UHARIBIFU WA USIMAMIZI WA MISITU
Miiko ya Waluguru dhidi ya vibali vya serikali, kipi kinaiacha misitu kwenye hatari?
Kwa karne nyingi, miiko na mamlaka za kimila zilisaidia kulinda misitu na vyanzo vya maji vya Milima ya Uluguru. Leo, licha ya sheria na mfumo wa vibali vya uvunaji wa mazao ya misitu, ukataji miti na biashara ya mkaa vinaendelea kushamiri. Uchunguzi wa Christine Haule unaonesha jinsi mgongano wa mamlaka, udhaifu wa usimamizi na gharama za nishati safi unavyochangia kuiacha Kiroka katika hatari ya kimazingira.

MILIMA ya Uluguru, kwa karne nyingi, imekuwa nguzo muhimu ya ikolojia, ikihifadhi misitu, kulinda vyanzo vya maji na kusaidia maisha ya mamilioni ya watu katika maeneo ya Morogoro na kwingineko.
Ulinzi wa misitu hiyo haukutegemea doria za askari wenye silaha, bajeti kubwa za Serikali au sheria zilizochapishwa kwenye magazeti ya serikali. Kwa kiasi kikubwa, ulitegemea mifumo ya jadi ya uhifadhi iliyojengwa katika imani, heshima kwa mazingira na miiko iliyoheshimiwa na jamii ya Waluguru.
Miti, vyanzo vya maji na maeneo fulani ya milimani yalikuwa na hadhi maalumu katika utamaduni wa jamii hiyo. Miiko na mamlaka za kimila zilisaidia kuweka mipaka ya matumizi ya rasilimali hizo na kuwafanya wananchi wajione kuwa sehemu ya wajibu wa kuzilinda.
Lakini leo mfumo huo wa jadi unakabiliwa na mabadiliko makubwa. Nafasi yake imechukuliwa kwa kiasi kikubwa na mfumo wa kisasa wa sheria, vibali na usimamizi wa taasisi za Serikali.
Hata hivyo, kuwepo kwa sheria na vibali hakujazuia uharibifu wa misitu ya Kata ya Kiroka. Badala yake, maswali yanaibuka kuhusu ufanisi wa mfumo huo, namna mamlaka zinavyogawanywa na nafasi ya jamii katika kusimamia rasilimali inayowazunguka.
Utafiti wa mwaka 2025 uliotajwa katika uchunguzi huu unaibua wasiwasi kuhusu athari za kupuuzwa kwa mifumo ya jadi ya uhifadhi. Miongoni mwa changamoto zinazojitokeza ni kuendelea kupatikana kwa mkaa unaozalishwa kwa njia zisizozingatia taratibu, huku bei yake ya chini ikiendelea kuufanya kuwa chaguo kwa watumiaji.
Uchunguzi huu unaonesha kuwa changamoto ya Kiroka si ukosefu wa sheria pekee, bali pia ni mgogoro wa kimamlaka kati ya viongozi wa jamii na watendaji wa Serikali. Hali hiyo inaibua swali muhimu: Je, mfumo wa sasa wa usimamizi wa misitu umeweza kuchukua nafasi ya mifumo ya jadi iliyodumu kwa karne nyingi?
Mgogoro wa mamlaka na ombwe la usimamizi
Kuporomoka kwa misitu ya Kiroka kunazua maswali kuhusu namna mamlaka ya kusimamia rasilimali za misitu yanavyogawanywa kati ya Serikali na jamii zinazoishi karibu na maeneo hayo.
Kwa mujibu wa baadhi ya viongozi wa eneo hilo, sheria za sasa zimeweka mamlaka makubwa ya usimamizi katika taasisi na watendaji wa Serikali, huku nafasi ya viongozi wa jamii na serikali za vijiji ikiwa ndogo.
Diwani wa Kata ya Kiroka, Jamila Taji, anasema mabadiliko hayo yamepunguza uwezo wa jamii kusimamia misitu na vyanzo vya maji ambavyo vimekuwa sehemu ya maisha yao kwa muda mrefu.
“Viongozi wa jamii na serikali za mitaa wamepoteza kabisa nguvu ya kusimamia misitu yetu. Sheria za sasa zinatoa mamlaka makubwa kwa watendaji wa Serikali kutoka wizarani na wilayani. Watendaji hawa mara nyingi wanahamishwa kutoka mikoa mingine; hawaijui historia ya maeneo husika, hawajui vyanzo vyetu vya maji vya kijadi, wala hawana uchungu na uharibifu unaotokea hapa kwa sababu hawaathiriki moja kwa moja,” anasema.
Wakati Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) ukisimamia biashara ya mazao ya misitu kwa mujibu wa Sheria ya Misitu, ikiwemo masharti yanayohusu uvunaji, usafirishaji na utoaji wa leseni, hali inayoripotiwa katika maeneo ya Kiroka inaonesha changamoto za utekelezaji.
Mahitaji ya mkaa katika miji mikubwa, hususan Dar es Salaam na Morogoro, yanaendelea kuweka shinikizo kwa misitu ya maeneo ya uzalishaji. Hali hiyo inahitaji mfumo wa usimamizi wenye uwezo wa kudhibiti uvunaji, kufuatilia usafirishaji na kuhakikisha kuwa vibali vinatolewa kwa kufuata masharti ya sheria.
Kwa wakazi wa Kiroka, tatizo si uwepo wa sheria pekee, bali ni kama sheria hizo zinaweza kutekelezwa kwa ufanisi na kuzuia uharibifu unaoendelea.
Chifu Kingalu: Miiko ililinda misitu kwa karne nyingi
Katika kitovu cha utamaduni wa Waluguru, Chifu Kingalu Mwanabanzi wa 15, anayefahamika pia kama Albert Sabu Kingalu, anaona kupungua kwa nguvu ya mifumo ya kimila kuwa sehemu ya tatizo la uharibifu wa misitu ya Uluguru.
Kwa Chifu Kingalu, kupotea kwa misitu si suala la mazingira pekee, bali pia ni kupotea kwa sehemu ya urithi wa kitamaduni wa Waluguru.
Anasema katika mfumo wa jadi, mtu aliyekata mti katika msitu mtakatifu au kuharibu chanzo cha maji bila idhini ya kimila alikabiliwa na adhabu za kijamii na hofu iliyohusishwa na imani za jamii.
Hali hiyo ilifanya watu waheshimu maeneo yaliyokuwa na umuhimu wa kiutamaduni na kimazingira.
“Leo hii hofu hiyo imetoweka. Watu wanakata miti bila woga wowote, si kwa sababu hawatambui uharibifu wanaofanya, bali kwa sababu wanatembea wakiwa na vibali rasmi mifukoni mwao vilivyosainiwa na mamlaka za kisasa,” anasema Chifu Kingalu.
Anadai kuwa baadhi ya vibali vinavyotolewa bila kuzingatia mazingira ya maeneo husika vinaruhusu wavunaji kuingia ndani zaidi ya maeneo ya misitu na karibu na vyanzo vya maji.
Kwa mujibu wake, hali hiyo inatishia mito na vijito vinavyotiririsha maji kutoka Milima ya Uluguru kwenda kwenye makazi na mashamba ya wananchi wa maeneo ya chini.
Hoja ya Chifu Kingalu inaibua mjadala mpana kuhusu nafasi ya maarifa ya jadi katika usimamizi wa rasilimali za asili. Je, mifumo hiyo inaweza kuunganishwa na sheria za kisasa ili kuongeza uwajibikaji na ufanisi wa uhifadhi?
Wananchi wanahisi gharama za uharibifu
Athari za uharibifu wa misitu hazibaki kwenye takwimu za mazingira. Kwa wakazi wa Kiroka, zinaonekana katika mabadiliko ya upatikanaji wa maji, hali ya kilimo na gharama za maisha.
Uchunguzi katika eneo hilo unaonesha kuwa wananchi wanahusisha kupungua kwa miti na mabadiliko ya mifumo ya mvua. Wanasema mvua hazinyeshi kwa wakati kama ilivyokuwa zamani, huku baadhi ya maeneo yakikumbwa na mvua kubwa zinazochochea mmomonyoko wa udongo.
Kupungua kwa unyevu na rutuba ya ardhi pia kunatajwa kuathiri uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, na kuongeza changamoto kwa wakulima wanaotegemea kilimo kujipatia kipato.
Mabadiliko hayo yanaathiri zaidi kaya zenye kipato cha chini, ambazo zina uwezo mdogo wa kukabiliana na kupanda kwa gharama za maisha na kupungua kwa uzalishaji.
Katika upande mwingine, mahitaji ya nishati ya kupikia yanaendeleza mzunguko wa utegemezi wa mkaa. Wananchi wanaojua umuhimu wa misitu wanakiri kuwa gharama za nishati mbadala bado ni kikwazo.
Hawa Michael, mama lishe katika Wilaya ya Morogoro, anasema analazimika kutumia mkaa kutokana na gharama kubwa za gesi ya kupikia.
Anasema baadhi ya wananchi waliwahi kupata majiko ya gesi ya mitungi midogo kwa Sh19,000, yakiwa na gesi. Hata hivyo, baada ya gesi hiyo kuisha, gharama za kujaza mitungi zilipanda na kufikia Sh29,000, hali iliyowafanya baadhi ya watumiaji kushindwa kuendelea nayo.
Anasema baadhi ya wananchi waliishia kuuza majiko hayo au kuyatumia kwa shughuli nyingine kwa sababu hawakuweza kumudu gharama za kujaza gesi.
“Tunatumia mkaa kwa sababu gesi ni ghali, lakini tunajua misitu inaisha,” anasema.
Hawa anasema Serikali inapaswa kuendelea kutoa elimu kuhusu uhifadhi wa mazingira na kuimarisha upatikanaji wa nishati safi kwa gharama zinazomudu wananchi wa kipato cha chini.
Anasisitiza pia umuhimu wa kuhamasisha jamii kuepuka uchomaji moto misitu, ukataji holela wa miti na uzalishaji wa mkaa usiozingatia taratibu.
Kwa hiyo, tatizo la matumizi ya mkaa haliwezi kutatuliwa kwa kuhimiza wananchi waache nishati hiyo bila kuweka njia mbadala wanazoweza kumudu.
Kilimo nacho kinakabiliwa na athari
Salehe Mkiki, mkulima na mkazi wa Kiroka, anasema juhudi za uhifadhi wa mazingira katika maeneo yao bado hazijawa za kutosha.
Anasema baadhi ya maeneo ya milimani yamepoteza uoto wa miti na kubaki wazi, hali ambayo wananchi wanahusisha na mabadiliko ya mvua na kupungua kwa uzalishaji wa mazao.
“Maeneo mengi ya milima sasa yanaonekana kuwa wazi, bila miti. Mvua zimebadilika na hata mazao hayastawi tena kama zamani,” anasema.
Mkiki anaiomba Serikali kuwapatia wananchi miche na mbegu za miti ili waweze kurejesha uoto wa asili na kuimarisha uhifadhi wa mazingira.
Kwa wakulima kama Mkiki, upandaji miti si suala la kurejesha mandhari ya kijani pekee, bali pia ni uwekezaji katika kulinda ardhi na mifumo ya maji inayotegemewa na kilimo.
Serikali za vijiji zimefungwa mikono?
Changamoto nyingine inayojitokeza katika uchunguzi huu ni uwezo mdogo wa serikali za vijiji na kamati za mazingira kushiriki katika maamuzi kuhusu vibali vya uvunaji wa mazao ya misitu.
Kwa mujibu wa hoja zilizotolewa na viongozi wa eneo hilo, hata pale ambapo viongozi wa vijiji wanapobaini uvunaji unaoweza kuathiri misitu yao, uwezo wao wa kuingilia kati unaweza kuwa mdogo iwapo mvunaji ana kibali kilichotolewa na mamlaka ya juu.
Hali hiyo inaibua maswali kuhusu nafasi ya serikali za vijiji katika kutoa maoni, kufuatilia utekelezaji wa vibali na kuripoti ukiukwaji wa masharti.
Wakati mvunaji anapofika kijijini akiwa na kibali chenye nembo ya Serikali na saini ya afisa husika, kamati za mazingira zinaweza kujikuta katika nafasi ngumu ya kuhoji uhalali wa shughuli hiyo.
Huu ni udhaifu unaoweza kujitokeza pale mfumo wa usimamizi unapokuwa wa kutoka juu kwenda chini bila kuweka utaratibu madhubuti wa kushirikisha jamii zinazozunguka misitu.
Kwa wakazi wa Kiroka, suluhisho haliwezi kuwa kuongeza doria au kuandika sheria kali zaidi pekee. Wanataka pia jamii na viongozi wa kimila washirikishwe katika maamuzi na usimamizi wa rasilimali hizo.
Miongoni mwa mapendekezo yanayotolewa ni kuimarisha mamlaka ya kimila kwa kuweka utaratibu wa kisheria unaotambua mchango wa viongozi kama Chifu Kingalu na wazee wa jamii katika kusimamia misitu na vyanzo vya maji vinavyohusishwa na mila za Waluguru.
Hata hivyo, ushirikishwaji huo unahitaji kuwekwa katika mfumo unaoeleweka, wenye uwajibikaji na unaozingatia sheria za nchi, ili kuzuia migongano ya mamlaka na kuhakikisha rasilimali zinalindwa kwa manufaa ya jamii nzima.
FAO yaunga mkono usimamizi na nishati safi
Katika juhudi za kukabiliana na uharibifu wa misitu na kuimarisha matumizi endelevu ya rasilimali, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya kupitia mradi wa CookFund, limeendesha mafunzo kwa wataalamu wa misitu kutoka TFS na wadau wengine.
Mafunzo hayo yanalenga kujenga uwezo wa usimamizi wa misitu, kuhakikisha uvunaji wa mazao ya misitu unazingatia taratibu za kisera na kisheria, na kusaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Afisa Programu wa FAO, Diomedes Kalisa, anasema shirika hilo linaunga mkono juhudi za kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa kama nishati ya kupikia na kuhamasisha matumizi ya nishati safi.
Anasema matumizi ya rasilimali za misitu kwa ajili ya nishati ya kupikia yanaweka shinikizo kubwa kwa misitu nchini, hivyo kuna umuhimu wa kuimarisha njia mbadala za nishati.
Kwa Kiroka, suluhisho linahitaji zaidi ya sheria na vibali. Linahitaji mfumo unaounganisha usimamizi wa Serikali, ushiriki wa jamii, maarifa ya jadi na upatikanaji wa nishati safi kwa gharama zinazomudu wananchi.
Mchanganyiko wa sheria za kisasa na mifumo madhubuti ya miiko ya jadi unaweza kuwa sehemu muhimu ya kurejesha ulinzi wa misitu ya Uluguru. Lakini ili hilo lifanikiwe, mamlaka zinapaswa kuondoa mianya ya usimamizi, kuimarisha uwajibikaji na kuhakikisha wananchi wana nafasi halisi katika maamuzi yanayohusu rasilimali wanazozitegemea.
Hatimaye, swali si kama Tanzania ina sheria za kulinda misitu. Swali ni kwa nini, licha ya sheria hizo, misitu ya Kiroka inaendelea kuwa hatarini - wakati jamii iliyoirithi imekuwa na mifumo ya kuilinda kwa vizazi vingi.
Umebakiwa na makala 2 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.
- Kiroka
- Milima ya Uluguru
- Misitu
- Mkaa
- Waluguru
- TFS
- Uhifadhi
- Nishati Safi
- Mabadiliko ya Tabianchi
- Mazingira
- Vibali vya Misitu