Habari
Mchezaji Hispania kushtakiwa kwa kuua bila kukusudia
Kuna kila dalili kwamba mchezaji wa Hispania ambaye alimgonga mwenzake uwanjani, huenda akafunguliwa mashitaka ya kuua bila kukusudia.

KIPA wa klabu ya FC Andorra, Jesús Owono, huenda akafunguliwa mashtaka ya kuua bila kukusudia, kufuatia kifo cha mshambuliaji wa Tenerife, Jesús de Miguel Alameda (30), aliyefariki baada ya kugongana naye wakati wa mchezo wa Ligi Daraja la Pili nchini Hispania.
Polisi wa Hispania, kupitia kitengo cha uchunguzi wa mauaji, wameanzisha uchunguzi kubaini iwapo Owono anaweza kuwajibishwa kisheria kwa tukio hilo lililotokea Jumatatu, Novemba 2, 2026.
Tukio hilo lilitokea dakika za mwisho za mchezo, wakati Owono alipotoka mbali na lango lake kujaribu kuondoa hatari ya kufungwa bao, lakini goti lake likagonga kifua cha De Miguel.
Mwamuzi alimwonyesha kipa huyo kadi nyekundu kwa kutumia nguvu kupita kiasi katika kuwania mpira. Mshambuliaji huyo alipoteza fahamu na baadaye kufariki hospitalini jana, Novemba 3.
Imeelezwa kwamba polisi wanatarajiwa kuchunguza video za tukio na kuchukua maelezo ya wahusika ili kubaini iwapo kulikuwa na uzembe wa jinai.
Hata hivyo, hakuna ushahidi uliotangazwa unaothibitisha kuwa Owono alimgonga mpinzani wake kwa makusudi. Klabu ya Andorra imekanusha kuwapo kwa nia ya kumdhuru mchezaji huyo.
Mamlaka za mahakama zimeeleza kuwa uchunguzi wa aina hiyo ni utaratibu wa kawaida kwa vifo visivyotokana na sababu za asili.
Iwapo ushahidi utathibitisha uzembe wa jinai, Owono anaweza kufunguliwa mashtaka.
Kwa sasa, hajatiwa hatiani, huku uchunguzi ukiendelea kubaini mazingira halisi ya tukio hilo lililoacha simanzi kubwa katika soka la Hispania.
Umebakiwa na makala 2 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.
- Andorra
- Kifo
- Hukumu
- Hispania