Tanzia
Tanzania yapoteza mwanadiplomasia Balozi Nicholas Kuhanga
Watanzania wanaomboleza kifo cha Balozi Nicholas Kuhanga ambaye utumishi wake umeacha alama ya kutukuka. Pambazuko linatoa pole kwa familia na Watanzania kwa kifo cha mwanazuoni huyu.

TANZANIA imepata pigo baada ya kifo cha mwanazuoni, mwanasiasa, mwanadiplomasia na kiongozi wa umma, Balozi Nicholas Kuhanga, aliyefariki dunia jijini Dar es Salaam akiwa na umri wa miaka 93.
Balozi Kuhanga, aliyezaliwa Aprili 28, 1933, Songea mkoani Ruvuma, ameacha historia ndefu katika utumishi wa umma, elimu na diplomasia, akihudumu katika nyadhifa mbalimbali muhimu za kitaifa kwa zaidi ya miongo kadhaa.
Kuhanga alianza kujijengea jina katika eneo la elimu, hususan elimu ya watu wazima, na baadaye akaingia katika siasa za kitaifa. Alikuwa Mbunge kati ya mwaka 1965 na 1980 na kushika nafasi ya Waziri wa Kazi na Maendeleo ya Watu mwaka 1975 hadi 1977, kabla ya kuwa Waziri wa Elimu kuanzia 1977 hadi 1980.
Katika kipindi chake serikalini, alishiriki katika juhudi za kupanua elimu nchini, wakati Tanzania ikiwa katika harakati za kuhakikisha fursa za elimu zinawafikia wananchi wengi zaidi. Chuo Kikuu cha Victoria nchini Canada kimemtaja kama mmoja wa waanzilishi muhimu wa maendeleo ya elimu barani Afrika.
Mwaka 1980, Kuhanga aliteuliwa kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), nafasi aliyohudumu hadi mwaka 1988. Katika kipindi hicho alisimamia upanuzi wa programu za kitaaluma, mifumo ya utawala na shughuli za utafiti katika chuo hicho.
Baadaye aliendelea kulitumikia taifa katika sekta ya elimu na kuwa mmoja wa viongozi waliowahi kuhusishwa na uanzishaji wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
Katika nyanja ya diplomasia, Balozi Kuhanga aliteuliwa mwaka 1991 kuwa Balozi wa Tanzania nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), akihudumu Kinshasa hadi mwaka 1995.
Kifo chake kinaacha pengo katika historia ya Tanzania, hasa katika elimu, uongozi wa umma na diplomasia. Ameacha urithi wa utumishi unaokumbusha mchango wa viongozi wa kizazi kilichojenga misingi ya taasisi nyingi za taifa.
Balozi Kuhanga anatarajiwa kuzikwa Jumatano – Septemba 23, jijini Dar es Salaam, huku familia, viongozi na wananchi wakikusanyika kuuaga mwili wa mwanasiasa, mwanazuoni na mwanadiplomasia huyo aliyelitumikia taifa kwa uaminifu na kwa muda mrefu.
- kifo
- kuhanga
- udsm