Jicho la Tai
Uhamisho wa magavana siyo sabuni ya makosa yao
RAIS Samia Suluhu Hassan alipowaapisha wakuu wa mikoa na makatibu tawala wapya Ikulu Ndogo ya Tunguu, Zanzibar, Septemba 2, 2026, alitoa kauli iliyostahili kusikilizwa na kutafsiriwa mara mbili.
Alisema wakuu wa mikoa ni “jeshi lake,” na kwamba baadhi ya waliohamishwa walikuwa wakilalamikiwa kwa makosa ya kiutendaji na pengine yanayohusu ukiukwaji wa masuala kadhaa ya dhamana zao. Badala ya kuwaondoa, aliwapa nafasi nyingine ya kujirekebisha na hapa ndipo naiona huruma ya mama.
Hata hivyo, kwangu mimi, huruma hii ni njema, lakini maswali hayana huruma. Kwa makosa madogo ya kiutendaji, uhamisho unaweza kuwa nafasi ya kuanza upya.
Kiongozi anaweza kukosea, kujifunza na kubadilika. Hata hivyo, pale taarifa zinazomfikia rais zikihusu tabia zisizofaa, kuingilia majukumu yasiyomhusu au tuhuma nzito, kuhamisha kituo pekee hakumalizi tatizo.
Ni kama kuhamisha pipa linalovuja kutoka sebuleni kwenda jikoni, halafu tukatangaza nyumba imekuwa safi.
Mkoa mpya siyo mashine ya kuosha rekodi, na mwenye tabia mbaya haachi, hasa anapokuwa na umri ulioenda kama hawa magavana wetu.
Ni kwamba wananchi wa Manyara, Lindi, Simiyu, Songwe au Morogoro hawapaswi kuwa maabara ya kupima kama kiongozi aliyelalamikiwa kwingine amebadilika.
Nao wanastahili uongozi bora tangu siku ya kwanza, siyo kusubiri mheshimiwa anayevurunda mahali ili wampokee.
Kama malalamiko yalikuwa ya kawaida, serikali ieleze hivyo. Kama yalihusu uzembe mkubwa, matumizi mabaya ya madaraka, kukosa uadilifu au jambo linaloweza kuwa la jinai, yafanyiwe uchunguzi wa haki na wa wazi.
Atakayebainika hana kosa asafishwe jina.
Atakayethibitika kukiuka maadili awajibishwe.
Na kama kuna ushahidi wa kosa la jinai, vyombo husika vifanye kazi bila kuangalia cheo.
Uhamisho usigeuzwe pazia la kuficha moshi. Natambua kuwa Rais Samia ana mamlaka ya kupanga safu yake na anaweza kuona uhamisho kuwa njia ya kuongeza ufanisi, lakini uongozi wa umma haupaswi kujenga dhana kwamba cheo ni koti linalohamishwa kutoka kabati moja kwenda jingine, hata likiwa na doa.
Uwajibikaji huimarisha taasisi; huruma isiyo na mipaka huzidhoofisha.
Tanzania haijakosa watu waadilifu, wenye elimu, uzoefu na uwezo wa kusimamia mikoa.
Wengi wao hawajawahi kupata nafasi, siyo kwa sababu hawawezi, bali kwa sababu milango huzunguka majina yaleyale.
Kwa nini nafasi ya pili, ya tatu au ya nne apewe anayelalamikiwa, wakati kuna mwingine anayeweza kuanza akiwa na mikono safi na ari mpya? Kiongozi anapopewa nafasi mpya, wananchi wanapaswa kujua amepimwa kwa vigezo gani.
Serikali iweke utaratibu wa kutathmini utendaji wa wakuu wa mikoa kwa matokeo yanayoonekana; huduma, usalama, usafi, miradi, nidhamu ya fedha na namna wanavyowasikiliza wananchi.
Kamwe uteuzi usiwe tu jambo la kuamini moyo wa mteuaji; ujengwe pia juu ya taarifa zinazoweza kupimwa. Zaidi ya yote, utumishi wa umma siyo shule yenye mitihani ya marudio isiyoisha. Kila uamuzi una gharama kwa wananchi, miradi na imani ya taifa. Anayepewa dhamana lazima ajue kuwa kushindwa kuna matokeo, siyo tiketi ya kwenda mkoa mwingine.
Kwa hiyo, naiheshimu huruma ya Rais Samia, lakini tunakumbusha kuwa huruma kwa kiongozi isimame sambamba na haki kwa wananchi. Aliyechemsha kidogo aonywe.
Aliyeshindwa kabisa aondolewe. Anayetuhumiwa achunguzwe. Uhamisho pekee usiwe msamaha wa kimyakimya na ninaamini kuwa taifa haliwezi kuendelea kubadilisha anwani za matatizo na kudhani limebadilisha tabia za watu. Ends.
Umebakiwa na makala 2 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.
- Wakuu wa mikoa
- Uwajibikaji
- Samia Suluhu Hassan