye eneo la makaburi ya familia ya Karume, Unguja.

Kifo chake kimeondoa mmoja wa watu waliobeba kwa karibu kumbukumbu za vipindi muhimu vya historia ya Zanzibar, kuanzia harakati za kupigania uhuru, Mapinduzi ya Januari 12, 1964, hadi miaka ya mwanzo ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Rais Samia Suluhu Hassan amesema kifo chake ni pengo kwa familia na Taifa, akimtaja Mama Fatma kuwa sehemu muhimu ya historia ya Zanzibar na Tanzania.

Mama Fatma, aliyepewa jina la Fatma Gullam Hussein Jamal wakati akizaliwa huko Bumbwini, Kaskazini Unguja, aliolewa na Sheikh Karume mwaka 1944 akiwa na umri wa miaka 15. Baada ya Mapinduzi ya 1964, akawa Mama wa Kwanza wa Zanzibar, nafasi aliyoshikilia hadi kuuawa kwa mumewe Aprili 7, 1972.

Asili yake ilikuwa ya mchanganyiko; baba yake alikuwa Mhindi huku mama yake akiwa wa mchanganyiko wa Kiarabu na Kiafrika. Licha ya kutopata fursa ya elimu rasmi shuleni, Mama Fatma alijijengea uelewa mkubwa wa historia na masuala ya jamii, kiasi cha kukumbukwa kwa uwezo wake wa kueleza matukio ya zamani kwa undani.

Katika maisha yake ya umma, alishiriki pia katika harakati za wanawake na kupigania haki yao ya kupiga kura wakati wa ukoloni. Alisimulia namna wanawake walivyoshiriki katika juhudi za kuhakikisha haki hiyo inapatikana Zanzibar.

Mama Fatma pia alikumbukwa kwa shughuli za kijamii, ikiwemo kusimamia na kusaidia maduka ya wajane huko Unguja na Pemba, jambo lililowapa wanawake hao fursa ya kujikimu na kuendelea na maisha baada ya kufiwa na waume zao.

Kwa upande wa michezo, alikuwa na mapenzi makubwa kwa Young Africans Sports Club (Yanga). Uongozi wa klabu hiyo umemtaja kuwa mwanachama na Mjumbe wa Baraza la Wadhamini, huku ukikumbuka mchango wake katika upatikanaji wa ardhi ya makao makuu ya klabu hiyo Jangwani, Dar es Salaam.

Kifo chake kimezua majonzi kwa familia, viongozi na wananchi. Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametuma salamu za pole kwa familia ya Karume na wananchi, huku Klabu ya Yanga nayo ikieleza huzuni kubwa kwa kumpoteza mmoja wa watu waliokuwa na nafasi katika historia ya klabu hiyo.

Hakika kuondoka kwake, Zanzibar imepoteza shahidi muhimu wa historia yake. Mama Fatma Karume ataendelea kukumbukwa kama mwanamke aliyeishi ndani ya historia na, kwa sehemu kubwa, kuwa sehemu ya historia yenyewe.

Bodi, manejimenti na watendaji wote wa Gazeti la Pambazuko tunatoa pole kwa familia na Watanzania wote kwa msiba huu. Alale panapostahili mama huyo aliyelea wengi kwa namna moja ama nyingine.

  • karume
  • kifo
  • tanzia
  • zanzibar

Soma Pia