Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Jicho la Tai

Mbunge kugawa bagia, hajamaliza kazi bado

NIMEMUONA kijana wangu Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Patrick Mwalunenge, akigawa visheti, bagia, soda, machungwa na mihogo ya kuchemshwa kwa wananchi wake.

Jumatatu, 10 Agosti 2026 · 04:15Dakika 2 kusomaToleo 177, uk. 5

Furaha iliyolipuka – wananchi wengi waliokuwepo ilikuwa kubwa kiasi kwamba kwa dakika chache, ilionekana kama vile barabara zote zimewekwa lami, maji yamefika kila nyumba na vijana wote wamepata ajira.

Wananchi wakionekana kushangilia, waligombea soda, wengine wakashika miwa, na wenye bahati wakaondoka na mihogo ya kuchemshwa.

Hakika matumbo kwa waliobahatika kupata mlo, yakatulia na ndimi zikapata utamu wake na hilo likafanya haki-tumbo kutendewa inavyostahili.

Hakika siyo vibaya mbunge kuwakaribia watu wake au kuwapa walau kitafunwa, lakini tatizo huanza pale bagia zinapotaka kupewa hadhi ya daraja, kisheti kuitwa zahanati na soda kuwasilishwa kama sera ya maendeleo.

Wabunge wengi huamini kuwa wanapogawa vitafunwa kwa wananchi, basi hoja zao nazo zimetafunwa na kumalizika. Hawa waheshimiwa hujenga hoja kwamba maendeleo huletwa na serikali, siyo wao.

Wanasahau kwamba miwa huisha utamu, chungwa hubaki maganda na mihogo hushibisha kwa saa chache, lakini ukosefu wa maji, ajira, dawa hospitalini, masoko ya wakulima na barabara nzuri hubaki palepale, ukiwasubiri viongozi wenye mipango na uthubutu.

Ieleweke kuwa kazi ya mbunge siyo kuendesha kantini ya kisiasa, bali mbunge hutumwa bungeni kutunga sheria, kuisimamia serikali, kuhoji matumizi ya fedha za umma na kupigania bajeti inayogusa maisha ya wananchi.

Anatakiwa kujua shida za jimbo lake, kuzipanga kwa vipaumbele na kuzifuatilia kwa uthabiti hadi zipatiwe majibu kutoka serikalini. Hapo ndipo uwakilishi unapogeuka kuwa maendeleo, badala ya onyesho la dakika chache mbele ya kamera.

Wananchi nao wanapaswa kujifunza kutofautisha kati ya zawadi na haki. Kisheti ni zawadi; maji safi ni haki. Bagia ni kitafunwa; shule bora ni haki.

Soda ni burudani; huduma nzuri za afya ni haki.

Chungwa linaweza kufurahisha ulimi leo, lakini mradi wa umwagiliaji unaweza kuilisha nchi kwa miaka mingi.

Kwa hiyo, kila mbunge anapofika na kapu la vitafunwa, wananchi wavitafune kwa furaha washibe, lakini wasisahau kufungua daftari la madai, na kuanza kuhoji ahadi za uchaguzi zimefikia wapi?

Wahoji endapo bajeti ya jimbo imeongezeka kwa kiasi gani? Vijana wameandaliwa mikopo na maeneo ya biashara? Barabara, shule na vituo vya afya vinaendeleaje? Majibu ya maswali hayo ndiyo kipimo cha uongozi.

Mbunge mwenye weledi hafurahii kofi pekee; anatafuta matokeo. Hataki wananchi wawe watazamaji wa ukarimu wake, bali washiriki kwa kupanga maendeleo yao.

Mwakilishi wa wananchi anatakiwa kutumia ubunifu kuvutia uwekezaji, kufungua masoko, kuhamasisha miradi na kuhakikisha serikali inawajibika. Akitoa mihogo, ni vizuri; lakini aeleze pia mkakati wa kuongeza thamani ya mazao ya wakulima.

Mwalunenge na wabunge wengine wakumbuke kuwa wananchi hawakuwachagua kuwa wagawaji wa utamu, bali watetezi wa kesho yao. Vitafunwa vinaweza kujenga ukaribu, lakini haviwezi kuchukua nafasi ya uwajibikaji na mwisho wa muhula, wapigakura hawapaswi kuhesabu visheti walivyokula; wanapaswa kuhesabu miradi iliyokamilika, huduma zilizoboreshwa na fursa zilizopatikana.

Mheshimiwa mimi Mzee Tai, sina shida ukigawa vitafunwa na hata chakula kabisa cha mchana ama jioni, lakini wakati unafanya ukarimu huu hakikisha unachochea kupatikana kwa maendeleo yenye mizizi.

Tambua kuwa tumbo linaweza kushiba leo; historia itakuuliza uliwajengea nini wananchi wako kwa kesho. Maendeleo hayawekwi kwenye sahani; hujengwa kwa mipango, uwajibikaji, ubunifu na matokeo yanayopimika katika maisha ya wananchi wote.

  • Uwakilishi
  • Bunge
  • Uwajibikaji

Soma Pia